Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Ndondi katika Kanisa na siasa

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
Awapasha viongozi wanaolinda mafisadi

Asema wananufaika na uozo wao


 "Ukimwambia Rais wa nchi kuwa hili ni kosa lako anakataa na kusema hapana mimi ni msomi tu, ni hawa walio chini yangu ndiyo waliyo wabaya. Hiyo si kweli, ni kutowajibika tu,"
KATIKA hatua inayoweza kutafsiriwa kuwa uongozi wa juu wa Kanisa Katoliki nchini umechoshwa na ubabaishaji wa viongozi waandamizi serikalini, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amesema uongozi wa juu hauwezi kukwepa kuhusika na uozo wa watendaji wake kwa kuwa wana uwezo wa kuwang’oa vinginevyo hiyo ni ishara kuwa viongozi hao wananufaika na makosa ya watendaji na wasaidizi wao na pia ni sehemu ya udhaifu huo.
Kauli hiyo kali ya Kardinali Pengo, ambayo si tu imeelekezwa kwa wanasiasa waandamizi nchini na duniani kwa ujumla bali hata kwa mapadre wa kanisa hilo, inaweza kutafsiriwa kama hatua ya kupinga kauli nyingine ya hivi karibuni ya Askofu wa kanisa hilo, Dk. Methodius Kilaini ambaye alinukuliwa akisema Rais Jakaya Kikwete bado ni chaguo la Mungu, isipokuwa wanaomwangusha ni watendaji wake wasaidizi na akichaguliwa tena asiwateue watendaji hao.
Miaka minne iliyopita Askofu Kilaini alimuelezea Rais Kikwete kuwa ni "chaguo la Mungu" na hivi karibuni akarudia kusema kwamba hajabadili msimamo wake, japo akaongeza kusema kwamba wasaidizi  na mawaziri wake wanamuangusha na hana budi kuachana nao iwapo atachaguliwa tena kuongoza nchi.
Kauli ya Kardinali Pengo aliitoa wakati wa akitoa Homilia katika Ibada ya Misa Takatifu ya Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA) wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam hivi karibuni, na ikapigiwa chapuo na Padre wa Kanisa hilo, Baptista Mapunda, alipokuwa akihubiri katika Kanisa Katoliki la Manzese kwenye maadhimisho ya Sikukuu ya Ekarist Takatifu.
Kwa mujibu wa gazeti rasmi la Kanisa Katoliki linaloitwa Tumaini Letu la Juni 4 hadi 10, mwaka huu, Kardinali Pengo anasema hatua ya viongozi wa ngazi za juu serikalini hapa nchini na duniani kwa ujumla ya kutowachukulia hatua viongozi wa chini yao wanaonekana kufanya vibaya katika utendaji wao wa kazi, ni kutaka kupata sehemu ya kutupia lawama.
Kardinali Pengo anakaririwa kueleza kuwa kutowachukulia hatua viongozi hao wanaofanya makosa mbalimbali serikalini kunalenga kulinda malsahi ya viongozi hao wa juu ili waendelee kuwapo na kujineemesha huku wakijua fika kwamba wanafanya makosa.
“Serikali za watu zimejaa mahangaiko na kero nyingi za kila aina. Watu masikini wanataabika, watu wanalia, wagonjwa wanakufa kwa ukosefu wa dawa na hawawezi wakapata hata msaada unaotakiwa halafu wewe unajilipa shilingi milioni tano.
“Huwezi kusema mama anayelia kwa maumivu ya kansa anakufa na hana hata dawa ya kutuliza maumivu kwamba hilo ni kosa la uchumi mbovu wakati viongozi wanajilipa mishahara mikubwa,” alisema Kardinali Pengo na kufafanua kuwa kama viongozi hao wanadai kuwa hali ya uchumi ni mbaya, ni vema mahangaiko na mateso wanayopata wananchi na wagonjwa mbalimbali, viongozi hao wataabike pamoja nao ili kuthibitisha ukweli wa hali mbaya ya uchumi.
