Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Makinda: Posho za vikao bungeni Sh. 200,000/-

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
SAKATA la posho za wabunge limechukua sura mpya baada ya Spika wa Bunge Anne Makinda, kupingana na Katibu wake, Dk Thomas Kashililah, kuhusu wabunge kuongezewa posho za vikao kutoka Sh70,000 hadi Sh200,000.


Mwishoni mwa wiki iliyopita Dk Kashililah alitoa taarifa kwa vyombo vya habari kukanusha taarifa ya wabunge kuongezewa posho hizo, lakini jana Spika Makinda alisema posho hizo zimeongezwa na tayari zimeanza kulipwa.


Spika Makinda alikiri nyongeza ya posho hiyo jijini Dar es Salaam katika mahojiano na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kuzindua wa Ripoti ya Dunia ya Umoja wa Mataifa kuhusu Haki, idadi ya watu na vijana


"Mbunge huyu alikuwa anapata Sh70,000 kwa hiyo tumemwongezea 130,000 na hupati (hapati)'unless' (isipokuwa) umefanya kazi ya Bunge na amesaini asubuhi na jioni. Kama hujafanya hivyo hupati hizo fedha,"alisema Makinda.


Juma lililopita gazeti hili liliripoti taarifa za ndani kwamba posho za wabunge zimepanda kutoka Sh70,000 hadi 200,000 hivyo kufanya bajeti ya posho hizo kwa mwaka kufikia Sh28 bilioni.


Kutokana na ongezeko hilo, taarifa hizo zilisema kila mbunge atakuwa akilipwa Sh80,000 kama posho ya kujikimu (perdiem) anapokuwa nje ya jimbo lake, posho ya vikao (sitting allowance) Sh200,000 na mafuta ya gari Sh50,000 kila siku, sawa na Sh330,000 kwa siku.


Wakati taarifa hiyo inaripotiwa Dk. Thomas Kashililah alisema hawezi kuzungumzia jambo hilo kwa sababu yeye si msemaji wa Bunge na akashauri atafutwe Spika.


Hata hivyo, baada ya mjadala wa takribani wiki moja wa wanaharakati, wabunge na wasomi kupinga nyongeza hiyo ya posho, Jumapili Iliyopita Dk Kashililah aliibuka na kukiri kuwa wabunge wanataka waongezewe posho za vikao, lakini mapendekezo hayo hayajaanza kutekelezwa.


Dk Kashililah alitoa kauli hiyo katika taarifa yake aliyoisambaza kwa vyombo vya habari jana. Kwa mujibu wa Katibu huyo Bunge, mapendekezo ya kutaka posho za wabunge zipande, yaliibuka katika mkutano wa wabunge mjini Dodoma Novemba 8, mwaka huu, lakini hadi sasa hayajaanza kutekelezwa.


"Suala la mabadiliko ya posho za vikao vya Bunge lilijitokeza katika Mkutano wa Wabunge, tarehe 8 Novemba, 2011 walipoiomba Serikali iangalie upya suala hilo kwa lengo la kuboresha,” alisema Dk Kashililah katika taarifa hiyo na kuongeza:


”Hadi tunapotoa tangazo hili, Serikali haijatoa taarifa iwapo posho hiyo imeongezeka kutoka Sh70,000 hadi Sh200,000."

Dk Kashililah aliendelea kueleza "Kwa mujibu wa Waraka wa Rais kuhusu Masharti ya Mbunge uliotolewa tarehe 25 Oktoba,2010, wenye Kumbukumbu namba CAB111/338/01/83 na kusainiwa na Katibu Mkuu Kiongozi, pamoja na stahili zingine, mbunge anastahili kulipwa posho ya kikao ambayo ni sawa na Sh70,000 kwa kila kikao na masharti hayo hayajafanyiwa marekebisho wala kufutwa.


"Kwa hiyo, taarifa hiyo iliyotolewa siyo sahihi, lakini endapo itatokea, mwenye mamlaka ya kupitisha kiwango kipya cha posho za vikao vya Bunge, itakuwa ni uamuzi kama uamuzi mwingine anaoutoa wa kuwaongezea watumishi wa umma mishahara, posho, marupurupu na mafao mengine." 


0 comments

Post a Comment