Subscribe to receive latest Updates
Stories: 3163
Comments: 284

Online :

You Are Here: Home - - Mahakama yakataa vielelezo 14 vya Mengi dhidi ya Manji

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, imetupitilia mbali nyaraka 14 zilizowasilishwa na Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi, kwa sababu hazina msingi.

Katika nyaraka hizo 14 zilizotupiliwa mbali na Hakimu Mkazi, Aloyce Katemana, upo mkataba kuhusu Kampuni ya Quality Finance Cooparation Group na Kagoda Agriculture.

Akitoa uamuzi huo jana, katika kesi ya madai ya Sh1 iliyofunguliwa na Yusuf Manji dhidi ya Mengi, Katemana alisema anazitupilia mbali nyaraka hizo kwa sababu hazimhusu Manji na hazina kibali kutoka kwa ofisa wa serikali.

Uamuzi huo ulifuatia Wakili wa Manji, Mabere Marando, kuomba mahakama kufuta nyaraka hizo zilizowasilishwa na Mengi kwa sababu haziendani na sheria za mahakama.

Marando alidai kuwa, sheria inakataa nakala zisizo halisi, lakini ipo sheria ambayo inaruhusu kuomba kibali ambacho ilitakiwa upande wa Mengi wakipeleke kabla ya kuanza kusikilizwa kwa kesi hiyo.

“Na kama waraka unahusu serikali, unatakiwa ufanyiwe marekebisho na ofisa aliyetoa nyaraka hizo na inatakiwa zilipiwe, lakini upande wa Mengi vitu hivyo vyote havijafanyika,” alidai Marando.

Aliongeza kudai kuwa, kutokana na hoja hizo, nyaraka zote zilizopelekwa mahakamani hapo na upande wa Mengi hazina msingi, ziondolewe mahakamani na kwamba, zinawapotezea muda kwa kuwa haziendani na sheria.

Pia, Marando aliutaka upande wa Mengi ueleze ulikozipata risiti za malipo za serikali kuhusu Kampuni ya Quality Finance Cooparation Group na aliyempa.

“Kuna mkataba kuhusu Quality Finance Cooparation Group na Kagoda Agriculture, lakini haumhusu Manji kwa sababu kesi hii inahusu udhalilishaji mtu na mtu sio mtu na kampuni,” alidai Marando.

Baada ya Marando kutoa hoja hizo, Wakili wa Mengi, Michael Ngaro, alizipinga hoja hizo zilizotolewa na jopo la mawakili wa Manji, Marando, Richard Rweyongeza na Ringo Tenga kwa madai kuwa, vielelezo hivyo vilitolewa wakati usio muafaka na aliomba mahakama isubiri muda ambao shahidi husika atafika kuthibitisha mahakamani.

Lakini akina Marando walipinga hoja hiyo na Hakimu Katemana alifikia uamuzi wa kuvitupilia mbali vielelezo hivyo.

Baaada ya kutolewa uamuzi huo, Ngalo aliomba mahakama kutumia busara kumruhusu aweze kukata rufani Mahakama Kuu dhidi ya uamuzi huo.

Wakati yote hayo yakiendelea mahakamani hapo, Manji alikuwa amekaa akisikiliza kwa makini.

Awali, mahakama hiyo ya Kisutu ilishuhudia mkanda wa video (DVD) wa hotuba ya Mengi wakati akizungumza na waandishi wa habari na alimtaja Manji kuwa ni miongoni mwa mafisadi Papa wanaohujumu nchi.

Watuhumiwa wengine waliotajwa kwenye mkanda huo na Mengi kuwa mafisadi papa, ni Mbunge wa Igunga na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CC-CCM) na Halmashauri Kuu ya Chama hicho (NEC-CCM) Taifa, Rostam Aziz.

Wengine ni wafanyabiashara, Tanil Somaiya, Jeetu Patel na Subash Patel, ambao alisema wanatuhumiwa kuiba mabilioni ya wananchi na kuzihamishia nje ya nchi.
Tags:

0 comments

Post a Comment