Mataifa Masikini Duniani yautaja mkataba ulioandaliwa na Denmark na Kuungwa Mkono na Marekani kuwa
ni Janga la kimataifa kwa Nchi masikini Duniani
Mwenyekiti wa G-77 aukataa mkataba wa Copenhagen
COPENHAGEN
Mwenyekiti wa kundi la mataifa 77 yanayoendelea, Lumumba Stanislas Di-Aping ameukataa mkataba wa mabadiliko ya hali ya hewa uliopendekezwa na Marekani na mataifa makubwa yanayoendelea, hivyo kutishia upinzani ndani ya mazungumzo ya Umoja wa Mataifa ya hali ya hewa huko Copenhagen. Amesema mkataba huo unakiuka tamaduni ya Umoja wa Mataifa na kwamba hauwezi ukaidhinishwa. Ameonya kuwa mkataba huo utaziweka nchi masikini katika hali mbaya zaidi na kuongeza kuwa nchi nyingine masikini huenda zikaukataa pia.
Bwana Lumumba kutoka Sudan alikuwa akizungumza saa chache baada ya Rais Barack Obama wa Marekani kusema kuwa ameafikiana kuhusu mkataba wa mabadiliko ya hali ya hewa pamoja na nchi za China, India na Afrika Kusini. Bwana Lumumba, ameishutumu Marekani na nchi mwenyeji, Denmark kwa kukandamiza haki za mataifa masikini na kuuita mkataba huo mbaya zaidi katika historia. Chini ya mkataba huo mataifa tajiri yatatoa fedha kwa mataifa masikini ili kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa, lakini nchi hizo tajiri hazijajitoa zaidi katika kupunguza matumizi ya gesi zinazoharibu mazingira.
0 comments