DPP asema ni pamoja na Karamagi na Msabaha Ramadhan Semtawa IKIWA sasa ni mwaka mmoja tangu kuibuka kwa sakata la mkataba wa kifisadi wa Kampuni ya Richmond Development (LLC), uchunguzi wa kijinai kuhusu mawaziri wawili wa awamu ya nne Nazir Karamagi na Dk Ibrahim Msabaha, sasa umejikita zaidi nchini Marekani ambako ni chimbuko la kampuni hiyo inayodaiwa kuwa ya kitapeli. Wiki iliyopita Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Edward Hoseah, aliirushia kombora ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DDP) akisema imekalia majalada 60 ya kesi za rushwa, pasipo kufafanua kama miongoni mwa majalada hayo lipo la Richmond linalomhusu Dk Ibrahim Msabaha na Karamagi. Lakini, vyanzo vya habari vilisema, jalada hilo la Richmond kuhusu Dk Msabaha na Karamagi, bado halijarudi kwa DPP na uchunguzi wake unafanywa na makachero wa Tanzania nchini Marekani. DPP Eliazer Feleshi, alipoulizwa kuhusu jalada hilo, alithibitisha kwamba, hadi sasa anachofahamu ni uchunguzi wa tuhuma hizo unaendelea Marekani na haujakwisha. Marekani ndiko chimbuko la taarifa za kampuni hiyo hewa, kitapeli na kifisadi ambayo imekuwa ikitikisa nchi na kuibua hali tete nchini baada ya kuwagusa vigogo mbalimbali, akiwemo Edward Lowassa, ambaye alijiuzulu Uwaziri Mkuu Februari mwaka jana pamoja na mawaziri, Karamagi na Msabaha. Lakini akijibu kuhusu hatma ya mashitaka ya vigogo hao wawili na uvumi wa yeye kukwamisha kesi zao, DPP Feleshi alisema:, "Watu waache uzushi, mbona hawasemi kama uchunguzi unaendelea Marekani, wamewahi kusema hili? Ninavyojua uchunguzi unaendelea." Kwa mujibu wa DPP Feleshi, "watu wanapaswa kufanya uchunguzi na kubaini ukweli kuliko kukalia na kusikiliza taarifa hizo za kizushi na zisizo na ukweli wowote," alifafanua. Mkuu huyo wa mashitaka alipoulizwa kwamba, amekuwa akitumia kigezo cha kutokamilika uchunguzi kukwamisha kesi za vigogo hao, na kwamba zipo taarifa zinazoonyesha kuwepo jinai, alijibu: " kama unazo zihusishe na kesi ya mahakamani na kuongeza:, "Kama unazo unashindwaje kuzihusisha na zile taarifa zilizotolewa mahakamani na bungeni za Naeem Gire wenzake?" alihoji. Hata hivyo, Gire na wenzake kwa sasa tayari wana kesi mahakamani na utaratibu ni makosa kuingilia mwenendo wa mashitaka uliopo mahakamani hasa kwa kutumia vyombo vya habari. Lakini, Bunge lilipitisha maazimio 23 ambayo miongoni mwao ni lile lililomtaka Dk Msabaha na Karamagi ambao walikuwa mawaziri wa Nishati na Madini kwa muda tofauti, wajiuzulu nyadhifa zao. Karamagi ndiye aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini wakati mkataba ukisainiwa Juni 23, 2006 na Msabaha alikuwepo katika hatua za awali na hadi anajiuzulu alikuwa Waziri wa Uhusiano wa Afrika Mashariki. DPP Feleshi alipoulizwa zaidi kama tayari alipitia taarifa ya Timu ya majadiliano ya mikataba Serikalini (GNT), hakutaka kuingia kwa undani kulitolea ufafanuzi. Hata hivyo, awali Feleshi, aliwahi kuweka bayana kwamba miongoni mwa mambo muhimu ambayo ofisi yake ilikuwa ikiangalia ni kupitia taarifa hiyo ya GNT ambayo hata bunge liliazimia kwamba mamlaka zake zichukue hatua kwa wajumbe wote. Wajumbe wa GNT wanaotajwa kuingiza serikali mkenge katika Richmond ni kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu (AG), Benki Kuu Tanzania (BoT) na Shirika la Tanesco ambalo ni madau mkuu katika mradi huo. Lakini, katika siku za karibuni kumekuwa na taarifa za ofisi ya DPP kukwamisha jadala hilo la akina Karamagi na Msabaha kwasababu ambazo hazikuweza kufahamika mara moja. |
You Are Here: Home - - Uchunguzi wa Richmond wahamia Marekani
IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
0 comments