![]() |
Mkuu wa Majeshi Mstaafu, George Waitara, na Mkuu mpya wa Mafunzo na Utendaji Kivita, Luteni Jenerali Seni Hinda, wakitafakari jambo |
Hayo yalisemwa jana kwa nyakati tofauti na Mkuu wa Usalama na Utambuzi Brigedia Jenerali Paul Meela na mtaalamu wa milipuko wa jeshi hilo Brigedia Jenerali Leonard Mdeme kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi hilo, Davis Mwamunyange, wakati wakizungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari katika ofisi za makao makuu ya jeshi hilo Upanga, jijini Dar es Salaam.
Viongozi hao wa jeshi walikuwa wakizungumzia tukio la milipuko ya mabomu iliyotokea katika kambi ya 511 KJ Gongo la Mboto, jijini Dar es Saalam.
Kauli yao hiyo ya kutojiuzulu, ilitokana na swali aliloulizwa na mmoja waandishi wa habari aliyehoji kwa nini Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk.Hussein Mwinyi, na Mkuu wa Jeshi hilo, Davis Mwamunyange, wasijiuzulu kutokana na milipuko hiyo.
Brigedia Jenerali Meela kwanza aliwataka wanahabari watambue kuwa ajira ya jeshi ni tofauti kabisa na ajira ya siasa, serikali wala sekta binafsi nakufafanua kwamba jeshi linaongozwa na Sheria ya Ulinzi wa Taifa No.24 ya mwaka 1964 ambayo inaainisha utendaji kazi wao na jinsi ya kuingia kazini, kupanda vyeo na kuondoka kazini.
“Na mbaya zaidi sisi JWTZ siyo kama watumishi wa serikali na sekta binafsi; tunaongozwa na sheria hiyo na ndiyo maana hata siku moja hamjasikia wanajeshi wanaungana na baadhi ya watumishi wa serikali kugoma, wala kuandamana kudai kuongezewa maslahi…hivyo basi sheria hiyo haimtaki kiongozi wa jeshi kujiuzulu kama baadhi ya watu wanavyotaka.
“….huku kwetu kuna kuwajibika pindi inapotakiwa uwajibike siyo kujiuzulu…na hadi sasa bado haijabainika nini chanzo cha milipuko hiyo hivyo tuachane na maneno yanayozagaa na hisia ambazo hazijengi nchi tusubiri ripoti ya uchunguzi ndiyo itatupa jibu,” alisema Brigedia Jenerali Meela.
Meela alisema jeshi limepokea taarifa hiyo ya mlipuko kwa masikitiko na linatoa pole kwa wahanga na pia na kuutaka umma uelewe kwamba hata jeshi pia limepata madhara kwani nyumba zake mbili, maghala yake yameteketea, askari wake wanne wameumia na kwamba tukio hilo ni ajali.
“Hivyo basi napenda kutangaza rasmi kwamba kufuatia kutokea kwa tukio hilo Kikosi Kazi kimeundwa kwa ajili ya kuchunguza chanzo cha milipuko na kikimaliza kazi yake kitatoa taarifa ya nini walichobaini…. tunawaomba wananchi hasa nyie waandishi wa habari muwe na subira katika kujadili tukio hili na muache kasumba ya kudhania kitu hiki ama kile ndicho kilisababisha milipuko ile kwani mkifanya hivyo mtakuwa mnaliyumbisha taifa,” alisema Brigedia Jenerali Meela.
Kwa upande wake Brigedia Jenerali Mdeme alikanusha vikali swali aliloulizwa na mmoja waandishi wa habari kwamba mabomu yale yalikuwa yakihifadhiwa kama mahindi na kwamba chanzo cha mlipuko ule ni joto kali lilosababishwa na mgawo wa umeme na kwamba tangu mwaka 1975, JWTZ haijawahi kupeleka wanajeshi wake nchi za nje kwenye mafunzo.
“Jamani! hizo taarifa ni za uongo na hazina ukweli wowote; mabomu yetu hatuyahifadhi kwa njia hiyo uliyoisema na kwa taarifa yenu sasa mimi ni mtaalamu wa milipuko na baada ya mlipuko ule kutokea nilikesha pale kufanya ukaguzi, nasema hivi kama mwanataaluma wa milipuko, mabomu yanaweza kuishi bila kulipuka hata kwenye joto kali sana ambalo hapa nchini kwetu hakuna joto hilo…na kila siku jeshi linapeleka wasomi nchi mbalimbali kusomea masula hayo kwa hiyo hilo swali lako halina ukweli wowote.
“…na muelewe milipuko inatofautiana na kuzuia milipuko isitokee ni kazi ngumu sana kuliko mnavyofikiri na tukio la Gongo la Mboto ni tofauti kabisa na lile la Mbagala,” alisema Brigedia Jenerali Mdeme.
Aidha Meela alikanusha kuwa ndani ya jeshi kuna baadhi ya wanajeshi wanajihusisha na masuala ya siasa na kuwataka waandishi wenye orodha ya majina ya wanajeshi wanaojihusisha na masuala ya kisiasa wampatie ili waweze kushughulikiwa.
Akizungumzia taarifa zilizozagaa mitaani kwamba wanajeshi wanaficha taarifa za idadi kamili ya vifo vilivyotokea ikiwa ni pamoja na wanajeshi wake, alisema si kweli kwamba wanaficha siri.
Katika hilo alikanusha kuwa hakuna mwanajeshi aliyekufa katika tukio hilo na kwamba kanuni za jeshi zinalitaka jeshi hilo kutoa taarifa za vifo vya askari wake.
![](http://www.blogger.com/img/icon18_edit_allbkg.gif)
0 comments