Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA LEO - Osama bin Laden aiponza Pakistani

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
RAIS wa Marekani, Barack Obama ameitaka Pakistani kufanya uchunguzi wa kina wa namna Kiongozi wa kundi la kigaidi la Al-Qaeda, Osama bin Laden alivyoweza kuishi nchini humo, tena karibu kabisa na kituo cha kijeshi kama Serikali haihusiki, huku akisema haiwezekani aishi nchini humo kwa miaka sita bila Serikali kujua.

Obama alisema kuna shaka kwamba kiongozi huyo wa kundi la kigaidi aliishi Pakistani kwa ufadhili ama Serikali au kundi fulani la watu linaloshabikia vitendo vyake.

"Ni lazima Pakistani ifanye uchunguzi wa namna Osama alivyoishi nchini humo kwa miaka yote hiyo bila Serikali kujua. Hii inaonyesha kuwa kama siyo Serikali yenyewe iliyomfadhili, basi kuna watu wanaomsaidia," alisema Obama katika mahojiano na Shirika la Habari la CBS.

Obama alisema ingawa hana ushahidi wa moja kwa moja unaoonyesha kuwa kuna watu ndani ya Serikali ya Pakistani waliomsaidia bin Laden, ni jambo linalofaa kuchunguzwa kwa makini.

Lakini alisema kutokana na mazingira aliyokuwa anaishi kiongozi huyo wa Al Qaeda, ni dhahiri kwamba kuna mtandao unaofahamika na inawezekana kabisa mtandao huo una watu kutoka Serikaliya Pakistani.

"Hatujui kama kuna baadhi ya kundi la watu kutoka Serikali ya Pakistani au la, au nje ya Serikali, lakini kinachotakiwa ni kufanyika kwa uchunguzi wa kina. Muhimu zaidi ni Serikali ya Pakistani kujichunguza yenyewe," alisema Obama na kuongeza:
"Ni vigumu kuelewa namna kiongozi huyo alivyoweza kuishi karibu na jeshi tena kwa miaka mingi hivyo bila hata kukamatwa na Serikali au jeshi la nchi hiyo, mpaka Marekani ikamkamate." Obama alisema kwamba pamoja na hayo, mauaji ya Osama yamemfanya sasa apate usingizi ambao viongozi kadhaa wa Serikali ya Marekani waliomtangulia waliukosa.

"Kutokana na mauaji ya Osama mimi siwezi kupoteza hata chembe ya usingizi wangu. Sasa nitalala usingizi mnono," alisema.Obama alisema kitendo cha nchi yake kumuua Osama si kosa kwani tayari ilitoa matangazo duniani kote kumtafuta na hakutokea. Alisema: "Kilichofanyika kwa Osama si kosa kwani tulikuwa tunamtafuta kwa muda mrefu sana. Watu wanaolalamikia tukio hilo hawana nia njema na Marekani.

 Lakini nasisitiza kwamba Marekani imetenda haki na watu wanapaswa kupima tukio hilo na yale aliyokuwa akiyafanya kiongozi huyo wa ugaidi duniani."

Pakistani imekuwa ikikanusha kumhifadhi kiongozi huyo wa Al-Qaeda. Rais wa nchi hiyo, Asif Zardari alikaririwa na vyombo vya habari juma lililopita akisema: "Serikali haihusiki kumhifadhi Osama, isitoshe imekuwa mstari wa mbele katika vita dhidi ya ugaidi." Kauli hiyo inaweza kuwa na mantiki kutokana ukweli kwamba nchi hiyo ndiyo iliyomkamata raia wa Tanzania aliyetuhumiwa kwa ugaidi, Mohammed Ghailan.

Pia imekanusha vikali tuhuma kuwa ilimpa hifadhi kiongozi huyo wa al Qaeda na imetoa amri ufanyike uchunguzi wa kwa nini idara yake ya ujasusi ilishindwa kumpata. Jana jioni, Waziri Mkuu wa Pakistani, Yousuf Raza Gilani alisema Serikali itaunda timu ya wataalamu wa jeshi kuchunguza suala la Osama kuwapo nchini humo bila taarifa.
 Alisema hayo alipolihutubia Bunge la nchi hiyo lililokutana kwa dharura kujadili suala hilo na kusisitiza: "Mauaji ya Osama bin Laden ni haki sahihi kwake."

Waziri huyo alipuuza madai kwamba mamlaka za Pakistani ama hazina uwezo wa kutosha kiintelijensia kujua uwapo wa Osama ama ziliamua kumhifadhi akisema kuwa, hayana ukweli.

Gilani pia aliliambia Bunge kuwa Serikali imepiga marufuku operesheni yoyote inayofanywa na Marekani kutafuta magaidi nchini humo lakini akasisitiza kuwa uhusiano wa nchi hizo mbili bado upo palepale.

0 comments

Post a Comment