IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
Waandishi Wetu
BAADA ya kumalizika kwa harakati za kusaka kura kwa wananchi, purukushani hizo sasa zinahamia ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano baada ya mbunge wa Urambo Mashariki, Samuel Sitta na wa Jimbo la Njombe Kusini, Anne Makinda jana walichukua fomu za kuwania nafasi ya Spika.
Mbali na wawili hao, mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Tambaza, Salim Kungulilo pia amechukua fomu ya kuwania uongozi wa taasisi hiyo muhimu ambayo ni moja ya mihimili ya nchi.
Kujitokeza kwa wanachama hao watatu kumekuja baada ya CCM kutangaza kuwa wanachama wake wanaweza kuanza kuchukua fomu za kuwania kiti hicho cha taasisi hiyo ya kutunga sheria.
Sitta, ambaye ameliongoza kwa mafanikio Bunge la Tisa, alichukua fomu hizo kwenye ofisi ndogo ya makao makuu ya CCM iliyo Mtaa wa Lumumba jijini Dar es salaam.
“Nina sifa zote za kuweza kuwa spika wa Bunge. Kazi niliyoifanya kwenye Bunge lililopita inajulikana, hivyo naomba kura kwa wabunge wote ili nimalizie kazi ambayo ilibakia katika ngwe iliyopita,” alisema Sitta mara baada ya kuchukua fomu.
Naye Makinda, ambaye alikuwa naibu spika kwa miaka mitano, alikataa kuzungumza lolote jana baada ya kuchukua fomu hizo badala yake amepanga kukutana na waandishi wa habari leo wakati anazirudisha.
Habari za ndani zimeeleza kuwa baada ya makada hayo kumaliza kujaza fomu hizo, Kamati kuu ya CCM itakutana Novemba 8 mwaka huu kuchuja majina ya wagombea kabla majina hayo hayajapelekwa kupigiwa kura kwa mujibu wa kalenda ya Bunge.
Akielezea changamoto mpya atakazopambana nazo katika Bunge jipya ambalo linaonekana kuwa na vijana wengi, Sitta alisema uwezo wa kupambana nayo kiuongozi anao na ndiyo maana alipewa jina la "chuma cha pua".
Akizungumzia jinsi uchaguzi jinsi ulivyoenda, Sitta alisema uchaguzi ulifanyika vizuri lakini kuchelewa kutangazwa kwa matokeo kumesababishwa na ukilitimba wa Tume ya Uchaguzi (Nec) kwa kutaka kuingiza matokeo kwanza kwenye mtandao wao na kusababisha wananchi kusubiri zaidi ya saa 48.
“Ukilitimba wa Nec ndiyo unaosababisha kuchelewa kwa matokeo... sioni sababu ya kuingiza kwanza kwenye kompyuta zao halafu ndiyo wawatangazie wananchi," alisema Sitta.
"Kufanya hivyo ndio kulisababisha watu kukesha usiku kucha na kujazana kwenye vituo vya kutangazia matokeo, jambo ambalo linaweza kusababisha chochote kutokea kwa kuwa wanaosubiri matokeo ni wananchi na wafuasi wa vyama mbalimbalimbali hivyo ni hatari.”
Sitta aliwapongeza wananchi ambao walivumilia ukiritimba huo wa Tume wa kuchelewesha matokeo, wengi wao wakikesha vituoni na kuongeza kuwa dosari hizo zote zilizojitokeza lazima atazizungumzia bungeni ili zibadilishwe kwa kuwa zinasababisha usumbufu na wakati mwingine vurugu.
Kuhusu ushindi kwenye jimbo lake, Sitta alisema: “Uchaguzi huu ulikuwa mgumu ndiyo maana tumeona watu maarufu tuliokuwa tunawafahamu wameangushwa. Kwa hiyo ushindi wangu hauna maana kwamba ulikuwa rahisi... ulikuwa mgumu kwa kwa hata wapinzani walijiandaa vya kutosha,.”
Akielezea maoni yake juu ya kujitokeza kwa idadi ndogo ya wapiga kura, Sitta aliitupia tena lawama Nec akisema kuwa kitendo cha kuendeshea zoezi la kupiga kura kwenye majengo ya serikali ambayo baadhi yako umbali wa kilomita 20, kulisababisha watu wengi waamue kutopiga kura.
“Naishangaa NEC... inalazimisha kuwa lazima kura zipigiwe kwenye majengo ya serikali tena imara; kwani wanaogopa nini, kwanza nchi yetu ni ya amani; kujifungia kwenye majengo imara ni ishara ya woga. Majengo hayo vijijini yapo mbali zaidi ya kilometa 20 na safari ya kwenda na kurudi ni kilomita 40. Mtu anaona bora asiende. Hata kama ana baiskeli, haiwezekani kwa sababu anakuwa na mkewe na watoto,” alisema Sitta.
Naye mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Tambaza, Salim Kungalilo jana alijitokeza kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa kugombea nafasi ya Spika.
Akizungumza jana baada ya kuchukua fomu, Kungulilo alisema amechukua uamuzi huo ili aweze kutoa mchango wake katika chombo hicho cha juu cha kutunga sheria nchini.
Kungulilo ambaye pia ni mwanasayansi Mtafiti alisema anao uzoefu mkubwa katika uongozi kwasababu amekuwa Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi.
You Are Here: Home - - Sitta,Makinda wachukua fomu za uspika CCM
0 comments