Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Mkuu wa Mkoa Dar ajuta ‘kuwatukana’ waandishi wa Habari

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter

KAIMU Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiq jana alijuta ‘kuwatukana’ waandishi wa habari baada ya baadhi yao, kuangua kilio mbele yake na kususia mkutano wake.  Waandishi hao, walisusa mkutano wake na kutimka, baada ya mkuu huyo, kuwataka waathirika wa mabomu ya Gongo la Mboto, wasiwaeleze shida zao kwa sababu waandishi wa habari, hawana msaada wowote kwao.

Sadiq alitoa kauli hiyo, muda mfupi baada ya waandishi wa habari waliokuwapo ofisi za Kata ya Ukonga ambako Zainab Kilo, alilalamika hajapata msaada wowote tangu kutokea kwa mlipuko wa mabomu katika Kambi ya JWTZ, Gongo la Mboto Februari 16, mwaka huu. 

Mwanamama huyo ambaye alionekana kuwa na jazba, alisema mjukuu wake Tizo Bisona (12), alipata majeraha kichwani na mgongoni, lakini tangu siku ya tukio mpaka leo (jana), alikuwa  hajapata msaada wowote licha ya kumpeleka mtoto huyo, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa matibabu kwa gharama zake.

“Mimi mwanangu ameumia kichwani na pia ameungua mgongoni, naishi eneo la Mzambarauni, lakini nashangaa mpaka leo, sijapata msaada wowote ule,”alisema Zainab.  Kauli ya Zainab aliyokuwa akiitoa kwa baadhi ya waandishi wa habari, ilimkera Sadiq ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi ya Mkoa na kuamua  kusimama na kumueleza mama huyo, kwamba waandishi wa habari, hawawezi kumsadia.

  “Maneno ya huyo mama yanaweza kuonyesha kwamba watu wote wa Gongo la Mboto hawapati msaada wowote, hao waandishi unaozungumza nao hawawezi kukusaidia lolote.

“Zaidi utakuta katika magazeti na Televisheni wameandika habari hizo,”alisema Sadiq.
  Kauli hiyo, iliwafanya baadhi ya waandishi wa habari kunyanyuka katika viti kwa jazba huku wengine wakitokwa na machozi na kusimama pembeni  huku wakilaani kitendo hicho, na kufafanua si cha  kiungwana na kimewashushia hadhi.

“Hajatutendewa haki hata kidogo, huu ni unyanyasaji, hawezi kusema sisi hatuwezi kusaidia lolote, eti hata unga hatuwezi kusaidia, ana maanisha nini,  hapa tuwe na msimamo dharau katika fani hii imezidi,” alisikika akisema mmoja wa waandishi hao. 

Baada ya kuona kuwa amekosea, Sadiq alimtuma mmoja wa watu waliokuwa katika ofisi hizo ili awaite waandishi hao, awape ufafanuzi wa kauli yake, lakini ombi hilo, lilikataliwa na waandishi hao, na Sadiq kulazimika kuwafuata  mahali walipokuwa wamesimama huku akiongozana na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova.

“Naona nimeeleweka vibaya, nilizungumza vile ili kutaka kumuonyesha yule mama kuwa kauli alizokuwa akitoa si sahihi, nieleweni jamani sijawanyanyasa kama ni ulimi umeteleza naomba mnisamehe,”alisema Sadiq.  Sadiq alisema kauli ya Zainab inaonyesha kuwa wapo waathirika wengi wa milipuko ya mabomu ambao bado hawajapatiwa msaada na kusisitiza kuwa ni changamoto kwao ili kuwafikia watu hao.  “Hata Chenge aliwahi kutoa kauli ya ‘vijisenti’ ikamletea matatizo, ni kauli tu. Ulimi umeteleza,” alisisitiza.

Akizungumzia hali hiyo, Kamanda Kova alitaka kauli ya Sadiq kutogeuzwa tukio kubwa  na kuwaomba waandishi walichukulie jambo hilo kuwa la kawaida kwa kuwa Kaimu Mkuu huyo wa mkoa, ni mtu mtaratibu.  “Jamani chukulieni hili jambo kama la kawaida, lengo lake halikuwa hilo, si kama amewakashifu,  tupo hapa kwa ajili ya kusaidia watu si vinginevyo,” alisema Kova.

Baada ya kauli hizo, Kova na Sadiq, walimtuma mmoja wa mabinti waliokuwa eneo hilo, kuwaandika majina waandishi wa habari waliokuwapo eneo hilo bila kufafanua majina hayo, yalihitajika kwa kazi ipi.

Baadhi ya waandishi wa habari si wa gazeti hili, walibaki na kuanza kuandika majina hayo na kupeleka karatasi hiyo, ndani ya jengo hilo, huku wengine wakipanda katika magari  na kuondoka kwa hasira katika eneo hilo.

Tags:

0 comments

Post a Comment