IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
BAADA ya kimya kirefu na tetesi na utabiri wa hapa na pale, hatimaye kumepambazuka Zanzibar, safari ya kuwania urais wa visiwa hivyo imeanza kwa Makamu wa Rais, Dk Ali Mohamed Shein, kutangazwa kujitokeza.
Kwa mujibu wa Katibu wa Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Vuai Ali Vuai, Makamu wa Rais, anatarajiwa kuchukua fomu keshokutwa kuomba ridhaa ya chama kuteuliwa kuwa mgombea urais za Zanzibar kwa tiketi ya CCM.
Vuai aliwambia waandishi wa habari mjini hapa Zanzibar kwamba, Shein atachukua fomu hizo katika ofisi ndogo ya makao makuu ya CCM Kisiwandui saa 9 alasiri siku hiyo.
Si peke yake kwa kuwa yalitajwa pia majina ya baadhi ya wanasiasa waandamizi ambao ni wanachama wa chama hicho ambao nao wamekuwa wakitajwatajwa kuwania nafasi hiyo visiwani humo.
Wana CCM hao ni pamoja na Waziri Kiongozi, Shamsi Vuai Nahodha, Naibu Waziri Kiongozi, Ali Juma Shamuhuna, Waziri Kiongozi mstaafu Dk. Mohamed Gharib Bilali, Balozi wa Tanzania nchini Italia, Ali Karume, na Hamad Bakar Mshindo.
Wote hao kwa mujibu wa Vuai, kila mmoja atatakiwa kulipia Sh milioni moja ili kupata fomu hizo kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa na chama hicho tawala.
Alisema, kila mmoja wao amepangiwa muda maalumu wa kwenda kuchukua fomu ili kuepuka usumbufu huku mikutano na waandidhi wa habari na wapambe wao wakiwamo wafuasi wakizuiwa wakati wa uchukuaji wa fomu hizo.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Idara ya Habari - Maelezo Zanzibar, Dk Bilali na Nahodha, watakuwa na mikutano tofauti na waandishi wa habari katika hoteli mbili tofauti mjini Zanzibar. Wakati Bilali atafanya wa kwake leo, Nahodha atakuwa nao keshokutwa.
Wanasiasa wengine ambao wanatajwa nao kutaka kuwania urais wa Zanzibar ni pamoja na Mohamed Aboud Mohamed, Muhamed Seif Khatib, Dk Omar Dadi Sharjak, Amina Salum Ali na Haroun Ali Suleiman.
Wakati huo huo, mjumbe wa Baraza wa Wakilishi, Ramadhani Nyonje Pandu (Mayuni – CCM) amebashiri kuwapo uwezekano mkubwa kwamba Rais ajaye wa Zanzibar atatoka ndani ya Baraza hilo.
Pandu alisema hayo jana wakati akichangia makadirio ya Matumizi ya Ofisi ya Waziri Kiongozi kwa mwaka 2010/11.
Alifafanua kuwa historia inaonesha, kuwa idadi kubwa ya wanaoshinda urais Bara na Visiwani wamewahi kuwa wabunge au wawakilishi na kutoa mfano wa Rais mtaafu Dk. Salmin Amour na Rais wa sasa Dk. Amani Abeid Karume ambao walikuwa wajumbe wa Baraza.
Pia Rais mstaafu Benjamin Mkapa na Rais Jakaya Kikwete ambao pia wamewahi kuwa wabunge katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika ubashiri wake, Pandu alisema katika majina ya wajumbe watatu wa Baraza mmoja wao ataibuka mshindi wa urais wa Zanzibar katika uchaguzi mkuu ujao.
Aliwataja wajumbe hao kuwa ni Nahodha, Shamuhuna na Haroun na kusisitiza kuwa nafasi ya urais wa Zanzibar haitachukuliwa na mtu kutoka nje ya Baraza.
Rais atakayechaguliwa Zanzibar Oktoba mwaka huu, atakuwa ni wa saba wa visiwa hivyo, akiwa ametanguliwa na marahemu Abeid Amani Karume, Aboud Jumbe Mwinyi, Idris Abdulwakil, Ali Hassan Mwinyi, Dk Salmin Amour na Amani Abeid Karume.
You Are Here: Home - - Shein kugombea urais Zanzibar
0 comments