Chadema waja juu
Lakini mkutano na waandishi wa habari jana, licha ya kufafanua kuhusu mshahara wa Katibu Mkuu wake, Dk Slaa na ununuzi wa magari, Chadema jana ilimuita Nape kuwa ni 'Vuvuzela' na kwamba hana sifa ya kuinyooshea kidole Chadema.
"Tuna ushahidi wa kutosha kuwa mmoja wa watu walionufaika na fedha za EPA kupitia kwa Jeetu Patel ambaye ameeleza vizuri jambo hili katika maelezo yake mbele ya kamati ya Rais," alisema Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa Chadema, Anthony Komu.
Naye Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Mabere Marando alidai kuwa Nape aliwahi kuomba kugombea ubunge kupitia Chadema baada ya kushindwa kupata nafasi hiyo kupitia CCM, lakini wakamtosa kwa kuwa hakuwa na sifa.
"Nilikuwapo kwenye kikao cha kumjadili Nape, tukaona kuwa hana sifa kumzidi John Mnyika ambaye sasa ni mbunge" alisema Marando. Lakini akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu, Nape aliwataka Chadema kutoa ushahidi unaoonyesha kuwa alihusika na ufisadi wa EPA.
"Atoe ushahidi hadharani, unajua hawa watu ni waongo, hata Watanzania watawashangaa," alisema Nape.
Kuhusu suala la kuhamia katika chama hicho, Nape alisema: "Tena uandike kabisa, mimi ndiyo ninao ushahidi wa wao kunitaka nikagombee kupitia chama chao nikakataa, kwa sababu siwezi kuhamia kwenye chama cha Wachagga, kile ni chama cha ukoo," alisema Nape.
Mishahara ya Makatibu Wakuu
Akifafanua mshahara wa Dk Slaa, Komu alisema kuwa Katibu wake hawajawahi kuomba, kushinikiza wala kuchagiza kulipwa kiasi cha Sh 7.5 milioni kama inavyodaiwa bali analipwa Sh 1,725,000 milioni wakati mbunge analipwa Sh 2,305,000 kabla ya kukatwa kodi.
Alifafanua kuwa Dk Slaa pia hulipwa Sh900,000 za mafuta kwa ajili ya kwenda na kurudi ofisini. Vingine ni malipo ya nyumba, mawasiliano na uwajibikaji na hivyo kuufanya mshahara wake kufikia Sh7,174,000 kwa mwezi.
"Sekretarieti ya Kamati Kuu ilipeleka pendekezo hilo katika vikao vyake vya Kamati Kuu na Baraza Kuu na pendekezo hilo likapitishwa kwa njia ya uwazi na likaingizwa katika mpango kazi wa chama," alisema Komu.
Naye Mabere Marando alikituhumu CCM kuwa kinamlipa Katibu Mkuu wao Sh 11 milioni akisema: "CCM wanapigia kelele mshahara wa Dk Slaa, mbona Mukama (Wilson) analipwa Sh11 milioni?. Mbona Rais Jakaya Kikwete analipwa posho nyingi tu? Ofisi yake iko Dodoma, lakini akienda huko analipwa posho, akirudi Dar es Salaam analipwa," alisema Marando.
Alipoulizwa na Mwananchi kuhusu madai ya Marando, Mukama alikataa kutaja mshahara wake akisema kuwa ni siri yake.
"Mimi leo ndiyo natimiza mwezi mmoja tangu niingine ofisini, hata mshahara wenyewe sijauona. Mshahara ni siri yangu mwenyewe, nimeingia hapa baada ya kustaafu kwa hiyo ndiyo hivyo, naomba msiniingize kwenye hizo 'debate' (malumbano)" alisema Mukama.
Lakini akijibu hoja hiyo, Nape alisema kuwa Mukama analipwa mshahara kulingana na daraja la viongozi na hurekebishwa kama watendaji wengine serikalini.
"Katibu Mkuu wetu analipwa Sh1.5 milioni na hukatwa kodi. Vilevile hulipwa posho isiyokatwa kodi ya Sh300,000. Hayo mengine ya usafiri ni mambo ya kawaida tu. Usafiri anao na hulipiwa umeme wa LUKU na nyumba. Siyo suala la kificho hilo," alisema Nape.
Mafuso ya Chadema
Wakijibu hoja ya Nape kuwa Chadema kimenunua magari chakavu, walikanusha wakisema kuwa magari hayo licha ya kutokuwa chakavu, siyo magari ya kawaida bali ni mitambo maalumu ya uenezi.
"Katika magari hayo kuna vipaza sauti (Public addressing system 3 sets) zenye thamani ya dola za Marekani 148,000 (Sh 222 milioni), jenereta tatu kila moja Sh15.5 milioni sawa na Sh47,000,000," alifafanua Komu.
Naye Marando alisema kuwa chama ndiyo kilimwomba Mwenyekiti Freeman Mbowe awauzie magari hayo ndipo akakubali. "Mimi mwenyewe nilihusika kumwomba Mbowe atupe magari yale, akakubali. Baada ya hapo Kamati Kuu iliunda kamati ya watu wanne chini ya makamu mwenyekiti Zanzibar Mohamed Issa kumwomba mwenyekiti akiachie chama magari hayo.
Naye Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Profesa Abdallah Safari alisema kuwa CCM inatumia ujinga wa Watanzania kama mtaji wake na kuwataka Watanzania kutoyumbishwa na propaganda za CCM.
0 comments