Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - CAG kukabidhi ripoti ya UDA

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
RIPOTI ya uuzaji Shirika la Usafiri Dar es Salaam (Uda), inatarajiwa kukabidhiwa Machi 20, mwaka huu kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, baada ya uchunguzi kukamilika.Hatua hiyo inakuja baada ya Pinda kuunda tume ya kuchunguza sakata la uuzaji wa shirika hilo, baada ya wabunge wa Dar es Salaam kulalamikia taratibu zilizofuatwa.


Pinda aliagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), kuchunguza mchakato mzima wa uuzaji hisa za shirika hilo kwa Kampuni ya Simon Group Ltd.


Akizungumza kwenye mahojiano maalumu na Mwananchi jana, Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh, alisema tayari ripoti hiyo imekamilika na kwamba, kuanzia Machi 14 hadi 20 watarajia kumkadhibi Pinda.
Utouh alisema kukamilika kwa zoezi hilo kunatokana na ofisi yake kushirikiana na Kampuni ya KPMG kuhakiki mchakato mzima wa uuzaji shirika hilo na kuwahoji watu waliotajwa kuhusika.


“Tumekamilisha zoezi la uchunguzi wa mchakato mzima wa uuzaji Shirika la Uda, tunatarajia kumkabidhi Waziri Mkuu ripoti hiyo wakati wowote kuanzia Machi 14 ili aweze kuipitia kama ataona kuna hatua zingine za kuchukua huo utakuwa uamuzi wake,”alisema Utouh.


Aliongeza kuwa hadi sasa hakuna upungufu uliojitokeza dhidi ya ripoti hiyo na kwamba, uamuzi utakaofanywa na Serikali utakuwa sahihi kulingana na zoezi lenyewe lilivyofanyika.
Utouh alisema walitakiwa kuwasilisha ripoti hiyo mapema Februari, lakini walishindwa kufanya hivyo kutokana na kutaka kujiridhisha kwa undani zaidi.


Alisema kutokana na hali hiyo, anaamini ripoti haijamuonea mtu yeyote hata kama kuna baadhi ya watu wanadaiwa kuhusika kwenye zoezi hilo, wametekeleza kulingana na hadidu rejea walizokabidhiwa na Pinda.


Hatua hiyo inafuatia kuibuliwa kwa kashfa ya uuzaji Uda na wabunge wa Dar es Salaam Agosti mwaka jana kwamba, taratibu zilikiukwa wakati wa uuzaji dhidi ya Kampuni ya Simon Group, inayomilikiwa na Robert Kisena.


Baadhi ya vigogo wanaodaiwa kuhusika na kashfa hiyo, ni Meya wa Dar es Salaam, Dk Didas Masaburi, aliyekuwa Mwenyekiti wa bodi, Idd Simba, na Meneja Mkuu wa Uda, Victor Milanzi. Wote wamehojiwa na tume.


UDA ilikuwa inamilikiwa kwa pamoja kati ya Halmashauri ya Dar es Salaam na Serikali Kuu kupitia Hazina, wakiwa na jumla ya hisa milioni 15, kila hisa moja ikiwa na thamani ya Sh100. Kutokana na mchanganuo huo, Halmashauri ya Dar es Salaam ilikuwa inamiliki asilimia 51 ya hisa hizo, huku Hazina ikimiliki asilimia 49.


Februari 11, mwaka jana, Bodi ya Wakurugenzi ya Uda, chini ya Idd Simba, ilikutana na uongozi wa Simon Group ikiongozwa na Kisena na kusaini mkataba, ambao ulithibitisha kwamba Uda ilikuwa imeiuzia Simon hisa milioni 7.8 sawa na asilimia 52.535 ya hisa zote kwa thamani ya Sh1.142 bilioni.

0 comments

Post a Comment