VITA ya CUF na Chadema iliyotokana na Chadema kutotaka ushirika na vyama vingine kwenye kambi yake ya upinzani, imehamia bungeni baada ya wabunge wa vyama hivyo jana kupeana mipasho katika Kikao cha Kwanza cha Mkutano wa Bunge la Kumi, ulioanza mjini Dodoma.
Kabla ya mkutano huo wa Bunge, Chadema ilieleza kuwa imeamua kuvitenga vyama hivyo kwa kuwa vinashirikiana na CUF ambayo kwa mtazamo wake, haina tofauti na CCM. "CUF na CCM wameamua kuungana Zanzibar na kuunda Serikali ya Mseto na kwa kuwa sheria ya vyama ya Zanzibar ndiyo inayotumika pia Tanzania Bara, Chadema imeona CUF na CCM ni wamoja," alieleza Katiba Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alipokuwa akitoa tamko la Kamati Kuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam mwezi uliopita.
Hata hivyo, siku chache baadaye CUF, ilifanya mkutano na waandishi wa habari na kueleza kuwa haina mpango kuilamba miguu Chadema ili iwaunganishe kwenye kambi hiyo ya upinzani, badala yake inaandaa barua kuliomba Bunge lipitishe kuwa na kambi mbili za upinzani bungeni.
Hoja hiyo jana ilifanya mkutano kuanza kwa moto pale Naibu Spika, Job Ndugai alipowasilisha azimio linalotoa tafsiri ya nini maana ya 'Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni' akitaka lipitishwe na Bunge hali ambayo ilitafsiriwa kuwa ni mkakati wa "kuivunja nguvu za kisheria Chadema".
Mkutano huo ulitoa tafsiri inayobainisha kuwa kambi rasmi ya upinzani bungeni ni mjumuiko wa wabunge wote wa upinzani bila kujali vyama wanavyotoka hivyo kutoa fursa kwa wabunge hao kuwa na haki ya kuchaguliwa kuongoza kamati tatu za bunge zinazohusika na Hesabu za Serikali.
Kamati hizo kwa mujibu wa kanuni za Bunge ni Kamati ya Bunge ya Serikali za Mitaa (LAAC), Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) na Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC).
Hata hivyo, tafsiri iliyoongezwa katika kanuni hizo za Bunge haimwondolei uwezo Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe kuteua wabunge anaowataka pale atakapokuwa akiunda Baraza la Mawaziri Kivuli.
Wakati wa mjadala huo, baadhi ya wabunge waliugeuza Ukumbi wa Bunge kuwa jukwaa la mipasho na mabishano.
Hali hiyo imejitokeza baada ya michango ya wabunge hao kuingiliwa kati na kukatishwa na wenzao waliokuwa wakichomeka maneno ya kebehi bila utaratibu, huku wengine wakiomba mwongozo wa spika na kutoa taarifa kadhaa. Mjadala huo ulimlazimu Spika wa Bunge, Anne Makinda kusimama mara kwa mara na kutoa maelezo huku akionekana kuachia baadhi ya vijembe na kebehi zilizopenyezwa na wabunge hao.
Mabadiliko hayo yaliyogusa kanuni ya 15 kifungu cha kwanza yametokana na Msimamo wa CUF na NCCR Mageuzi kutaka Bunge liwe na kambi mbili za upinzani. Naibu Spika wa Bunge, Ndugai aliewaeleza wabunge kuwa maombi hayo yaliyowasilishwa bungeni na Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila na Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed.
"Maneno ya kambi rasmi ya upinzani sasa yatasomeka, kambi inayoundwa itakuwa ni ya vyama vya upinzani vyenye wawakilishi bungeni," alisema Ndugai na kuongeza: "Azimio la Kamati ya Kanuni ambayo mimi ni makamu wake inaona upo ulazima Kanuni za Bunge za mwaka 2007 zikaongezewa tafsiri na kutengua kanuni ya 15 kifungu cha kwanza."
Baada ya maelezo hayo ya Naibu Spika, Spika wa Bunge, Makinda ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni za Bunge alisimama na kueleza kuwa wenye uamuzi ni wabunge ambao watachangia hoja na baadaye kulipigia kura ambapo Kafulila alikuwa mchangiaji wa kwanza kati ya wachangiaji nane.
Akichangia hoja kabla ya kupigwa kura na kupitisha azimio hilo, Kafulila alisema mabadiliko aliyopendekeza yeye na Hamad Rashid, yataondoa mgogoro ulioibuka kati ya wapinzani na kuwezesha wabunge wengine kuwemo na kuchaguliwa kuongoza Kamati za Bunge na uwaziri kivuli.
Kafulila alisema wachache wanaopinga suala hilo, kimsingi hawana hoja zaidi ya ubinafsi wao na ubaguzi. "Wachache ambao wanapinga azimio la mabadiliko haya, sioni kama wana hoja zaidi ya ubaguzi. Kama leo wapinzani tumepata asilimia 20 ya viti tunapingana, je itakuwaje tukipata asilimia 60?," alihoji Kafulila huku akipigiwa makofi na wabunge wengi wakiwa ni wale wa CCM.
Aliongeza: "Tuonyeshe muafaka wa kitaifa, kama umepewa kidogo huonyeshi upendo, je ukipewa 60 itakuwaje. ni muhimu tufanye kazi pamoja tofauti zetu ziwe nje na si ndani ya Bunge, tukubaliane pamoja anayekwenda kinyume awajibishwe nasi NCCR tutakuwa watiifu kwa kiongozi wa upinzani.
