Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Mpendazoe awataja mawaziri walioanzisha CCJ

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter

Baada ya kumtaja Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, kuwa mmoja wa waanzilishi wa CCJ, jana aliwataja Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta, na Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrisson Mwakyembe, akisitiza kuwa ndio waliokuwa waasisi wakuu wa CCJ.
Mpendazoe aliwataja mawaziri hao wakati akihutubia maelfu ya wakazi wa mji wa Njombe, waliofurika katika viwanja vya National Housing, katika mfululizo wa maandamano na mikutano ya hadhara ya chama hicho inayoendelea kwenye mikoa ya nyanda za juu kusini.
Mbali na hao, aliwataja makada wengine wa CCM walioshiriki kuanzisha CCJ kuwa ni Victor Mwambalaswa, Daniel Ole Porokwa na Paul Makonda.
Alisema uwepo wa Sitta na Mwakyembe katika baraza la mawaziri unaifanya serikali ya Rais Jakaya Kikwete kuwa ya bandia, kwani viongozi hao wanamdharau na walishawahi kuasi CCM kwa lengo la kujiunga na CCJ.
“Sitta na Mwakyembve ndio waanzilishi wakuu wa CCJ, nilishirikiana nao kuanzisha kile chama, lengo lilikuwa tuungane na CHADEMA ili kuongeza nguvu ya kupambana na ufisadi na uongozi mbovu wa CCM, lakini wenzangu walikuja kunisaliti dakika za mwisho.
“Sitta aliahidiwa kupewa uspika na Mwakyembe uwaziri, lakini baadaye wote wamepewa uwaziri baada ya Sitta kunyimwa uspika waliokuwa wamemuahidi kumpa tena.
Wenzangu hawakuwa na dhamira ya dhati, waliongozwa na uchu wao wa kupenda zaidi madaraka. Wako na Kikwete kwa sababu tu ya vyeo vyao. Wasijifanye kupambana na ufisadi...wala wasidanganye CCM imejivua gamba. Wote ni mafisadi...hakuna wa kuiamini CCM,” alisema Mpendazoe na kushangiliwa.
Alisisitiza kuwa wana-CCM hao wamebaki ndani ya chama hicho na serikali yake si kwa sababu ya utiifu na uzalendo wao kwa chama chao bali wamesukumwa na vyeo vya uwaziri na ukuu wa wilaya walivyopewa na Kikwete mwenyewe bila kujua.
Alisema ameamua kuliambia taifa ukweli wote kuhusu wana CCM hao ili umma wa Watanzania uepuke kudanganywa na propaganda zao za kujifanya wanapambana na ufisadi.
Wakati akimtaja Nape siku mbili zilizopita mbele ya wakazi wa Mbamba Bay mkoani Ruvuma, Mpendazoe alisema kijana huyo alishiriki kuandika katiba ya chama hicho.
Alisema ndiye aliyepewa jukumu la kutafuta nakala za katiba za vyama vingine tawala nchini Afrika, ili kupata katiba nzuri ya kuigwa katika kuandika katiba ya CCJ.
Aliwaambia wakazi hao kuwa Nape alilitekeleza vizuri jukumu hilo kwani alifanikiwa kuipata katiba ya chama cha ANC kinachotawala Afrika Kusini, ambayo alisema ndiyo iliyotumika kwa kiasi kikubwa katika kuandika katiba ya CCJ.
“Huyu Nape anayepiga kelele za kuitetea CCM kujivua gamba ni mnafiki mkubwa pengine kuliko wanafiki wote hivi sasa. Nathibitisha kwa wananchi wa Mbamba Bay na Watanzania wote kwa ujumla kwamba Nape Nnauye alishiriki kuanzisha CCJ, nilikuwa naye, tulikuwa wana CCM sita.
“Nape ni mhaini ndani ya CCM kwa sababu alishakula njama za kutaka kuiangusha, tofauti na Nape, mimi nilijiamini mapema na nilijitoa CCM mapema baada ya kuona hiki chama hakiwafai Watanzania.
“Sasa leo wanajivua gamba halafu Nape wanampa cheo. Niwaulize, hivi kati ya Nape na Lowassa yupi ni mbaya kwa CCM? Ni Nape aliyeona CCM haifai na kushiriki kuanzisha CCJ ili kuiangusha au Lowassa?” alihoji Mpendazoe na umati ukajibu, “Wote hawafai.”
Kisha aliendelea: “Tulifanya naye vikao vyote vya siri hadi tukaanzisha CCJ, leo anaitetea CCM, ni mnafiki mkubwa,” alisema Mpendazoe na kushangiliwa.

