Uchaguzi wa mikoa nchini Ufaransa
Wafaransa wamethibitisha ,jana,katika duru ya pili ya uchaguzi wa mikoa,upinzani wao dhidi ya chama cha mrengo wa kulia cha rais Nicolas Sarkozy anaetazamiwa kulifanyia mageuzi baraza la mawaziri.
Waziri mkuu Francois Fillon amekwenda katika kasri la rais la Elysee kuzungumzia uwezekano wa kufanyiwa marekebisho baraza la mawaziri baada ya pigo kubwa walilopata wafuasi wa UMP na washirika wao katika uchaguzi wa mikoa.Kabla ya hapo waziri mkuu Francois Fillon alisema "atabeba sehemu yake ya jukumu" kufuatia duru hiyo ya pili ya uchaguzi ambayo mawaziri wake 20 walikua miongoni mwa wagombea.
Mrengo wa shoto na washirika wake -walinzi wa mazingira,wataendelea kuongoza katika idadi kubwa ya mikoa ya Ufaransa baada ya kujinyakulia asili mia 53,85 ya kura dhidi ya asili mia 35 walizopata wafuasi wa chama cha rais Sarkozy UMP na washirika wake.
Asili mia 48.8 hawajateremka vituoni;hata hivyo idadi hiyo ni ndogo ikilinganishwa na asili mia 53.6 mnamo duru ya kwanza.
Chama cha siasa kali za mrengo wa kulia,Front National kitawakilishwa katika mikoa 12 kwa kujikingia asili mia 9 katika daraja ya taifa.Katika mkoa wa kaskazini Front national kimejikingia asili mia 22 ya kura na huenda idadi ya wapiga kura ikawa kubwa zaidi katika mkoa wa kusini-ambao ndio ngome ya kiongozi mkongwe wa chama hicho kinachopalilia chuki dhidi ya wageni,Jean Marie Le Pen.
Baada ya pigo la jana,baadhi ya vigogo vya UMP,ikiwa ni pamoja na mkuu wa kundi la wabunge wa UMP,Jean Francois Copé wameanza kupaza sauti kuzungumzia umuhimu wa "mkataba mpya wa walio wengi."
Kwa upande wao wafuasi wa mrengo wa shoto na washirika wao wanajivunia ushindi.Mwenyekiti wa chama cha kisoshialisti Martine Aubry anasema:
Tutaanza kuwajibika moja kwa moja katika mikoa,ili kutekeleza ahadi za uchjaguzi tulizotoa.Kwaajili ya kubuni nafasi za kazi na kwaajili ya mustakbal wa vijana wa nchi yetu.Hatutopoteza hata dakika moja,tukizingatia changamoto hizi kunwa zinazotukabili.
Uchaguzi huu umefanyika katika wakati ambapo umaarufu wa rais Nicolas Sarkozy umekua ukipungua sana mnamo miezi ya hivi karibuni.Kwa kujipatia ushindi mkubwa wafuasi wa mrengo wa shoto,chama cha kishosialisti kimeanza upya kujipuka na Martine Aubry kuvalia njuga kuweza kuchaguliwa kama rais mnamo mwaka 2012.
0 comments