Bunge hili ni alama ya demokrasia." Hamad Rashid alianza kuchangia hoja hiyo kwa kukanusha kuwa CUF sio kibaraka wa CCM. Aliunga mkono hoja hiyo na kueleza kuwa CUF nayo ina haki ya kuingia katika kambi ya upinzani kama ilivyo kwa Chadema.
Hamad awaita Chadema 'watoto'
Kiongozi huyo wa upinzani katika Bunge la Tisa alisema kuwa kinachowasumbua ndugu zao wa Chadema, ni hali ya mambo aliyoyaita ya 'kitoto' ambayo wanashindwa kufafanua mambo kwa utu uzima huku akikumbushia machungu ya Muungano kufuta kauli za Chadema wa wabunge wa Zanzibar wanachaguliwa na idadi ndogo ya wabunge.
Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee ambaye hotuba yake alichangia hoja hiyo huku ikikatishwa mara kwa mara na wabunge kutoka CCM na CUF wakitaka mwongozo wa Spika, alisema wabunge wa Chadema wanalazimishwa kuungana na watu ambao haikubaliani nao kimsingi, kikanuni na kwamba huo ni mpango wa CCM.
Mdee awabatiza wapinzani wengine 'CCM B'
"Huwezi kumlazimisha kiongozi wa upinzani bungeni, kuunda kambi ya pamoja na wabunge wa vyama vingine ambao kikatiba na kikanuni hawakubaliani, na kwamba wabunge hao ni sawa na 'CCM B' ,"alisema Mdee. Mdee ambaye alikuiwa akitumia maneno ya ukali wakati wote wa hotuba yake alisema kama mpango huo unalenga kuzima moto wa Chadema, basi hilo halitawezekana na kwamba moto wa chama hicho utabaki ule ule.
"Kama mpango, huo ni kuzima muziki wa Chadema, nawahakikishia kuwa hamtaweza kuuzima kwani muziki wa Chadema utakuwa mkubwa zaidi bunge hili. Hao CUF wanaotaka kutulazimisha, mbona wao mwaka 2005 waliunda kambi yao hadi walipolazimishwa, sasa waache unafiki," alisema Maneno hayo ya Mdee yalisindikizwa pia na kauli zisizo rasmi za wabunge waliosikikika wakisema, "Wanunue vyombo waanzishe bendi."
Akichangia mjadala wa azimio hilo,Tundu Lisu ambaye pia ni Mnadhibu wa Kambi rasmi ya upinzani bungeni pia alipinga azimio hilo na kwenda mbali zaidi akidai kuwa Bunge linataka kuwafungisha ndoa ya lazima ambayo wao Chadema hawaitaki.
Mbunge huyo wa Singida Mashariki alisema kubadilishwa au kutolewa kwa ufafanuzi ya kanuni hiyo, kunalenga kuua upinzani bungeni na kuhoji kuwa haiwezekani CCM ambayo inaongoza Serikali ikaweka utaratibu wa kuwaundia kamati za kusimamia fedha za umma.
"Hapa inaonyesha kuwa tunataka kufungishwa ndoa ya lazima kama walivyofanya kule ng'ambo ya bahari (Zanzibar), hivi kuna maana gani kwa mbunge anayetoka chama chenye mbunge mmoja katika nchi akapewa jukumu la kusimamia fedha za umma au mbunge kutoka Zanzibar ambaye wapiga kura wote wa wabunge hao hawafikii idadi ya wapiga kura wa mbunge mmoja tu John Mnyika wa Ubungo," alihoji Lisu na kuongeza: "....Kamwe haitawezekana, watu tunaotaka kuwaondoa madarakani, leo hii tuwape madaraka ya kutuundia kambi ya upinzani bungeni.
Hivi hapo tunategemea kupata nini ndani? Hapa tutapoteza usimamizi wa fedha za Serikali," alisema Lisu. Kauli hiyo ya Lisu ilimkera Mbunge wa Bariadi, Mashariki na mwenyekiti wa UDP, John Cheyo aliyeingilia kati, bila ruhusa ya spika na kusikika akisema, "This is not true, (hii si kweli), mimi nimeongoza kamati hiyo, kwa ufanisi na uadilifu mkubwa," alisema Cheyo na kutoa karipio akimtaka Lisu kufunga mdomo.
Cheyo ataka wabunge wa
Chadema wapunguze jazba
Katika mchango wake kabla ya Lisu, Cheyo aliwataka wabunge wa Chadema kupunguza hasira na jazba badala yake kukubaliana na wabunge wa vyama vingine kuwa mbunge yoyote wa upinzani anaweza kuongoza kamati za fedha. "Chadema punguzeni hasira ili tutengeneze bunge linalotegemewa na Watanzania wote, lakini na ninyi CCM kwa kuwa kura zimepita hebu tawaleni na mtu akitaka kuwaletea kitu cha ajabu mnyamazisheni mara moja," alisema Cheyo.
Wabunge wa CCM waliochangia hoja ya azimio la mabadiliko hayo ya Kanuni za Bunge walikuwa ni George Simbachawene (Kibakwe) na Angela Kairuki (Viti Maalum) ambao wote waliunga mkono mabadiliko hayo huku wakiitupia madongo Chadema kuwa kina ubinafsi.
Sent from my iPhone

0 comments