Kikao cha mwaka cha Umoja wa mataifa kinachoendelea mjini New York Marekani, kimeshuhudia kuendelea mvutano juu ya mizozo ya kimataifa hususan kati ya Marekani na Urusi na kuathiri usuluhishi wa mizozo hiyo.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi, Sergei Lavrov, amesema Urusi inazingatia kuwa ushirikiano kati yake na Marekani ni muhimu lakini Urusi lazima iyateteye maslahi yake.
Mzozo wa Georgia uligubika mazungumzo ya hivi karibuni kati yake na mwenzake wa Marekani Condoleeza Rice lakini bado mvutano unaendelea huku Urusi ikisema haielewi kwanini nchi za magharibi na hususan Marekani zilipanda juu kuilaani kuhusu mzozo wa Georgia badala ya kulizingatia suala hilo kwa jumla. Na mvutano huo unapelekea kuwa vigumu kuyasuluhisha masuala ya kimataifa ya wakati huu, sio tu mzozo huo wa Georgia na eneo la Caucacus kwa jumla bali pia mizozo mingine kama mzozo juu ya mpango wa kinyuklia wa Iran na Korea ya kaskazini.
Mvutano huo kati ya Marekani na Urusi ulijitokeza pia huko New York Marekani ambako kando na kikao hicho cha mwaka cha Umoja wa mataifa kinachoendelea kumekuwa kukifanyika mikutano mbali mbali kati ya wataalamu au wanadiplomasia au hata kati ya marais kuyajadili masuala kem kem.
Urusi imepinga kushiriki katika mkutano wa mawaziri wa mambo ya kigeni wa nchi 6 ambazo zinahusika na mazungumzo juu ya suala la kinyuklia la Iran, ikiwa ni pamoja na Marekani, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, China na Urusi. Mkutano huo ulikuwa umepangwa kufanyika kesho mjini New York Marekani kando na mkutano huo wa mwaka wa Umoja wa mataifa. Urusi imelipiza kisase dhidi ya kuahirishwa mkutano wa nchi 8 tajiri zaidi kiviwanda ama G8 vile vile kando na kikao hicho cha Umoja wa mataifa, kutokana na ombi la Marekani kukiwa na utata juu ya suala la kuialika Urusi ambayo inashutumiwa na nchi nyingi za kundi hilo la G8 na hususan Marekani kwamba haijayaondoa majeshi yake kutoka Georgia.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier, anasema mvutano huo unatia wasi wasi na huo sio mkondo unaotakiwa na ule unaotakiwa ni kurejea kwenye meza ya mazungumzo.
Maafisa wa Marekani walitishia kuiondoa Urusi kutoka kundi la nchi 8 tajiri zaidi duniani ama G8 lakini hakuna hatua rasmi imekwishachukuliwa juu ya hilo.
Inahofiwa kundi hilo la G8 likageuka mhanga wa mvutano huo kati ya Marekani na Urusi. Mkutano wa kilele wa viongozi wa nch wa kundi hilo umepangwa kufanyika ifikapo mwezi Mei mwakani katika kisiwa cha Maddalena nchini Italy. Waziri mkuu wa Italy, Silvio Berlusconi, alitangaza hivi karibuni mjini London Uingereza kwamba hana shakashaka yoyote Urusi itaalikwa wakati kuna baadhi ya nchi ambazo zingependelea Urusi ichukuliwe hatua za kuitenga.
0 comments