Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Zitto aifadhili NCCR-Mageuzi kupitia kwa Kafulila

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
Zitto aifadhili NCCR-Mageuzi kupitia kwa Kafulila
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe, ambaye anamuunga mkono aliyekihama chama hicho.
Na Elizabeth Ernest

NAIBU Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe ametangaza kumuunga mkono swahiba wake David Kafulila kugombea ubunge jimbo la Kigoma Kusini kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi na tayari ametoa magari matatu kwa ajili ya kumsaidia kujiimarisha jimboni huko.

Vyanzo vya habari vya kuaminika kutoka kwa watu walio karibu na Zitto na Kafulila vinasema kwamba, kiongozi huyo wa Chadema ameamua kumuunga mkono Kafulila ili kuhakikisha jimbo hilo linaondoka mikononi mwa CCM na kwenda upinzani.

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, NCCR-Mageuzi ilishika nafasi ya pili huko Chadema ikishika nafasi ya tatu kwenye matokeo ya ubunge. Katika uchaguzi wa mwaka 2000, jimbo hilo lilichukuliwa na NCCR-Mageuzi kabla ya 2003 kuchukuliwa na CCM katika uchaguzi mdogo.

Katika uchaguzi wa serikali za mitaa wa hivi karibuni, Chadema kilijizolea viti 12, NCCR-Mageuzi 11 na CCM kilipata viti 20. Kulingana na takwimu hizo, upinzani uliongoza.

Mwaka 2005 kama Chadema ambacho kilishika nafasi ya tatu kingeiunga mkono NCCR-Mageuzi, Jimbo hilo sasa lingekuwa katika mikono ya upinzani kwa kuwa kura za kambi hiyo zilikuwa nyingi kuliko za CCM.

Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, Zitto anaamini kwamba, Kafulila ndiye aliyejenga Chadema kama chama ikiwa ni pamoja na kuimarisha mahusiano na NCCR-Mageuzi katika maeneo ambayo chama hicho kina nguvu.

“Zitto amekwisha weka bayana kuwa katika Uchaguzi Mkuu ujao upande wa jimbo hilo anamuunga mkono Kafulila kwa kuwa anaamini atashinda na kuimarisha upinzani,” kilisema chanzo cha kuaminika.

Maelezo hayo ya Kabwe yamekuja huku Kafulila akijiandaa kwenda jimboni humo kuhutubia mikutano ya hadhara akitumia magari ya Zitto.

Habari zilizolifikia gazeti hili jana zinasema kuwa Kafulila ambaye sasa ni mwanachama wa NCCR-Mageuzi ataanza ziara yake mkoani humo Desemba 8, mwaka huu akiwa na viongozi wa kitaifa wa NCCR-Mageuzi.

Kwa mujibu wa habari hizo, Kafulila pia anatarajia kuzungumza na wanachama wa Chadema mkoani Kigoma na kuzunguka maeneo mbalimbali kwa magari ya Zitto ambaye ni mbunge wa Kigoma Kaskazini.

Kafulila aliliambia gazeti hili jana kuwa atatumia magari ya Zitto kwa kuwa ni rafiki yake wa karibu.

“Mimi na Zitto ni marafiki wa siku nyingi, tayari nimezungumza naye na amekubali kunisaidia kama rafiki yake wala sijakodisha," alisema Kafulila jana na kuongeza:

"Amenipa magari yake kwa ajili ya usafiri kwa sababu nitaondoka na watu wangu huku Dar kwenda Kigoma”.

Alifafanua kuwa jambo kubwa analokwenda kufanya Kigoma ni kuwaeleza wanachama wa Chadema sababu zilizomwondoa kwenye chama hicho na hatima yake kisiasa.

Zitto hakupatikana jana kuzungumzia ufadhili wake kwa Kafulila na taarifa iliyopatikana kutoka kwenye familia yake ilieleza kuwa yuko masomoni Ujerumani.

Alipoulizwa kuhusu magari hayo, mama wa mzazi Zitto, Shida Salum alisema kuwa Kafulila na Zitto ndio wanaostahili kuzungumzia suala hilo.

"Mimi siwezi kusema chochote, hawa ni marafiki nadhani wenyewe ndio wanaoweza kuzungumza zaidi," alisema.

Awali mmoja wa wanachama wa Chadema atakayekuwa katika ziara hiyo ambaye hakutaka kutajwa gazetini, alieleza kuwa msafara huo utakuwa na magari manane; matatu ya Zitto Kabwe na magari matano ya NCCR-Mageuzi

"Magari hayo yatabeba watu mbalimbali wakiwemo wanachama wa Chadema zaidi ya 50 ambao watatangulia kwa ajili ya kwenda kuandaa mazingira ya kumpokea Kafulila na msafara wake na katika maandamano maalum yaliyoandaliwa kwa ajili yake," alisema mwanachama huyo na kuongoza:

"Kimsingi Kigoma yote hakuna mwanachama wa Chadema aliyefurahishwa na kitendo kilichofanywa na viongozi wa chama hicho kuwaengua na wote wana hamu kubwa kumsikiliza Kafulila".