“Ukimwambia Rais wa nchi kuwa hili ni kosa lako anakataa na kusema hapana mimi ni msomi tu, ni hawa walio chini yangu ndiyo waliyo wabaya. Hiyo si kweli, ni kutowajibika tu,” alisema.
Katika kuwaasa viongozi wenzake ndani ya Kanisa hilo, Kardinali huyo mwenye hulka ya kuzungumza kwa kuchuja maneno yake alitoa wito kwa mapadre wa kanisa hilo kuwa mfano wa kuigwa na kutambua majukumu yao ikiwa ni pamoja na jukumu lao.
“Sisi viongozi wa Kanisa hatujajifunza kusema samahani ni kosa langu. Tunapokataa kumwambia Mwenyezi samahani ndipo hapo mambo yanapokuwa mabaya zaidi. Sisi tusipojua kusema samahani tutawakokota wote kwenda Jehanamu nasi….tuombeeni sisi mapadre kuwa wa kwanza kukaa kwenye kiti cha kitubio na kupokea samahani zenu, kwani bila kuwa na moyo huo tutaangamia wote,” alisema.
Kwa upande wake, Padre Mapunda katika kuonyesha kuunga mkono kauli za Pengo akiwa katika Kanisa Katoliki Manzese, Dar es Salaam, hivi karibuni, naye alisema kuwa matukio ya baadhi ya wananchi kujichukulia sheria mkononi ni ishara ya kuchoshwa na hali ya kukithiri kwa ubinafsi nchini akiweka bayana kuwa hali pia si shwari kwa viongozi wa dini.
 Kwa tafsiri inayojitokeza kutokana na kauli yake hiyo; ni kwamba viongozi wa dini wameunda genge moja na baadhi ya viongozi wa kisiasa katika kupuuza maslahi ya wananchi.
“Kuna baadhi ya viongozi wa dini ambao wanakubali kupokea vijisenti vya wanasiasa kwa ajili ya kupindisha ukweli na kuongeza ushawishi kwa waumini ili wawachague katika nyadhifa zao. Hiyo ni dhamira kubwa ya kuliangamiza Taifa. Viongozi lazima wakubali kuacha ubinafsi…hiyo ndiyo dhambi inayoteketeza Taifa. Wanawaacha wananchi waliowapa madaraka katika dimbwi la taabu na umasikini.
“Inasikitisha kumwoma Mcha Mungu akiuza utu wake kwa mtu binafsi eti kwa ajili ya kupata uongozi, ni muhimu kutambua kuwa viongozi wa mtindo huo hawatakiwi kabisa na ni lazima tuachane nao.
“Sishabikii siasa bali ni wajibu wangu kuwaelimisha wananchi kuchagua kiongozi anayefanana na maadili ya Mungu ili kuweza kufikia malengo ya kiimani na maendeleo ya nchi kwa ujumla,” alisema padri huyo.
Katika maelezo yake ya hivi karibuni, Askofu Kilaini, ambaye amehamishiwa mkoani Kagera kutoka Jimbo Kuu la Dar es Salaam, alinukuliwa akisema;
“Mwaka 2005 niliwahi kusema kuwa Kikwete ni chaguo la Mungu... kwa maana kwamba kiongozi yeyote anayechaguliwa na watu anakuwa amesimamishwa na Mungu. Miaka minne baadaye ameendelea kupendwa kwa kiasi kilekile na wananchi kwa kuwa kweli ni chaguo hasa ambalo Watanzania walilihitaji.”
Akinukuliwa na gazeti moja nchini, Askofu Kilaini alisema: “Yapo mambo ambayo hayakwenda vizuri katika kipindi hiki, lakini ukiangalia yeye kama rais hawezi kujua kila kitu... anahitaji kusaidiwa na watendaji wake wa karibu na hawa wamekuwa wakimwangusha mara kwa mara."
Tags:

0 comments

Post a Comment