• ASEMA KANUNI HAZIRUHUSU, AWASHAURI WAUNGANE
SPIKA wa Bunge Anna Makinda amesema ni jambo lisilo wezekana kuwepo na kambi zaidi ya moja ya upinzani bungeni.
Makinda alisema hayo alipokuwa akijibu swali la mwandishi wa gazeti hili aliyetaka kujua kanuni na sheria za Bunge kuhusu uundwaji wa kambi mbili za upinzani bungeni kama wanavyotaka kufanya wabunge wa Chama cha Wananchi wakishirikiana na wale wa NCCR-Mageuzi.
Juzi aliyekuwa kiongozi wa Kambi ya Upinzani wakati wa Bunge la tisa Hamad Rashid (CUF) na Mbunge wa Kigoma Kusini David Kafulila (NCCR-Mageuzi), waliungana kuweka azimio la kutaka kuwepo na kambi ya upinzani isiyo rasmi bungeni kwa madai kuwa CHADEMA imejitenga nao.
Akitoa ufafanuzi huo Dar es Salaam jana wakati wa semina ya wabunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Spika huyo alisema kambi ya upinzani inayotambuliwa kwa mujibu wa kanuni za Bunge ni moja hivyo kuwa na kambi nyingine ni jambo lisilowezekana.
Alisema utaratibu wa kuwa na kambi ya upinzani ni uwepo wa asilimia 12.5 ya wabunge wa upinzani bungeni ambao kwa mujibu wa kanuni za Bunge ndio wenye uwezo wa kuunda kambi hiyo.
“Ni vizuri hivyo vyama wabunge wao wakakaa pamoja ili kuwa na kambi yenye nguvu kwa wapinzani wote… ili kuwa na kambi ya upinzani ni lazima upate asilimia 12.5 sasa CHADEMA wamefanikiwa katika hilo, kinachotakiwa ni kuridhia kwa jambo hilo,” alisema Spika huyo.
Aidha, alifafanua kwamba CHADEMA hawakukosea kuunda kambi ya upinzani lakini ni muhimu kuwa na kambi moja kama ilivyokuwa kwenye Bunge la tisa ambapo vyama vyote viliunda kambi moja yenye nguvu.
“…Unajua kazi kubwa ya upinzani ni kuhakikisha wanaibana serikali katika utendaji hivyo kitendo cha kutokuwa na kambi moja kutawafanya wabunge wengine kushindwa kujua sehemu kuunga mkono hoja mbalimbali zinazowasilishwa bungeni,” alisema.
Spika huyo wa kwanza mwanamke nchini alisema ili upinzani uwe imara na uweze kuibana vilivyo serikali wanatakiwa kujenga mshikamano miongoni mwao kwa kutakiwa kukaa pamoja na kupanga mikakati ya kuibana serikali.
Wakati Spika Makinda akisema hayo, Mkurugenzi wa Bunge na Halmashauri wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) John Mrema alisema viongozi wa chama hicho walikuwa kwenye kikao jana kujadili suala hilo na kwamba watatoa tamko lao mbele ya waandishi wa habari wakati wowote juma hili.
“Kwa sasa hatuwezi kulizungumza jambo hilo maana siku nzima ya jana tulikuwa tukifanya kikao na kati ya tulichokuwa tukijadili ni pamoja na jambo hilo ambapo tunategemea kukutana na waandishi kwa ajili ya kueleza tulipofikia,” alisema Mrema.
0 comments