Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Obama ateua balozi mpya tanzania

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter RAIS Barack Obama wa Marekani amemteua Alfonso Lenhardt kuwa balozi wake nchini Tanzania. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam jana, Rais Obama alimteua Alfonso baada ya mashauriano na kupata ridhaa ya Baraza la Seneti kwa mujibu wa Katiba ya nchi hiyo. Akizungumza wakati wa kutangaza mabalozi wapya watakaoiwakilisha Marekani kwenye nchi mbalimbali, Obama alisema Wamarekani watafaidika na wawakilishi hao katika nchi za nje kutokana na vipaji, uzoefu na kujitoa kwao. Aliongeza kuwa ni imani yake watatoa mchango mkubwa hasa katika kipindi hiki muhimu cha kuimarisha ubia kati ya Marekani na mataifa mbalimbali duniani kote. "Wamarekani watafaidika sana kwa kuwa na watumishi wao hawa waliotukuka na ambao ni wawakilishi wao kwa kutumia vipaji, uzoefu na kujitoa kwao kikamilifu, watatoa mchango mkubwa sana tunapoendelea kuimarisha ubia kati ya Marekani na Mataifa mbalimbali duniani kote na kukabiliana na changamoto kubwa za karne ya 21. Ninashukuru kwa utumishi wao, nina shauku kubwa ya kufanya kazi na kila mmoja wao,"alisema Obama. Mei 2004, Lenhardt aliwahi kuwa Rais na Afisa Mtendaji Mkuu wa Baraza la Kitaifa la Kuzuia Uhalifu (National Crime Prevention Council - NCPC)nchini Marekani ambalo ni taasisi isiyo ya Kiserikali na isiyozalisha faida. Aliwahi pia kuwa Makamu wa Rais wa Kundi la Makampuni ya Shaw akishughulikia Uhusiano na Serikali, Septemba 4, mwaka 2001 aliteuliwa kuwa Mpambe wa Bunge (Sergeant-at-Arms), wa 36 wa Bunge la Seneti la Marekani na kuwa Mmarekani wa Kwanza mwenye asili ya Kiafrika kuhudumu katika wadhifa huo ndani ya Bunge la Marekani. Aidha, alihudumu kama Makamu wa Rais na Afisa Mwendeshaji Mkuu wa Baraza linaloshughulikia Wakfu Mbalimbali (Council on Foundations) na Lenhardt alistaafu kutoka katika Jeshi la Marekani August 1997 akiwa na cheo cha Meja Jenerali, baada ya kulitumikia jeshi hilo kwa zaidi ya miaka 30 katika ngazi mbalimbali za uongozi. Wadhifa wake wa mwisho jeshini ulikuwa ni Mkuu wa Kamandi ya Uajiri, yenye makao makuu yake huko,Fort Knox, KY, ambako aliongoza na kusimamia taasisi iliyojumuisha zaidi ya watu 13,000 waliokuwa katika vya kazi 1,800. Aidha, aliwahi kudumu kama Afisa Mwandamizi wa Polisi Jeshi (Senior Military Police Officer) katika oparesheni zote za kipolisi na masuala ya usalama katika Jeshi la Marekani sehemu mbalimbali duniani. Lenhardt alizaliwa katika jiji la New York, ana Shahada ya Kwanza ya Sayansi ya Sheria kuhusu Makosa ya Jinai kutoka katika Chuo Kikuu cha Nebraska, Shahada ya Pili ya Sanaa Katika Utawala kutoka katika Chuo Kikuu cha Central Michigan na Shahada ya Pili ya Sayansi ya Utawala katika Sheria kutoka katika Chuo Kikuu cha Serikali cha Wichita. Lenhardt pia ni mhitimu wa awamu ya 94 Katika Chuo cha Kitaifa cha Mafunzo ya Usalama cha FBI, programu ya Viongozi wa Upepelezi wa Makosa ya Jinai ya Jeshi la Marekani na mhitimu wa Chuo cha Kitaifa cha Mafunzo ya Kivita (the National War College) na Chuo Kikuu cha Mambo ya Kijeshi na Usalama (National Defence University).
Tags:

0 comments

Post a Comment