Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - MAUAJI ARUSHA: Wakenya wamrukia Said Mwema

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter CHADEMA YAANIKA KILICHOSABABISHA VURUGU ARUSHA


FAMILIA ya raia wa Kenya, Paulo Njuguna Kayehe, aliyeuwawa na polisi kwa risasi wakati wa vurugu za kuvunja maandamano ya CHADEMA Januari 5 mwaka huu, imekuja juu dhidi ya Jeshi la Polisi, ikiitaka serikali ya Tanzania kuchunguza na kuwachukulia hatua waliohusika kumpiga risasi ndugu yao na kusababisha kifo chake.
Akizungumza mjini Arusha jana ndugu wa marehemu, Timoth Kitau Kayehe, alisema ndugu yao huyo hakuja Tanzania kwa ajili ya siasa, na kwamba polisi hawawezi kujitetea kwa matumizi mabaya ya risasi za mtoto kutawanya na kuua waandamanaji.
Alisema Kayehe alikuja Tanzania ‘kutafuta maisha,’ hivyo polisi wanapomhusisha na maandamano ya CHADEMA wanaibua hoja na hisia nyingine.
Alisema kutokana na umoja uliopo baina ya nchi wanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki, wanafamilia wanaomba uchunguzi wa kifo hicho ufanyike, na wahusika wachukuliwe hatua ili kulinda ushirikiano uliopo.
''Hatutegemei (hatutarajii) suala hili lifikie hatua ya kuhatarisha uhusiano ulipo baina ya nchi zote mbili za Afrika Mashariki kwa kuamini uchunguzi utafanyika na hatua zitachukuliwa kwa waliohusika juu ya suala hili''alisema Kayehe.
Naye Ofisa Ubalozi wa Kenya hapa nchini, Robert Mathenge, alisema kuwa mwili wa raia huyo wa Kenya Paulo Njuguna Kayehe ulitarajiwa kusafirishwa jana kwenda Nakuru, Kenya, kwa ajili ya mazishi katika eneo la Elbaru baada ya taratibu zote ikiwemo uchunguzi wa madaktari kufanyika.
Afisa huyo alisema baada ya kuwapata ndugu wa marehemu, wameshughulikia suala la uchunguzi na hatimaye wamekamilisha wakiwepo ndugu hao.
Baada ya kukamilika kwa taratibu hizo za uchunguzi CHADEMA kilimkabidhi ofisa huyo wa ubalozi rambirambi ya shiliungi milioni mbili kwa ajili ya kusaidia kusafirisha mwili huo nchini Kenya.
Akikabidhi fedha hizo mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema, alisema wao kama CHADEMA na kama walivyofanya kwa marehemu wengine wawili waliokwishazikwa, wameamua kutoa kiasi hicho cha fedha kama rambirambi yao.
''Tunatoa rambirambi hii kwa kuwa aliyefariki nae pia ni ndugu yetu kama wale wengine kwa kuwa sisi kama Afrika Mashariki sote ni ndugu hivyo tunawajibu wa kufanya hiki ambacho tunakifanya''alisema Lema.
Lema alisema kuwa marehemu Njuguna naye atabaki katika historia ya harakati dhidi ya haki za Watanzania kutokana na kifo chake kutokea wakati wa harakati za kudai demokrasia hapa nchini, kitendo ambacho alisema kimeacha fundisho, hasa ikizingatiwa kuwa hakuwa sehemu ya chama hicho, na haijulikani polisi walimkuta wapi kumpiga risasi.
Lema alisema inasikitisha kwamba polisi walimpiga risasi, halafu wakamwacha akigaragara bila kumpeleka hospitali, hadi baada ya saa tatu. Alifariki akiwa anapatiwa matibabu hospitalini.
Maaskofu wamuwekea ngumu Wassira
Katika kile kinachoonekana kumuwekea ngumu Waziri wa Ofisi ya Rais Mahusiano, Steven Wassira wakati akifanya majumuisho kuhusu sakala la mauaji na uchaguzi wa Meya mjini Arusha, maaskofu wameonekana kukataa kubadilisha msimamo wao wa awali wa kutomtambua meya wa jiji hilo.
