Uturuki imetoa wito wa kufanyika kwa mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, baada ya wanaharakati wanaoiunga mkono Palestina kuuawa baada ya vikosi vya jeshi la Israel kuivamia meli iliyokuwa na misaada ya kibinaadamu kwa ajili ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza. Wakati huo uo, Uturuki imemuondoa balozi wake nchini Israel.
Uturuki imetoa wito wa kufanyika mkutano wa dharura kutokana na taarifa za kuwemo raia wa nchi hiyo miongoni mwa watu waliouawa katika uvamizi huo, ambapo taarifa za hivi punde zimesema kuwa baraza hilo litakutana baadae leo. Akihutubia kwa njia ya televisheni, Naibu Waziri Mkuu wa Uturuki, Bulent Arinc, amesema kulikuwa nahadi Waturuki 400 miongoni mwa watu 600 waliokuwemo ndani ya meli hiyo ya Kituruki ya Mavi Maramara wakati shambulio hilo lilipofanyika. Arinc amesema kiasi wanaharakati 10 waliuawa wakati wanajeshi wa majini wa Israel waliposhambulia moja kati ya meli sita zilizoko kwenye msafara ulioandaliwa na mashirika ya haki za binaadamu likiwemo lile la Uturuki. Kufuatia shambulio hilo kiasi Waturuki 10,000 waliandamana katika uwanja mkuu mjini Istanbul kupinga shambulio hilo.
Wakati Uturuki ikitoa mwito huo, mataifa mbalimbali duniani yamelaani vikali shambulio hilo lililofanywa na Israel dhidi ya meli. Rais Bashar al-Assad wa Syria na Waziri Mkuu wa Lebanon, Saad Hariri kwa pamoja wamelaani shambulio hilo wakisema kitendo hicho ni cha kihalifu. Assad na Hariri wameutolea mwito Umoja wa nchi za Kiarabu-Arab League, Jumuiya ya nchi za Kiislamu-OIC, na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuchukua hatua za haraka ili kukomesha vitendo vinavyofanywa na Israel. Aidha, Umoja wa Falme za Kiarabu-UAE, nao umelaani shambulio hilo na umetaka uchunguzi wa kimataifa ufanyike kuhusiana na shambulio hilo.
Waziri Mkuu wa Israeli, Benjamin Netanyahu ameunga mkono kitendo kilichofanywa na vikosi vya jeshi lake baada ya kuishambulia meli ya Flotilla na kusababisha vifo hivyo. Bwana Netanyahu ambaye yuko Ottawa, leo amekutana na Waziri Mkuu wa Canada, Stephen Harper kabla ya kuelekea Marekani hapo kesho kwa ajili ya mkutano wake na Rais Barack Obama.
Marekani kwa upande wake imelizungumzia shambulio hilo, ambapo taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Ikulu ya Marekani, Bill Burton imeeleza kuwa nchi hiyo imesikitishwa na vifo hivyo pamoja na watu waliojeruhiwa. Marekani, miongoni mwa nchi nyingine, imekuwa ikijaribu kuanzisha tena mazungumzo ya amani ya moja kwa moja kati ya Waisrael na Wapalestina, lakini jitihada hizo zimekuwa zikigonga mwamba katika miezi ya hivi karibuni. Nchi nyingine zilizolaani shambulio hilo ni pamoja na Ufaransa, Urusi, Ugiriki na Kuwait. Naye mjumbe wa amani ya Mashariki ya Kati, Tony Blair ameelezea masikitiko yake kuhusiana na shambulio hilo. Bwana Blair amesema ameshitushwa na kitendo hicho kilichofanywa na Israel. Nao Umoja wa Afrika umesema umeshtushwa na shambulio hilo dhidi ya meli ya wanaharakati. Umoja huo umetaka uchunguzi juu ya suala hilo ufanyike.
0 comments