Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Ni Sophia Simba tena leo katika vichwa vya habari..

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
Sophia Simba amkataa mteule wa Rais Jakaya Kikwete
Mwenyekiti wa UWT-CCM Sophia Simba ambaye pia ni Waziri wa Utawala Bora katika Ofisi ya Rais Kikwete.

SASA ni dhahiri kuwa hali ya kisiasa ndani ya Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT), si shwari kutokana na nguvu na ushawishi wa Mwenyekiti Sophia Simba kuweka rehani ajira ya katibu mkuu wa jumuiya hiyo, Husna Mwilima.

Simba, ambaye amekuwa akitikisa anga za kisiasa katika siku za karibuni baada ya kurushia watu tuhuma mbalimbali kwenye mkutano wa Kamati ya Mzee Mwinyi na Wabunge, anadaiwa amefanikiwa kulishawishi Baraza Kuu la UWT kuazimia kwa kauli moja kutoridhia utendaji wa Mwilima na kumtaka mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete ampangie kazi nyingine.

Kikwete alimtangaza Mwilima kuwa ameteuliwa kushika nafasi hiyo ya utendaji kwenye jumuiya hiyo mwezi Aprili, akiwa amemuondoa kwenye wadhifa wake wa ukuu wa wilaya, ikiwa ni utaratibu mpya wa uteuzi wa watendaji wa jumuiya za CCM.

Lakini sasa mwenyekiti huyo wa CCM atalazimika kuangalia upya utaratibu huo baada ya habari hizo za kutaka mtendaji huyo aondolewe kwenye jumuiya hiyo ambayo ni moja ya nguzo muhimu za chama hicho tawala.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari vya kuaminika kutoka ndani na nje ya UWT, kikao hicho cha Baraza Kuu kilichofanyika Dodoma kuanzia Novemba 17 hadi 20, kilipitia utendaji wa Mwilima na kuweka bayana kuwa hakimtaki aendelee na kazi kutokana na sababu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kile kinachodaiwa kutomheshimu mwenyekiti wake Simba.

Sophia Simba anadaiwa kuwa alisoma tuhuma dhidi ya katibu wake mbele ya wajumbe wa Baraza Kuu.

Lakini, taarifa rasmi ya UWT iliyotolewa jijini Dar es Salaam jana, haikueleza azimio hilo la kutaka Mwilima aondolewe, lakini liliweka bayana kwamba katika kikao hicho liliazimia kutoridhishwa na utendaji wa katibu huyo katika kutekeleza maagizo ya vikao vilivyopita.

UWT haina mamlaka ya kumfukuza kazi katibu mkuu kwa kuwa huteuliwa na mwenyekiti wa CCM, lakini baraza kuu la jumuiya hiyo ndilo linalomuidhinisha baada ya kuteuliwa.

Baraza pia lina uwezo wa kumshauri mwenyekiti wa CCM kumwondoa mtendaji wake mkuu kama hatekelezi vema majukumu ya umoja.

Kikatiba, majina ya makatibu wakuu wa jumuiya za CCM hupendekezwa na mwenyekiti wa chama ambaye pia ni Rais na baadaye humpatia katibu mkuu wa chama ambaye hupeleka jina hilo kwa mwenyekiti wa jumuiya husika ambaye naye hupeleka Baraza Kuu kwa ajili ya kuidhinishwa.

Hata hivyo, taarifa hiyo ya UWT ilifafanua kwamba katiba ya umoja huo inamtaja katibu mkuu kuwa ndiye mtendaji mkuu wa jumuiya, hivyo Baraza lilimtaka Mwilima atoe ufafanuzi wa baadhi ya maagizo ya vikao ambayo hayakutekelezwa.

"Ukweli ni kwamba, katika kikao hicho Baraza Kuu la UWT halikuridhishwa na utekelezaji wa baadhi ya maagizo ya vikao vilivyopita. Hivyo Baraza Kuu lilimtaka kutoa ufafanuzi kwa baadhi ya maagizo ya vikao ambayo hayakutekelezwa," ilifafanua UWT katika taarifa hiyo iliyosainiwa na Sarah Msafiri Ally ambaye ni mkuu wa idara ya oganaizesheni, siasa na mahusiano ya kimataifa.