Mara baada ya vurugu na vifo vya raia, maaskofu hao waliahidi kutotoa ushirikiano wowote kwa meya huyo, huku wakishinikiza kwamba uchaguzi urudiwe wakidai kwamba hakushinda kihalali.
Hata hivyo, Wassira akifanya majumuisho ya mazungumzo na maaskofu hao alisisitiza kuwa tatizo la kanuni humalizwa kwa kanuni, na kwamba uchaguzi wa meya hauwezi kurudiwa kama CHADEMA wanavyodai. Aliwataka wananchi watulie na kuijenga nchi kwa kuwa uchaguzi umepita.
Hata baada ya kauli hiyo ya Wassira, hakuna kiongozi wa dini aliyekuwa tayari kufuta kauli yao ya kutoutambua uchaguzi wa Meya Gaudence Lyimo.
Wassira alisema hata kama uchaguzi ukirudiwa CHADEMA hawawezi kushinda kwa kuwa CCM ina viti (16) na CHADEMA ina viti (14); ingawa ukweli ni kwamba CHADEMA wana viti 15. TLP wana viti viwili.
Lakini muda wote wa tamko lake hilo Maaskofu hao akiwemo Askofu Thomas Laizer (KKKT) na Askofu Josephat Leburu (Katoliki) walikaa kimya.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, alipozungumza na gazeti hili kuhusu kauli ya Wassira, alisema inaonyesha kuwa ni kiongozi mbabe asiyejua dhamana ya ofisi aliyokabidhiwa.
“Kiongozi yeyote mwenye hekima hawezi kufika Arusha leo, katika hali iliyopo, akatoa maneno ya namna hii, ya kejeli na kebehi,” alisema Mbowe.
Alisema Arusha ya sasa inahitaji kiongozi mpatanishi, si mbabe.
“Ni bahati mbaya tuna viongozi wababe na wachonganishi ambao wako tayari kupinda sheria za uchaguzi kwa maslahi yao. Kama Wassira hajui, lile si tatizo la Arusha tu, ni la kitaifa. Asicheze na akili za Watanzania wanapodai haki zao,” alisema.
Wakati huo huo, Wassira amemtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi Mkoani Arusha Thobias Andengenye kumaliza tatizo la waandishi wa habari kupigwa na Polisi na kuharibiwa mali zao katika maandamano ya wafuasi wa CHADEMA ya Januari 5 mwaka huu.
Siri ya machafuko Arusha yaanikwa
Katika hatua nyingine, mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba, jana alifafanua chanzo cha vurugu za Arusha, ili kuweka sawa rekodi ambazo zimekuwa zikipotoshwa na polisi, CCM na baadhi ya vyombo vinayoegemea serikalini au vinavyifanya propaganda za CCM.
Kwa mujibu wa Mwigamba, chanzo kikuu cha kuvurugika kwa uchaguzi wa meya Arusha, ni hatua ya mkurugenzi wa Jiji (msimamizi wa uchaguzi) kufanya hila za kuibeba CCM, na kuwaengua CHADEMA katika kinyang’anyiro cha uchaguzi.
Katika uchaguzi huo, CCM baada ya kugundua kuwa idadi ya madiwani wao isingeweza kuwahakikishia ushindi, walikula njama na mkurugenzi, wakafanya uchaguzi kwa kificho baada ya kuwakwepa CHADEMA ili wasipige kura.
Hali hiyo ilisababishwa na mvutano kati ya CCM na CHADEMA kufanya uchaguzi ushindikane mara mbili. Madai yaliyosababisha kushindikana kwa uchaguzi huo ni mawili.
Kwanza, CHADEMA walipinga uamuzi wa mkurugenzi kukataa kumwapisha diwani wa TLP, ambaye ilidhaniwa angeweza kukiongezea CHADEMA kura. Pili, CHADEMA walihoji sababu ya kumwapisha Mbunge wa Viti Maalumu kutoka Tanga, Mary Chatanda, na kukataa kumruhusu diwani wa TLP, mkazi wa Arusha. Wakataka Chatanda aondolewe, mkurugenzi akawakatalia.
