Rais Jakaya Kikwete
VIGOGO wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wenye ubavu wa kumvaa Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, wataanza kujulikana Julai Mosi, mwaka huu, takriban siku 23 kabla ya kuvunjwa rasmi kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeelezwa wiki hii mjini Dodoma.
Wagombea hao wa urais watatakiwa kuchukua fomu na kuzirejesha siku saba baadaye, yaani Julai 8 mwaka huu na majina yao yatafikishwa kwenye Mkutano Mkuu wa CCM, Julai 18, mjini Dodoma, kwa ajili ya uteuzi, ikiwa ni siku mbili baadaye, baada ya mgombea urais wa Zanzibar kuteuliwa na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC).
Mteule wa kugombea urais Zanzibar tofauti na urais wa Jamhuri, hutangazwa na NEC ambayo safari hii katika kumpata Rais wa saba wa Zanzibar, itafanya kazi hiyo Julai 16, 2010.
Katika nafasi za kugombea urais wa Muungano ni Mbunge wa Maswa pekee, John Shibuda ndiye aliyetangaza nia ya kutaka nafasi hiyo na kwa upande wa urais wa Zanzibar, viongozi kadhaa wanatajwa akiwamo Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohammed Shein, Waziri Kiongozi Shamshi Vuai Nahodha na Naibu Waziri wa Afrika Mashariki, Mohamed Aboud Mohamed.
John Shibuda
Wengine wanaotajwa kuwania kuongoza Visiwani ni Naibu Waziri Kiongozi, Juma Shamuhuna, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Muungano, Muhammed Seif Khatibu na aliyekuwa Waziri Kiongozi, Dk. Gharib Bilali.
Kwa upande wa Bunge, litavunjwa rasmi Julai 23, mwaka huu takriban miezi mitano ijayo, mapema zaidi kuliko ilivyokuwa ikifanyika awali.
Wakati Bunge hilo likivunjwa Julai 23, wabunge wa CCM wenye kutaka kutetea nafasi zao watapaswa kuchukua fomu kwenye chama chao siku tatu baada ya Bunge kuvunjwa, yaani Julai 26 na kulazimika kurejesha fomu hizo siku mbili baadaye, yaani Julai 28.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa saa nane usiku wa kuamkia Jumanne, wiki hii, mjini Dodoma na Katibu wa NEC- Itikadi na Uenezi, Kapteni mstaafu John Chiligati, siku hizo za uchukuaji na urejeshaji fomu kwa wanaotaka kuwania ubunge kwa tiketi ya CCM zinawahusu pia wagombea wa ujumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar.
Akizungumzia kuhusu madiwani, Chiligati aliwaambia waandishi wa habari kuwa wagombea watachukua fomu Julai 10 na kuzirudisha Julai 14 na kwamba kuanzia Julai 31 hadi Agosti 7, ni siku za wagombea ubunge, uwakilishi-Zanzibar na udiwani kufanya kampeni kwenye matawi ya chama hicho.
“Watapiga kura za maoni katika matawi yote nchini Agosti 8, kwa wagombea wote wa ubunge, uwakilishi na udiwani.
Akifafanua kuhusu kura za maoni, alisema NEC imehimiza kila wanachama wa CCM kujiorodhesha kwenye daftari la wanachama katika tawi lake na mwisho wa kujiorodhesha ni Julai 30, mwaka huu na baada ya hapo upokeaji wanachama wapya utasitishwa hadi mchakato wa kura za maoni uhitimishwe.
“Watakaopiga kura za maoni ni wale tu watakaokuwa wamejiandikisha kwenye daftari katika tawi,” alisema Chiligati na kuongeza kuwa wagombea wote wa ubunge bila kujali nyadhifa zao za sasa watatembezwa wakati wa kuomba ridhaa kwa wanachama kwa kutumia magari ya chama yatakayokodiwa na watakula chakula kilichoandaliwa na chama.
“Hatutaki mtu ashindwe kugombea au kufanya kampeni za kuomba kura za maoni kwa kuwa hana gari kama mwingine, hana pikipiki au baiskeli. Wote watatumia usafiri wa chama, chakula cha chama na watazunguka pamoja, katika kila tawi ambako kila mmoja atajieleza,” alisema Chiligati.
Katika hatua nyingine, NEC imekata mzizi wa fitina na hasa malumbano yaliyoanzia katika Umoja wa Wanawake (UWT) wa chama hicho wa kutaka Wabunge wa Viti Maalumu waliokaa kwa mihula zaidi ya miwili kuachia nafasi hizo ama wakagombee kwenye majimbo au wajiengue kabisa kwenye ubunge.
Katika uamuzi wake wa sasa, NEC imekubali Viti Maalumu iwe na ukomo wa mihula miwili lakini utaratibu huo utaanza rasmi kutumika mwaka 2015, ili wahusika wa sasa wajiandae, ikiwa ni kinyume na alivyotarajia Mwenyekiti wa UWT, Sophia Simba, aliyekuwa akipigania utaratibu huo uanze, katika uchaguzi wa mwaka huu.
0 comments