WAUMINI wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship wamepiga kambi ya saa 24 kanisani kwao Mwenge, Dar es Salaam, kulizuia Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kupitisha umeme wa msongo mkubwa wa kilovolti 132 mbele ya kanisa lao.
Waamini hao wanaume kwa wanawake, tangu jana wamepeana zamu kwa kupangiana makundi ya kuikabili TANESCO usiku na mchana.
Ujumbe mzito wa kanisa hilo kwa shirika hilo la umeme umewekwa wazi katika fulana maalumu walizovaa, zenye maandishi ya maonyo na kejeli yasomekayo: “TANESCO muogopeni Mungu” (mbele) na “Baada ya Richmond mmegeukia Kanisa” (nyuma).
Akizungumzia tukio hilo huku akiwa amezungukwa na waamini hao, Askofu Mkuu, Zakary Kakobe, alisema wamefikia uamuzi huo baada ya shirika hilo kutoa taarifa kwamba kazi ya kupitisha nyaya hizo itaanza mapema mwezi huu na kwamba wametengeza fulana zaidi ya 50,000 ili waamini wakataokuwa kwenye kambi hiyo waweze kutambulika.
“Waamini wamevaa fulana hizo ili kujitofautisha na wapitanjia na kuanzia leo watapiga kambi ya saa 24 huku wakibadilishana zamu za kuingia na iwapo TANESCO watafika mahali hapa kwa ajili ya kuanza kazi hiyo itakuwa rahisi kukabiliana nao.
“Tumeamua kufanya hivyo maana taarifa ya TANESCO ilieleza kuanza kazi mwanzoni mwa mwezi huu, hivyo waamini watakuwepo wakati wote mahali hapa,” alisisitiza.
Askofu Kakobe alisema uchunguzi waliofanya umebaini kuwa ufisadi wa mkataba tata wa kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Richmond umerudishwa kwa mfumo mwingine ambao kwa sasa unataka kuwalaghai wananchi wanyonge.
“Huu umeme ulikuwa upitishwe upande wa pili wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kule wakakutana na wasomi ambao walitoa athari za nyaya hizo na kuishauri TANESCO ijaribu kupitisha chini ya ardhi, lakini wakaogopa gharama,” alisema.
Kakobe alisema baada ya TANESCO kuona imeshindikana walihamia upande wa pili (wa kanisa) ambako walijua Walokole ni wanyonge na kwamba wataishia kuingia kanisani na kupiga magoti wakikubali madhara hayo yawafike.
“Hili suala tumelichunguza kwa mapana tumegundua kuwa ule ufisadi wa Richmond umerudi kwa njia tofauti, hivyo tumeweka kambi mahali hapa kuanzia sasa kwa kupokezana na tutakuwa tayari kukabiliana nao, lakini si kwa silaha,” alisema Askofu Kakobe.
Aidha, Kakobe alihoji iwapo umeme huo hauna madhara, inakuwaje TANESCO wang’ang’anie kuvunja mabango ya kanisa yenye urefu wa mita 13 huku nguzo zinazobeba umeme huo zikitakiwa kuwa na urefu wa mita 23.
Alisema baadhi ya wananchi wamekuwa kimya kwa kutopinga upitishaji wa umeme huo zikiwepo taarifa zisizo rasmi kuwa wamekwishalipwa fidia ya sh milioni 100 hasa kuanzia maeneo ya Ubungo.
Hata hivyo alieleza wamejipanga vilivyo kukabiliana na upitishwaji wa umeme huo kwani kuna uwezekano hapo baadae kuja kubomoa eneo la mbele la kanisa hilo ukiachana na mabango.
“Sisi tunafahamu kinachotaka kufanyika hapa, ndiyo maana tumeamua kujipanga. Lazima wajiulize mbona kipindi cha ujenzi wa barabara hatukupingana na wakala wa barabara Tanroads? Wakati wa upanuzi tulitoa ushirikiano mkubwa. Tulifanya hivyo kwa kuwa walitushirikisha kabla hawajaanza,” alisema.
Pamoja na mambo mengine, askofu huyo alisema uchunguzi waliofanya umebaini kuwa serikali imepanga kunyanyasa baadhi ya makanisa.
“Wamezoea kusema kuwa Kardinali Pengo ni mlima, eti Kakobe ni kichuguu ndiyo maana kama lingekuwa kanisa lake wasingeligusa, sasa napenda kuwaeleza kuwa Kakobe si mlima Kilimanjaro tu bali ni Everest,” alisisitiza.
Alisema anashangazwa na maelezo yanayotolewa na TANESCO kuwa upitishaji wa umeme huo ni kwa ajili ya jamii, huku kwa upande mwingine wanaharibu maendeleo yaliyofanywa na jamii hiyo hiyo.
Hata hivyo, alisema katika kipindi hiki Watanzania wanatakiwa kuwa makini na propaganda zinazotolewa na baadhi ya viongozi wa serikali, kwani nyingi zina madhara.
Alitoa mfano kuwa wakati wa uingizwaji wa dawa za uzazi wa mpango, kinamama walielezwa hazina madhara, lakini baada ya kutumia wakaelezwa kwamba zina madhara.
Mfano huo aliufananisha na upitishaji wa umeme huo ambao kwa sasa TANESCO wanasisitiza hauna madhara, lakini itafika kipindi watatangaza madhara ya umeme huo kwa watu wanaoishi jirani.
Alisema hawako tayari kukubali upitishwaji wa umeme huo, akaongeza kwamba hata Wajapan waliofadhili mradi huo hupitisha miundombinu kabla ya wananchi kuingia katika eneo husika.
“Nimetembea nchi nyingi ikiwemo Japan, tena kule kwao miundombinu hupitishwa kabla ya wananchi kuanzisha makazi. Sasa iweje hapa nchini wapitishe wakati tayari kuna watu wanaishi katika maeneo hayo?” alihoji Kakobe.
Hivi karibuni TANESCO lilitoa taarifa ikiwaondoa hofu waamini wa kanisa hilo kwamba hawataathiriwa na upitishaji wa umeme huo mradi ambao umefadhiliwa na Serikali ya Japan.
0 comments