JOPO la uangalizi wa shughuli za Bunge kutoka Kituo cha Sheria na Haki za binaadamu (LHRC) limesema wamesikitishwa na kitendo cha Bunge la Kumi linaloendelea jijini Dodoma kuchakachua baadhi ya kanuni na kubadilisha maana na tathmini ya sura nzima ya kanuni hizo.
Hayo yalisemwa juzi na mmoja wa waangalizi wa shughuli hizo, Deus Kibamba, wakati wa sherehe za uzinduzi wa ripoti ya tathmini ya utendaji wa Bunge la Tisa zilizofanyika katika kituo cha Sheria na Haki za Binaadamu.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili mara baada ya sherehe hizo, Kibamba alisema Bunge la Kumi limeanza kuchakachua kanuni zilizobadilishwa mwaka 2007 ambapo wabunge kutoka chama cha upinzani wakitimia asilimia 12 wanaweza kuunda kambi ya upinzani lakini Bunge limebadilisha kanuni hiyo hadi kubadili sura nzima ya kanuni hiyo.
“Tumesikitishwa sana na kitendo cha Bunge la Kumi cha kubadilisha kanuni ambayo ilirekebishwa na Spika aliyepita wa Bunge la Tisa ambapo kanuni hiyo ilisema wabunge wa upinzani wakitimia asilimia 12 wanaweza kuunda kambi ya upinzani lakini tumeshuhudia CHADEMA ikichakachuliwa na kurekebishwa kwa kanuni hiyo,” alisema Kibamba.
Pia alisema kanuni na sheria za Bunge zinasema kambi ya upinzani inaweza kuchagua wenyeviti wa kamati tatu muhimu wanazopewa lakini cha ajabu chama tawala kimewachagulia kambi ya upinzani wenyeviti wa kamati hizo.
Akitoa mfano wa wenyeviti waliochaguliwa na chama tawala ni Mbunge wa Bariadi Mashariki John Cheyo ambaye alishawahi kufukuzwa kazi na kambi ya upinzani katika Bunge lililopita jambo ambalo alisema halijawatendea haki kambi ya upinzani ya kumjadili na kufanya maamuzi ya kumrejesha au laa.
Pia alieleza kusikitishwa kwake na kitendo cha vyama vingine vya upinzani kufurahia chama tawala kuchakachua kanuni na kuweza kuzibadilisha kwa ajili ya maslahi yao binafsi.
Aidha alisema kitendo cha kumchagua Mbunge wa Monduli, Edwad Lowassa, kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Mambo ya Nje Ulinzi na Usalama ambayo Mbunge wa Urambo mashariki Samwel Sitta ni mmoja wa wajumbe inaashiria kuwa Bunge la Kumi ni la kulipana visasi na kukomoana.
Wakati huohuo, Baraza la Vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAVICHA) limemtaka Spika wa Bunge, Anne Makinda, kuongoza Bunge kwa kufuata kanuni na taratibu za Bunge na si kuongozwa kwa itikadi ya chama chake.
Hayo aliyasema jana Katibu wa Baraza la Vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAVICHA) Ally Chitanda wakati wa kutoa tamko la mustakabali wa wabunge wa chama hicho kwa juhudi wanazozionyesha bungeni katika kutofautiana na wabunge wa vyama vingine vya upinzani.
Alisema kuanzia Bunge lilipoanza wabunge wa CHADEMA wameonyesha msimamo kwa kuonyesha kile wanachokihitaji kwa maslahi ya Watanzania kwa kutokubaliana na hoja za wabunge wengine.
Chitanda alisema kuwa mwenendo wa Bunge unaonyesha Spika Makinda anashindwa kuliongoza kutokana na kukifuata chama chake katika kutaka kupunguza makali ya wabunge wa CHADEMA.
“Tunataka Spika kufanya kazi zake kwa utashi na misingi inayopaswa kuendesha Bunge kama mhimili unaojitegemea, hii italeta heshima kwa chombo hicho na kuachana na itikadi au shinikizo kutoka upande fulani kwa maslahi binafsi,” alisema Chitanda

0 comments