TAMKO lililo tolewa na Chadema kuwa hakiwezi kushiri- kiana na vyama vingine vya upinzani bungeni kwa sababu, vimeungana na CUF ambayo ‘imefunga ndoa’ na CCM na kuunda serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, inaonekana kuvitesa vyama hivyo.
Katibu Mkuu Chadema, Dk Willibrod Slaa, hivi karibuni alikaririwa akisema Kamati Kuu ya Chadema, imeona chama hicho hakiwezi kuwa na ushirikiano wenye tija na vyama hivyo bungeni, na kumwagiza kiongozi wa kambi ya upinzani kuunda baraza kivuli la mawaziri la wabunge wa Chadema pekee.
“Kamati Kuu imeendelea kuzingatia umuhimu wa vyama vya siasa kushirikiana katika kuimarisha nguvu ya upinzani nchini.
Hata hivyo, Kamati Kuu imezingatia kuwa, CUF na CCM wamejiunga kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar na kwa kuwa, sheria inayoruhusu uwepo wa vyama vya siasa inahusu pande zote za Muungano, inaamini CCM na CUF ni wamoja hata Bara,” alisema Dk Slaa.
Jana Mwenyekiti wa Umoja wa vyama hivyo ambavyo vipo nje ya kambi rasmi ya upinzani Bungeni, Hamad Rashid Mohamed na Katibu wake, David Kafulila, walikuwa wazungumzie suala hilo, lakini ilitolea taarifa kuwa mkutano huo uliahirishwa hadi leo.
Pamoja na kutolewa kwa taarifa hiyo, Makamu mwenyekiti wa umoja huo, Khalifa Suleiman Khalifa, alijikuta akitolea ufafanuzi msimamo wao baada ya kubanwa na waandishi wa habari na kusema tamko hilo haliwezi kuwalazimisha Chadema.
Khalifa, ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Gando (CUF), alisema Chadema wana haki ya kuunda kambi yao bila kuvishirikisha vyama vingine.
“Nawashangaa sana Chadema wanaposema kuwa hivi sasa CUF na CCM lao moja, vyama hivi viliamua kuunda serikali ya umoja wa kitaifa ili kumaliza siasa ya mvutano visiwani Zanzibar, hoja wanayoitoa sidhani kama inawatendea haki Watanzania,” alisema Khalifa na kuongeza:
“Chadema wanatakiwa kutambua kuwa, kilichopo Zanzibar ni serikali ya umoja wa kitaifa sio serikali ya mseto, kama hawataki sawa…sisi hatuko rasmi kama wao. Tutaendelea kuwawakilisha wananchi kwa kuwa ndio kazi ya mbunge.
”
Akitolea ufafanuzi habari zilizoenea kwamba wamewasilisha kwa spika maombi ya kutaka kubadilishwa kwa kanuni za bunge ili kuondoa neno ‘kambi rasmi bungeni’ ili nao watambuliwe, alisema suala hilo ni gumu kupatiwa ufumbuzi.
“Ili chama kiweze kuunda kambi hii, lazima kiwe na wabunge zaidi ya 45, yaani asilimia 12 ya wabunge wake wote, Chadema wamefikisha hilo, sisi tumepeleka hoja tu ila hatujapeleka pendekezo. Kanuni zinatakiwa kutizamwa upya ili kukidhi haja,” alisema Khalifa.
Khalifa aliungwa mkono na Mbunge wa Mkanyageni (CUF), Mohammed Habib Mnyaa, ambaye alifafanua kwamba CUF ilikubali kuwa kitu kimoja na vyama vingine wakati kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni alipotokea kwenye chama hicho.
0 comments