Katika hotuba yake hiyo iliyoonekana kuteka hisia za mamia ya wasikilizaji, Mpendazoe alisema CCJ ilianzishwa kwa siri kubwa na Nape alishiriki kikamilifu katika kuhakikisha mawasiliano yao yote yanakuwa ya siri kwani walifungua mtandao maalum wa kuwasiliana kwa internet.
Hata hivyo, alisema baadaye wenzake waliufuta mtandao huo baada ya kubadili mawazo dakika za mwisho hasa baada ya kuahidiwa vyeo na Rais Kikwete.
Alisema hata pale ilipolazimu kukutana, yeye, Nape pamoja na wengine, walikuwa wakipendelea kukutana kwenye vinywaji eneo la Mlimani City jijini Dar es Salaam ili wasitiliwe shaka na maafisa usalama wa taifa aliosema walikuwa wakiwapeleleza wana CCM wote waliohisiwa kula njama za kuanzisha chama kipya.
Mpendazoe aliyewahi kuwa msemaji wa CCJ taifa kabla ya chama hicho kunyimwa usajili wa kudumu, alisema Nape alibadili mawazo ya kujiunga CCJ dakika za mwisho baada ya Rais Jakaya Kikwete kumuahidi na hatimaye kumteua kuwa mkuu wa wilaya ya Masasi.
Alibainisha kuwa kitendo hicho kinaonyesha jinsi kijana huyo asivyo na msimamo na alivyo na uchu wa madaraka.
“Lengo letu la pamoja lilikuwa ni kupinga uongozi mbaya wa CCM na ufisadi tukiwa nje ya CCM maana haiwezekani kupambana na ufisadi ukiwa ndani ya CCM, ukifanya hivyo unakuwa adui. Lakini kumbe mwenzetu ndani ya moyo wake kilichomsukuma kuanzisha CCJ ni kukosa cheo kikubwa ndani ya CCM.
Sasa hilo sikulijua, nililijua baada ya Rais Jakaya Kikwete kumteua kuwa mkuu wa wilaya ya Masasi, hapo alibadili mawazo ya CCJ. Ni kijana msaliti, mnafiki na asiye na msimamo, hafai kuongoza watu, ana uchu wa madaraka …kama si kupewa ukuu wa wilaya Nape asingekuwa CCM leo.
“Alikuwa anatazama tu majaaliwa ya tumbo lake. Huyu naye ni fisadi lakini hajavuliwa gamba, wanafiki watupu,” alisema Mpendazoe na kuamsha shangwe zaidi.
Aidha, alieleza kuwa ili kuwaepuka maofisa usalama wa taifa, wakati mwingine walikuwa wakifanya vikao vyao vya kuanzisha CCJ ndani ya gari pamoja na Nape akiwepo.
Alieleza zaidi kuwa Nape akiwa idara ya mambo ya nje ya CCM katika ofisi ndogo ya chama hicho Lumumba jijini Dar es Salaam, ndiye aliyekuwa akiiba siri za CCM zilizohusu kuwafukuza wote waliohisiwa kuwemo kwenye mpango wa kuanzisha chama kipya cha siasa.
Alieleza kuwa Nape anayemjua yeye ni mtu asiyeukubali uongozi wa Rais Jakaya Kikwete katika chama na serikali kwani katika vikao vyao vya mwanzoni kabisa walivyoazimia kuanzisha CCJ, kijana huyo alikuwa akimkosoa Kikwete na kuelezea udhaifu wake.
“Na ndiye tuliyekuwa tukimtuma kwa wafadhili kupokea fedha za kuanzishia CCJ. Ndiye aliyetafuta pango la ofisi ya CCJ. Kwa kuwa yeye alikuwa kijana zaidi, alifanya mambo mengi ya kufuatilia kwa siri taratibu za uanzishwaji wa chama,” alisema Mpendazoe na kuongeza: “Kikwete anaongoza chama feki, CCM ina watu ambao walishamdharau kama Nape na ambao wanamuona ni kiongozi dhaifu…, lakini kwa sababu mwenyewe aliwapa vyeo bila kuwajua leo wamelazimika kubakia ndani. Mimi siwezi, na ndiyo maana leo niko CHADEMA nikiendeleza dhamira ile ile ya kuwanusuru Watanzania na ufisadi,” alisema na kushangiliwa tena.
Aliwataka wakazi wa Mbamba Bay kutorudi nyuma na kurubuniwa tena na CCM inayosema imejivua gamba, kwani suala limejaa usanii na unafiki mkubwa.
Alisisitiza kuwa kote alikopita na CHADEMA amejiridhisha kuwa chama hicho sasa ndicho kipenzi na tumaini pekee la Watanzania.
“Mimi sitarudi nyuma kama Nape, nitasonga mbele na CHADEMA, tumekwenda kwenye vijiji na miji mingi, CHADEMA ndiyo tumaini pekee la Watanzania….ndugu zangu tusirudi nyuma, huu ndio wakati wa kujikomboa. Kila haki na wakati wake…tusiipoteze fursa hii,” alisema.

0 comments

Post a Comment