Alisema awali CCM ilikuwa na wajumbe 15 na CHADEMA 14, huku TLP ikiwa na madiwani wawili.
“Ingawa walituzidi mtu mmoja, wao walikuwa wanahofia kuwa baadhi ya madiwani wao na wale wa TLP wangeipigia kura CHADEMA. Hiyo ingefanya sisi tushinde umeya. Kwa hiyo, wakaamua kumleta mbunge wao wa viti maalum wa Tanga, na wakati huo huo wakashirikiana na mkurugenzi kumzuia diwani mmoja wa TLP kupiga kura kwa maelezo kwamba hatambuliki, wakati diwani huyo alikuwa tayari ana barua ya utambulisho. Sisi tulipinga ukiukwaji huo wa taratibu, hasa wa kuzuiliwa kwa diwani wa TLP. Kwa hiyo, uchaguzi uliahirishwa.
“Lakini Mkurugenzi alikuja kuwaalika CCM peke yao kushiriki uchaguzi kwa kumpelekea barua kila diwani wao kama sheria na kanuni zinavyotaka. Madiwani wa CHADEMA hawakupewa barua za kikao hicho cha pili; badala yake barua zote zilipelekwa katika Bar ya Pentagon inayomilikiwa na diwani wetu, ambaye hata hivyo hakuwapo wala hakuzipokea. Kanuni zinataka kila diwani apewe barua yake na asaini kuthibitisha kwamba ameipokea lakini barua hizo ziliachwa kwa muhudumu wa Bar tena hata bila kusainiwa kama zimepokelewa,
Alisema kwa ukiukwaji huo wa kanuni na taratibu, madiwani na wabunge wa CHADEMA Arusha hawakuwa na taarifa kuhusu kikao hicho ambacho CCM kwa kumshinikiza diwani mmoja wa TLP walifanya uchaguzi wa umeya na naibu meya peke yao.
“Kwa hiyo, tunachokipinga Arusha si suala la Mary Chatanda bali ni ukiukwaji wa sheria na kanuni uliofanywa na mkurugenzi waziwazi ili kuwapa hawa jamaa ushindi,” alisema Mwigamba.
Vijana CHADEMA nao watoa tamko
Viongozi wa Baraza la Vijana wa CHADEMA (BAVICHA), Mkoa wa Dar es Salaam, umesema uko tayari kutumia nguvu ya umma kuwawajibisha viongozi waliohusika katika tukio la Arusha la polisi kuvunja maandamano ya amani ya chama hicho na kusababisha vurugu na mauaji ya raia.
Kauli hiyo, ilitolewa jana na Katibu wa BAVICHA, Renatus Mlashani, wakati akitoa tamko la baraza hilo kulaani maafa yaliyotokea mkoani humo.
Tamko lao hilo pia lililaani kauli nyepesi zilizotolewa na viongozi wa juu wa serikali akiwemo, Rais Jakaya Kikwete mbele ya mabalozi kwamba mauaji yaliyotokea ni ya bahati mbaya.
BAVICHA imedai kuwa kauli hiyo ilikuwa nyepesi kwani haikupaswa kutolewa na mkuu wa nchi kama yeye.
Kauli nyingine ni ya Waziri wa mambo ya Ndani Shamshi Vuai Nahodha, kwamba serikali ipo tayari kuzikutanisha pande mbili ili kupata suluhu, BAVICHA inadai kuwa kauli ilitakiwa kutolewa kabla ya maafa kutokea.
Mlashani alisema kutokana na kauli za viongozi hao, viongozi wa Jeshi la Polisi, akiwemo Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Said Mwema, Mkuu wa Operesheni na Mafunzo wa jeshi hilo Paul Chagonja na kauli za viongozi wa CCM, wanapaswa kuwajibika wenyewe na kama watashindwa kufanya hivyo wawajibishwe na umma.
Mlashani alisema kuwa, Chama chao kitaendelea kufanya maandamano ya amani na mikutano ya hadhara nchi nzima ili kuimarisha na kukuza demokrasiakwani ni haki yao kufanya hivyo.
Tags:

0 comments

Post a Comment