IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
SPIKA wa Bunge, Samuel Sitta, ni mmoja wa viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wenye wakati mgumu katika harakati za kurejea bungeni, kutokana na mashambulizi yanayoelekezwa kwake kutoka ndani na nje ya CCM, Tanzania Daima Jumapili imebaini.
Kwa takriban wiki mbili hivi sasa, Sitta amekabiliwa na upinzani mkali ambao wachambuzi wanadai ni jitihada za washindani wake kuzima tambo zake na dhamira yake ya kurejea bungeni au katika uspika, baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Habari ambazo Tanzania Daima Jumapili imezipata kutoka kwa makada wa CCM zinadai kuwa kiongozi huyo wa Bunge anaweza kutoswa katika mapendekezo ya chama chake kuwania nafasi hiyo kwa sababu ya msimamo wake wa kupambana na ufisadi, ambao nusura uiangushe serikali.
Sitta anadaiwa kuwa amekuwa akishabikia mijadala ambayo ilikuwa ikizidisha chuki na makundi ndani ya CCM pamoja na kuruhusu serikali inayoongozwa na chama chake ishambuliwe na wapinzani pamoja na makada wenzake.
Wakati kiongozi huyo akionekana kupata kukabiliana na upinzani ndani ya chama chake, limezuka kundi la viongozi wa upinzani likimshambulia Sitta kwa kubainisha kuwa hawezi kupambana na ufisadi.
Juzi Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia, alisema Spika Sitta hawezi kuwa mpambanaji wa ufisadi wakati rekodi yake inaonyesha kuwa ni miongoni mwa kundi hilo ambalo limesababisha nchi kuwa maskini na maisha ya watu kuwa magumu kadiri siku zinavyosonga mbele.
Mbatia alimtaka Sitta aondoke CCM kama anataka kupambana na ufisadi, vinginevyo watu wataanza kuamini tuhuma mbalimbali zinazohusishwa na Sitta, kama vile madai ya yeye kuhusishwa na uchotaji wa kiasi cha shilingi milioni 200 na kuzipeleka katika Jimbo lake la Urambo Mashariki, pamoja na kukubali kupangishiwa nyumba yenye thamani ya shilingi milioni 10 kwa mwezi.
Kabla ya kuibuka kwa Mbatia, Mwenyekiti wa TLP, Agustine Mrema, naye alishamshutumu Spika Sitta kuwa hana dhamira ya kweli ya kupambana na ufisadi kwa kuendelea kubakia ndani ya CCM.
Hata hivyo shutuma hizo za Mrema zilijibiwa na Sitta, akisema Mrema amefilisika kisiasa na kifedha, na kwamba anapewa pesa kuipigia debe CCM, hasa Rais Jakaya Kikwete.
Baadhi ya wachunguzi wa masuala ya siasa waliozungumza na Tanzania Daima Jumapili, wamebainisha kuwa Sitta ataandamwa na kila aina ya tuhuma katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Walibainisha kuwa tabia hiyo ya kuanza kuzushiwa baadhi ya mambo iliyoanza kuibuka hivi sasa, ni sawa na ile ya mwaka 2005, ambapo makundi yaliyokuwa yakiwaunga mkono wagombea wa nafasi ya urais ndani ya CCM walikuwa wakiitumia dhidi ya wapinzani wao.
Wameweka wazi kuwa mwaka huu nafasi za ubunge zitakuwa na upinzani mkali, hasa baada ya kutokea kwa kashfa mbalimbali zilizowahusisha wabunge na mawaziri ambao wengine wameshang’oka madarakani.
Sababu kubwa waliyoielezea ni kuwa makundi ndani ya CCM yamejengeana chuki, licha ya juhudi mbalimbali za kuwasuluhisha kuendelea kila kukicha.
Sitta amekuwa miongoni mwa vigogo wa CCM wanaosemekana kuwa na kundi kubwa la makada wanaotaka baadhi ya wanachama wenzao wang’olewe ndani ya chama kwa madai ya kushiriki katika vitendo vya ufisadi.
Mara kadhaa kumekuwepo na taarifa za kuandaliwa kwa mikakati kabambe ya kumng’oa Sittta madarakani, likiwemo jaribio la baadhi ya wajumbe katika mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) uliofanyika mwaka jana kupendekeza anyang’anywe kadi ya uanachama.
Taarifa za kiongozi huyo kutaka kuvuliwa unachama kwenye NEC, zilithibitishwa na yeye mwenyewe (Sitta) hivi karibuni alipokuwa akitoa risala kwenye harambee ya kidini, ambapo aliweka wazi kuwa ukweli wake wa kuwaumbua mafisadi ulihatarisha uanachama wake.
Aidha Sitta, mara kadhaa amenukuliwa na vyombo vya habari akiwalalamikia baadhi ya makada wenzake kwa kutembeza fedha na kuwafadhili wapinzani wake jimboni kwake kwa lengo kutaka wananchi wasimchague.
Zipo taarifa kuwa moja ya makundi ya CCM linahusishwa na jitihada za kumng’oa Sitta bungeni, na linatumia nguvu zote, wakiwamo ‘mamluki’ kummaliza kisiasa.
Swali kubwa linaloonekana kuwaumiza vichwa wachambuzi wa masuala ya siasa, ni kama Sitta ataweza kurejea katika kiti chake, hasa baada ya kutamba bungeni kwamba ana uhakika wa kukalia kiti hicho baada ya uchaguzi wa mwaka huu.
You Are Here: Home - - CCM kumtosa Sitta?
0 comments