Alisema katika ziara hiyo, wanachama hao wanatarajia kurudisha kadi za Chadema na kujiunga rasmi na chama cha NCCR-Mageuzi.

Takribani wiki moja na nusu iliyopita, Dk Slaa alifuta nyadhifa za afisa habari wa chama hicho, David Kafulila pamoja na Afisa Mwandamizi wa Bunge na Halmashauri, Danda Juju na kuwa wanachama wa kawaida ambapo baada ya uamuzi huo, Kafulila na Juju kwa nyakati tofauti walitangaza kujiengua katika chama hicho huku Kafulila akijiunga na Chama cha NCCR-Mageuzi.

Kafulila na Juju walifutwa nyadhifa zao kwa madai kuwa walikuwa wakitoa habari za chama hicho kwa vyombo vya habari kinyume na taratibu, jambo ambalo walilipinga vikali na kudai kuwa walifanyiwa hivyo kwa kuwa walikuwa mstari wa mbele kuzungumza ukweli na kutetea haki kwa maslahi ya chama.

Habari hizo zilidai kuwa katika mazungumzo hayo, Dk Slaa alisema kitendo cha Mbowe kumtaka atekeleze agizo lake la kuwafuta uanachama Kafulila na Juju amemfanya aeleweke vibaya kwa watu wake wa karibu.

Habari zilifafanua kuwa Dk Slaa alimweleza Mbowe kuwa shughuli nyingi ndani ya chama hicho anazifanya kwa kujitolea na kwamba kama ni Ubunge angeweza kuupata hata kama angekuwa mwanachama wa chama kingine na kusisitiza kuwa anayoshutumiwa na watu kuhusu uamuzi wa kuwavua nyadhifa Kafulila na Juju aliujua kabla.

Tangu Juju na Kafulila watangaze kujitoa Chadema, Mbowe hajawahi kuzungumza lolote licha ya tuhuma zilizotolewa dhidi yake ambazo zilipigiliwa msumali na Juju ambaye alidai kuwa kama Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za serikali(CAG) atakikagua chama hicho na kukuta mambo shwari atakuwa tayari kwenda jela.

Habari zaidi zilieleza kuwa mara baada ya kikao hicho, Dk Slaa wakati anatoka alikutana mlangoni na Muasisi wa chama hicho na Gavana wa kwanza mzalendo Benki Kuu ya Tanzania, Edwin Mtei alimwomba wazungumze, lakini Dk Slaa alisisitiza kuwa ana safari ila baada ya kuombwa kwa muda mrefu na Mtei alikubali. Inadaiwa kuwa mazungumzo yao yalidumu kwa saa mbili.

Habari hizo zilieleza kuwa maofisa wawili wa juu wa chama hicho (majina tunayo) wako katika hatua za mwisho za kujivua uanachama na inadaiwa kuwa mmoja wao ameshaandika barua ya kujivua uanachama kwa madai kuwa mchango wake katika chama umekuwa hauthaminiwi na kwamba shughuli zake nyingi zimekuwa zikifanywa na Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa Chama hicho, John Mnyika.

Mwananchi lilipomtafuta Dk Slaa kuzungumzia suala hilo, alisema kuwa chama hicho hakiwezi kukaa na kujadili masuala ya Kafulila na Juju kwa madai kuwa ni ya kipuuzi.

“Hivi wewe una cheti kweli cha uandishi wa habari. Nikuulize swali kwamba, hapo kwenu Mwananchi wamefukuzwa watu wangapi tena bila hata uongozi kujua mbona hamuandiki, Chadema tuna mambo mengi ya msingi ya kuzungumza hatuwezi kukaa na kujadili suala la Kafulila na Juju” alisema Dk Slaa na kuongeza:

“Maswali haya kuanzia leo iwe mwisho kuniuliza, sisi hatuwezi kukaa na kujadili upuuzi wa Kafulila na Juju, tena andika mwandishi wala usiogope; nasema ni upuuzi”

Dk Slaa alisema kuwa ndani ya Chadema mtu yeyote akifanya mambo kinyume na utaratibu lazima achukuliwe hatua kali za kinidhamu kwa kufuata katiba ya chama hicho.

Alisisitiza kwamba, mambo yote yanayozungumzwa kuhusu chama hicho hayana msingi na yanatolewa na watu wasioipenda Chadema na wanaotaka kukiona chama hicho kikipoteza dira.

Tags:

0 comments

Post a Comment