Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - MTIKILA APEWA KICHAPO......

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter

MWENYEKITI wa Chama cha Democratic (DP), Mchungaji Christopher Mtikila, amejeruhiwa kwa kupigwa na wananchi wanaodaiwa kukerwa na hatua yake ya kuzidi kuchambua kifo cha aliyekuwa mbunge wa Tarime, Chacha Wangwe.

Mtikila ambaye alikimbizwa katika Hospitali ya Wilaya ya Tarime, alipata kipigo hicho jana wakati akiwa jukwaani, akimnadi mgombea wake wa udiwani, Johanes Sandu, katika viwanja vya Sabasaba, mjini Tarime.

Kabla ya kuanza kupata kipigo hicho, Mchungaji Mtikila alianza kwa kunadi sera za chama chake cha DP, huku akiwashawishi wananchi wa Tarime kuwa chama hicho ndicho mbadala wa maendeleo yao.

Huku akisikilizwa, Mtikila alisema jimbo hilo litapata maendeleo ya haraka iwapo wananchi wataamua kuwachagua wagombea wa ubunge na udiwani kutoka chama chake.

Hata hivyo Mtikila alianza kuibua miguno ya hapa na pale alipoanza kuzungumzia kifo cha Wangwe, aliyefariki dunia kwa ajali ya gari mkoani Dodoma, mwishoni mwa Julai mwaka huu, akihusisha tukio hilo na njama zilizopangwa na viongozi wa CHADEMA.

Habari kutoka Tarime zinaeleza kuwa, wakati akiendelea kueleza kuhusu hilo, wananchi walianza kupiga kelele za kumtahadharisha aache kuzungumzia suala hilo, jambo ambalo alilikataa na badala yake akawa akisisitiza kuwa angeendelea kueleza kile anachokiamini na kukifahamu.

‘Siwezi kuacha kusema kwa sababu ya watu wachache waliokubali kudanganywa kuwa, Wangwe aliuawa kwa ajali ya gari. Nina ushahidi kwamba alipigwa risasi na kuwekwa kwenye gari na kisha likapinduliwa, halafu tukaambiwa amekufa kwa ajali,” alinukuliwa akisema Mtikila.

Mchungaji huyo alipomaliza kutoa kauli hiyo, ghafla mawe yalianza kuvurumishwa katika jukwaa alilokuwapo na moja ya mawe hayo likampata kisogoni na kumjeruhi.

Tukio hilo lilisababisha polisi waingilie kati kumnusuru mwanasiasa huyo, hatua ambayo ilihitimisha shamrashamra za kampeni katika eneo hilo la Tarime Mjini na watu kutawanyika katika maeneo tofauti baada ya vurugu za mawe kurushwa kuendelea.

Huku akivuja damu, Mtikila aliingizwa katika gari moja lililokuwapo eneo la mkutano na akakimbizwa katika Hospitali ya Wilaya ya Tarime ambako alihudumiwa kabla ya kwenda kituo cha polisi kuandikisha maelezo yake kuhusu kile kilichotokea.

Ofisa mmoja wa juu wa polisi aliyezungumza na Tanzania Daima kwa sharti la kutotajwa jina gazetini kwa kuwa yeye si msemaji rasmi wa jeshi hilo, alithibitisha kuhusu kujeruhiwa kwa Mtikila wakati akihutubia mkutano huo na kwamba tayari baadhi ya watuhumiwa walikuwa wakihojiwa na polisi.

‘‘Nadhani unajua utaratibu na miiko ya kazi yetu, mimi si msemaji wa Jeshi la Polisi. Hata hivyo ninachoweza kukuthibitishia pasipo kuwapo kwa ulazima wa kuandika jina langu ni kwamba, ni kweli Mtikila amejeruhiwa na watu wanaotuhumiwa kumjeruhi wanahojiwa,” alisema ofisa huyo aliyeko Tarime.

Akizungumzia tukio hilo, Msimamizi wa Uchaguzi Mdogo wa Ubunge katika jimbo hilo, Titus Kangezi, alikiri kupata taarifa kuhusu kujeruhiwa kwa Mtikila wakati akihutubia na akasema hata yeye alikuwa akijaribu kupata taarifa kamili kuhusu kile kilichotokea.

‘‘Hata mimi ndiyo kwanza nimezipata taarifa hizi za Mtikila kupigwa na kujeruhiwa. Hapa nilipo nafuatilia ili kupata taarifa kamili ya kile kilichotokea,” alisema Kangezi.

Akizungumza kwa simu kutoka Tarime, Mtikila mwenyewe alikiri kujeruhiwa na kuvuja damu nyingi baada ya kupigwa jiwe wakati akihutubiwa mkutano huo wa hadhara.

“Ni kweli nimepigwa, kuna mtu mmoja amenirushia jiwe akanijeruhi kisogoni. Nimevuja damu nyingi sana na hivi sasa nipo hapa katika kituo cha polisi naandikisha maelezo, baadaye nitawapa taarifa kamili,” alisema Mchungaji Mtikila akizungumza kwa unyonge.

Tukio la Mtikila kupigwa linakuja siku chache tu baada ya matukio ya vurugu katika kampeni hizo kutokea katika mikutano ya kampeni ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kabla ya hapo katika kampeni za NCCR-Mageuzi ambazo zilimhusisha mwanasheria maarufu wa chama hicho, Dk. Sengondo Mvungi.

Utete wa hali ya kisiasa Tarime, eneo ambalo limekuwa likikabiliwa na mapigano ya koo, yamesababisha kupelekwa kwa wingi kwa askari wa kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), lengo likiwa ni kudhibiti hali ya amani na utulivu wakati wa kampeni hizo ambazo zitahitimishwa siku moja kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mdogo Oktoba 12 mwaka huu.

Tags:

0 comments

Post a Comment