Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Dowans yamuibua Mama Maria Nyerere

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
•  ASEMA WANANCHI WATAICHUKIA CCM DAIMA

SAKATA la serikali kutaka kuilipa mabilioni ya fedha kampuni ya Dowans, limeendelea kuchukua sura mpya, ambapo safari hii mke wa Baba wa Taifa, Maria Nyerere, ameitaka serikali ya Rais Jakaya Kikwete isikimbilie kuilipa kampuni hiyo badala yake ivute subira.
Mjane huyo wa Baba wa Taifa, amesema serikali inapaswa kuvuta subira kwanza juu ya suala hilo na si kubariki malipo hayo kwa harakaharaka na kwamba iwapo Mahakama ya Usuluhishi ya Kimataifa (ICC), imeamuru, basi isiwe kigezo cha leo ama kesho kulipwa.
Mama Maria Nyerere alisema hayo juzi nyumbani kwake, Mwitongo Butiama, wilayani Musoma, Mara alipozungumza na waandishi wa habari waliokuwa wameambatana na msafara wa viongozi wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), kutoka mikoa ya Mbeya na Shinyanga.
Viongozi hao wa UVCCM waliotembelea nyumbani kwa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ni pamoja na kamanda wa umoja huo kutoka mkoa wa Mbeya, Mwakajumilo Isaac, na mjumbe wa Mkutano Mkuu Taifa wa UVCCM kutoka Wilaya ya Kishapu, mkoani Shinyanga, Dinawi Gabriel.
Katika ufafanuzi wake juu ya malipo hayo ya Dowans, Maria Nyerere alisema: “Licha ya Mahakama ya ICC kuiamuru Tanzania iilipe Dowans sh bilioni 94, ni vema serikali ikatafakari kwa umakini mkubwa na si kukimbilia kulipa!”
Alisema viongozi wa serikali na wana CCM kwa ujumla, wanapaswa kuliangalia kwa umakini zaidi suala hilo, ili lisije kuleta athari na kusababisha wananchi kukichukia chama hicho.
“Kwa hili la Dowans kutaka kulipwa, mimi nashauri serikali isikimbilie kulipa fedha hizo…bilioni 94 ni fedha nyingi na kama hawatafikiria kwa umakini mkubwa wananchi wanaweza kuichukia daima CCM.
“Tusikurupuke, tusikimbilie kuilipa Dowans….huu ndiyo ushauri wangu kwa serikali na wana CCM kwa ujumla,” alisema mke huyo wa Baba wa Taifa, huku akiwatania waandishi wa habari kwa kusema: “Ninyi mnataka ama hamtaki Dowans ilipwe?”
Hata hivyo, Maria Nyerere aliwataka viongozi wa CCM kurudia utaratibu wa zamani wa Baba wa Taifa wa kutumia vikao vyake vya ndani kukosoana, kukemeana na hata kuchukuliana hatua za kimaadili ili kuzima mambo ya chama kutoka nje.
“Baba wa Taifa aliwahi kusema kwamba bila CCM madhubuti nchi itayumba! Kauli hii ina maana kubwa sana kwa wana CCM waizingatie!” alibainisha.
Hata hivyo, alisema siku zote amekuwa akifuatilia na kusikiliza mambo ya Richimond, Dowans na EPA, lakini baadhi ya viongozi na wanasiasa wameonekana dhahiri kuchukizwa na kuamua kujitoa kupambana na mambo wanayoona hayana faida kwa taifa na wananchi wake.
Naye Mjumbe wa kamati ya utekelezaji wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Husein Bashe, alisema vijana hawapo tayari kuipokea CCM ikiwa chama cha upinzani hivyo ni vema viongozi waliopo madarakani wauambia umma kama wameshindwa kutekeleza sera za chama hicho kikongwe.
Alisema vijana wanasikitishwa na malumbano ya takriban miaka mitatu kuhusu kampuni za Dowans na Richmond kufua umeme wakati wananchi wakiendelea kukaa gizani kwa sababu ya kutokuwapo kwa umeme.
Alibainisha kuwa wimbo wa Dowans na Richmond umechosha na kama viongozi hawana jipya ni vema wakaachia madaraka ili kuwapisha wenye dhamira ya dhati ya kulitumikia taifa kwa maslahi ya wengi.
Alisema inasikitisha kuona wanafunzi wengi wa shule za kata wakifeli mitihani yao kwa sababu ya uhaba wa walimu, madawati, vitabu lakini viongozi hawashtuki na badala yake wamekuwa wakiendeleza wimbo wa Dowans na Richmond.
“Hatuko tayari kuipokea CCM ikiwa chama cha upinzani, tumechoshwa na matatizo tuliyonayo, viongozi wachape kazi na kama hawawezi waachie ngazi” alisema.
Wakati huohuo, Chama cha Wananchi (CUF) kinatarajia kufanya mandamano ya amani Jumatatu ijayo kupinga mpango wa serikali kuilipa kampuni ya Dowans.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Julius Mtatiro, alisema maandamano hayo yataanzia eneo la Buguruni na kuishia katika viwanja vya Kidongo Chekundu.
Maandamano hayo yatakayoongozwa na Profesa Ibrahim Lipumba na kuongozwa na viongozi wa kitaifa wa CUF ambao watahutubia maelfu ya waandamanaji na kutoa msimamo wa chama juu ya suala hilo.
Aidha, aliwataka wananchi, wanaharakati, mashirika mbalimbali na wapenzi wa CUF kujitokeza kwa wingi katika maandamano hayo.
Kuhusu kupata kibali kutoka Jeshi la Polisi, Mtatiro alisema tayari wameshalitaarifu jeshi hilo juu ya maandamano hayo kupitia barua yenye Kumbu.CUF/AK/DSM/NKM/B/002/A2/2011/08 ya Januari 28, mwaka 2011.
Alisema wanatarajia jeshi hilo halitajaribu kuhujumu maandamano hayo kutokana na ‘taarifa za ki-telijensia’ ambazo zimekuwa maarufu hivi karibuni.
Sakata la kulipwa kwa kampuni hiyo limekuja baada ya serikali kupitia Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, kutangaza kuamua kuilipa kampuni ya Dowans fedha hizo kama ilivyoamuliwa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi (ICC).
Tags:

0 comments

Post a Comment