Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - JK: Tutazingatia ushauri wa wabunge kuhusu Dowans

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
HATIMAYE Rais Jakaya Kikwete amelitolea ufafanuzi suala la Kampuni ya kufua umeme ya Dowans akisema Serikali itazingatia ushauri wa Kamati ya Wabunge wa CCM iliyokaa hivi karibuni.

Akihutubia wanachama wa CCM wakati wa kilele cha maadhimisho ya miaka 34 ya chama hicho zilizofanyika kitaifa Dodoma jana, Rais Kikwete alisema Serikali yake iko makini kutafuta ufumbuzi wa tatizo la Dowans ambao hautaleta madhara makubwa kwa wananchi.

Akitoa historia juu ya kilichosababisha nchi kutafuta ufumbuzi wa haraka, Rais Kikwete alisema alipoingia madarakani, miongoni mwa changamoto zilizojitokeza, ni ukame uliosababisha kukauka kwa vyanzo vya maji na hatimaye nchi kuingia gizani.

Alisema mavuno ya chakula yalikuwa mabaya na kukawa na njaa kali ambapo watu 3,776,000 walilazimika kuhudumiwa na Serikali. Aidha, mito mikubwa na midogo ikapungukiwa sana maji na mingine kukauka kabisa.

Alisema jitihada zilifanyika na moja ya hatua ilikuwa ni kutafuta kampuni ambayo ingeweza kupata suluhisho la haraka na ndipo mchakato ulipofanyika wa kumpata mzabuni ambaye angefanya kazi hiyo.

“Mimi nilitilia shaka nilipoambiwa kwamba Kampuni ya Richmond iko tayari, lakini wanataka tuwalipe kwanza dola milioni 10.

Niliwambia walete hiyo mitambo, kisha sisi tuwalipe. Shaka yangu ilikuwa ni ya kweli, kwani badala ya kuleta mitambo, wakauza mkataba huo kwa Dowans,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:

“Hawa Dowans ni kweli walileta mitambo na umeme ukapatikana, lakini suala likaja, je hawa walioingia mikataba nao si ilikuwa kampuni ya mfukoni?

Ndipo Bunge likalazimika kuunda tume na ikagundulika kwamba Richmond kweli ni kampuni ya mfukoni”.

Hata hivyo, Rais Kikwete alisema badala ya watu kutafuta jinsi ya kutatua tatizo lililopo mbele yao, wakawa wanamhusisha kuhusika na Kampuni hiyo ya Dowans.

“Yapo maneno mengi eti mbona Rais yuko kimya sana, hatujamsikia kusema chochote? Niseme nini zaidi na hao wote wameshasema kwa niaba yangu? Wapo wanaosema niko kimya kwa sababu nahusika na Downs, na eti ndiye mwenyewe hasa.

Wapo wanaosema niko kimya au nashindwa kuchukua hatua, kwa sababu marafiki zangu wamehusika, nawalinda, ” alisema Rais Kikwete na kuongeza:

“Jambo ninalotaka kulizungumzia sasa sikutaka kulizungumza, kwa sababu Waziri Mkuu alishalifafanua baada ya semina ya wabunge wa CCM na hata John Chiligati, Katibu wa Siasa na Uenezi Taifa alishalizungumzia.

Sikuona umuhimu wa kufanya hivyo kwa sababu viongozi wenzangu hao wameelezea kwa ufasaha uamuzi wa Kamati Kuu na ule wa kikao cha pamoja cha wabunge wa CCM”.

Akiweka msimamo juu ya kutohusika kwake na Dowans, Rais Kikwete alisema: “Napenda kuwahakikishia wana-CCM na wananchi wenzangu, kuwa sina uhusiano wowote wa kimaslahi kwa namna yoyote ile na Kampuni ya Dowans.

Sina hisa zozote wala manufaa yoyote yale. Pia sina ajizi wala kigugumizi cha kuchukua hatua kwa sababu ya rafiki yangu au hata kama angekuwa ndugu yangu kahusika”.

Alisema uamuzi uliofanywa na Kamati Kuu na Kamati ya Chama ya Wabunge wa CCM ulifanywa chini ya uongozi wake na hivyo; “ ni uthibitisho tosha wa ukweli huo.

Waliokuwepo kwenye vikao hivyo wanajua ukweli wa haya ninayosema. Ningekuwa na maslahi au hofu tusingefanya uamuzi ule.”

Alisema anachobaini katika sakata hili ni yeye kukubaliana na ombi la Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kwa wakati huo ambalo liliiomba Serikali igharamie ukodishaji wa mitambo kutoka nje, jambo ambalo alisema lilikubaliwa kulingana na hali halisi.

Aliongeza: “Ili kukabiliana na tatizo hilo, ushauri ulitolewa na Tanesco nasi tukaukubali kuwa wakodishe mitambo ya kuzalisha umeme kutoka nje.

Serikali tukaombwa kugharamia ukodishaji huo. Taratibu za kisheria zikafanywa, tenda zikatangazwa na washindi wakapatikana Aggreco, Richmond na Alstom.

Kampuni za Aggreco na Alstom zilileta mitambo yao kwa wakati, lakini Richmond ikawa
inasuasua.

“Wakati huo huo maneno mengi yakawa yanazagaa kuhusu Richmond kutostahili kupewa tenda kwa sababu ya kutokuwa na uwezo na kutokuwa hai.

“Ikadaiwa kuwa wamepewa tenda kwa sababu ya kubebwa na baadhi ya viongozi serikalini. Maneno hayo yalifanya Wizara ya Fedha isite kutoa fedha za kuanzia kwa kampuni hiyo.

“Aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini wakati ule alipokuja kuniomba niingilie kati ili kampuni hiyo ilipwe malipo ya awali nikakataa na kumwambia Waziri aachane nao kwani kampuni hiyo ni ya shaka”.

Rais Kikwete alisema hata hivyo Richmond haikulipwa malipo hayo kwa kushindwa kutimiza mkataba, ingawa alisema maneno yalizidi kadri makali ya kukosa umeme yalivyoendelea kuuma.

Aliongeza kwamba baada ya hapo Kampuni ya Richmond ikauza mkataba wake kwa Dowans ambayo ilileta mitambo na uzalishaji umeme ukafanyika na kupunguza kabisa makali ya mgawo.
Tags:

0 comments

Post a Comment