Katika taarifa hiyo, UWT imetaja maazimio mbalimbali yaliyofikiwa, ikiwa ni pamoja na kutoridhishwa na malumbano baina ya baadhi ya wabunge wa CCM.

"Baraza Kuu linaipongeza NEC kwa kuteua kamati maalumu ya kuchunguza chanzo cha tatizo kwa dhamira ya kutafuta ufumbuzi wa kudumu... Baraza Kuu linashauri malumbano hayo yamalizwe kwani hayana maslahi kwa CCM na taifa kwa ujumla," inafafanua.

Habari zaidi kutoka kwa baadhi ya wajumbe wa baraza kuu zilithibitisha kwamba ajira ya Mwilima iko hatarini huku sababu moja kuu ikiwa ni kile wanachodai ni kutomheshimu Simba.

Mmoja wajumbe kutoka moja ya mikoa ya kaskazini aliliambia gazeti hili kwamba Mwilima ameonyesha uwezo mdogo kiutendaji ndiyo maana licha ya kupewa onyo na kamati ya utekelezaji, bado alishindwa kujisahihisha.

Mjumbe huyo, ambaye aliomba kuhifadhiwa jina lake, alifafanua kuwa baada ya kupata taarifa hizo za utendaji wa katibu kutoridhisha, liliazimia aelezwe bayana mapungufu hayo bila kumficha.

"Kitu hicho kilifanyika na yeye mwenyewe kuomba radhi," alisema mjumbe huyo.

"Tumeona ni vema aelezwe ajue mapungufu yake, kwani kama akiachwa bila kuelezwa ni tatizo; ameshindwa kusimamia utekelezaji wa kazi za kila siku za kiutendaji kwa sababu ya uwezo mdogo.

"Alishapewa onyo la kwanza na kamati ya utekelezaji, lakini alishindwa kujirekebisha ndipo baraza likamweleza bayana kutoridhishwa na utendaji wake."

Mjumbe huyo ambaye ni mwenyekiti wa mkoa alisema sababu nyingine ni katibu huyo kuelezwa kutomheshimu mwenyekiti wake Simba, hali ambayo ilichukiza wajumbe.

Mjumbe mwingine kutoka mkoa wa Kanda ya Ziwa, aliliambia gazeti hili kwamba kilichokuwa kikijadiliwa na kuazimiwa ni utendaji usioridhisha wa katibu huyo.

Akizungumza kwa shariti la kutotajwa jina lake, mjumbe huyo alifafanua uamuzi huo ni utaratibu wa kawaida tu ndani ya vikao halali vya jumuiya hiyo ya chama.

Mjumbe huyo alisema hakuna mpasuko ndani ya uongozi wa UWT, lakini akasisitiza kwamba makundi yapo kwa wapambe.

Vyanzo vya habari vinadai kwamba tayari Baraza Kuu la UWT, limemwagiza Sophia Simba kumueleza Kikwete amtafutie ajira nyingine.

Inadaiwa kwamba wakati wa kutoa msaada wa UWT kwa waathirika wa milipuko ya mabomu Mbagala, Simba alimtaka Mwilima kumkabidhi vifaa hivyo akavitoe yeye, lakini katibu huyo aligoma na kuwatuma watendaji wa chini.

Mwilima pia anadaiwa kuandaa orodha ya makatibu wa mikoa na wilaya wa UWT bila ya kushauriana na mwenyekiti wake, ambaye inadaiwa pia alikuwa na orodha yake, ikiwa ni jitihada za kujijenga ndani ya jumuiya hiyo baada ya kupata ushindi mdogo.

Habari zinaeleza kwamba viongozi hao wa UWT wamefikia hatua ya kukatiana simu.

“Katika siku za hivi karibuni, katibu hataki kabisa kupokea simu ya Sophia Simba. Amemwambia wazi kama ana agizo aandike barua,” alisema.

Simba na Mwilima hawakuweza kupatikana jana kuzungumzia suala hilo.

Tags:

0 comments

Post a Comment