IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
NENO muafaka kuielezea siku ya leo ni 'hukumu' dhidi ya wanasiasa ambao walitumia kipindi cha takriban siku 70 kutangaza sera zao, kuchambua za wenzao ili wananchi wawachague kuongoza nchi. Hukumu hiyo itafanywa na wananchi ambao walikuwa wakifuatilia mikutano ya kampeni na taarifa zinazohusiana na Uchaguzi Mkuu wa nne tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi.
Uchaguzi huo unafanyika wakati CCM ikitaka kuendeleza ubabe wake kwa kuipa nafasi serikali ya awamu ya nne imalize kipindi chake cha miaka mitano, huku wapinzani wakitaka kumsimika rais wa awamu ya tano ambaye atakuwa wa kwanza kutoka upinzani tangu mfumo wa vyama vingi urejeshwe nchini mwaka 1992.
CCM kinataka mgombea wake, Jakaya Kikwete amalizie kipindi kingine cha miaka mitano na amejikuta kwenye mpambano mkali dhidi ya Dk Willibrod Slaa wa Chadema, ambaye aliacha ubunge wa Karatu na kujitosa kwenye kinyang'anyiro cha urais na Prof Ibrahim Lipumba wa CUF ambaye anawania nafasi hiyo ya juu kwa mara ya nne.
Wagombea hao watatu wanafuatiwa na Hashim Rungwe anayewania kiti hicho kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi, Peter Mziray Kuga (APPT-Maendeleo), Mutamwenga Mugaiywa wa TLP na Faham Divutwa wa UPDP ambaye hatakuwemo kwenye kinyang'anyiro hicho baada ya kutangaza kujiondoa juzi.
Visiwani Zanzibar, mpambano unaonekana kuwa baina ya mgombea wa CCM, Dk Mohamed Shein na wa CUF, Maalim Seif Sharrif Hamad. Lakini pia watakumbana na upinzani kutoka kwa Juma Ali Khatib (Tadea), Ambari Hamis (NCCR-Mageuzi), Haji Khami (NRA), Kassim Bakari Ali (Jahazi Asilia) na Said Soud wa Chama cha Wakulima (AFP).
Jumla ya watu 19,670,631 wanatarajiwa kujitokeza kwenye vituo vya kupigia kura Tanzania Bara na Visiwani kuchagua rais wa Jamhuri ya Muungano, rais wa visiwa vya Zanzibar, wabunge, wawakilishi, na madiwani watakaoongoza kwa kipindi cha miaka mitano ijayo. Kati yao wanaume ni 9,834,322 na wanawake ni 9,852,286.
Kwa upande wa Zanzibar, waliojiandikisha ni 407,000 kwa mujibu wa taarifa ya mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (Zec), Salum Kassim ni 407,000. Idadi hiyo ni sawa na asilimia 80.3 ya Wazanzibari wote wanaostahili kupigakura.
Lakini ni pungufu kwa tofauti ya asilimia 10.5 ya watu waliojiandikisha kupiga kura mwaka 2005.
Katika uchaguzi wa mwaka 2005, Kikwete aliibuka mshindi kwa kupata kura, 9,123,952 (80.28%), Ibrahim Lipumba (CUF) 1,327,125 (1.68%), Freeman Mbowe (Chadema) 668,756 (5.88%), Augustine Mrema (TLP) 84,901 (0.75%) Sengondo Mvungi (NCCR-Mageuzi) 55,819 (0.49%)
na Christopher Mtikila (DP) 31,083 (0.27%) Wengine ni Emmanuel Makaidi (NLD) 21,574 (0.19%), Anna Senkoro (PPT-Maendeleo)18,783 (0.17%) Leonard Shayo (MAKINI) 17,070 (0.15%), Paul Kyara (SAU) 16,414 (0.14%). Marais ambao wamewahi kuingoza serikali ya Jamuhuri ya Muungano hadi sasa ni Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliyeongoza awamu ya kwanza, Alhaj Ali Hassan Mwinyi awamu ya pili na Benjamin Mkapa.
Walioshiriki kuwania kiti cha urais katika uchaguzi wa mwaka 2005 Zanzibar ni Amani Abeid Karume (CCM)
aliyepata kura 239,832 sawa na asilimia 53.2, Shariff Hamad (CUF) 207,773 sawa na asilimia 46.1, Haji Mussa Kitole (Jahazi Asilia) 2,110 sawa na asilimia 0.5, Abdalla Ali Abdalla (DP) 509 sawa na asilimia 0.1, Simai Abdulrahman Abdulla (NRA) 449 sawa na asilimia 0.1 na Maryam Ahmed Omar (Sauti ya Umma) 335 sawa na asilimia 0.1.
Kwa upande wa Bara, kampeni zilikuwa na ushindani mkubwa na kwa muda mwingi zilitawaliwa na amani na utulivu, lakini kadri hamasa ilivyoongezeka miongoni mwa wanachama na wafuasi wa vyama, ndivyo munkari ulivyozidi. Hali hiyo ndiyo ilisababisha mtu mmoja kuuawa katika vurugu zilizotokea baina ya wafuasi wa CCM na Chadema wilayani Maswa, Shinyanga huku watu wengine kadhaa wakijeruhiwa kwenye vurugu zilizotokea Kilimanjaro, Mara, Dodoma na jijini Dar es salaam.
Mgombea wa ubunge wa Jimbo la Maswa Magharibi, John Shibuda ndiye aliyeathirika na vurugu za jimboni kwake baada ya Tume ya Uchaguzi (Nec) kuzuia mikutano ya kampeni ya chama chake siku tatu kabla ya muda wa kumaliza kampeni.
You Are Here: Home - - HUKUMU,watanzania kuamua
0 comments