IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
HADI saa 8.00 mchana jana, kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) kilichokuwa kifanyike kuanzia saa 4 asubuhi katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo,Iringa, kilikuwa hakijaanza.
Baadhi ya wajumbe wamethibitisia kuwa kuna mgogoro mkubwa wa uongozi.
Kikao kilichokuwa kikiendelea wakati huo, kilikuwa cha Kamati ya Utekelezaji ya Umoja huo, kilichokuwa kikifanyika ndani ya ofisi ya CCM ya mkoa.
Juzi usiku, wajumbe wengi wa Baraza hilo walikutana mjini hapa kula, kunywa na kucheza muziki katika hafla ambayo taarifa zake zilidai kwamba ingehudhuriwa na Mwenyekiti wa UVCCM, Hamad Yusuph Masauni, ambaye hata hivyo, alifika saa saba usiku akifuatana na baadhi ya wapambe wake, baada ya wajumbe karibu wote kuwa wameondoka.
Taarifa ambazo hata hivyo hazikuthibitishwa na wahusika, zilidai kwamba baadhi ya wajumbe walisema hawako tayari kuingia katika kikao hicho kama ajenda ya kuwajadili na hata kuwang’oa Masauni na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja huo Zanzibar, Nassoro Moyo, haitakuwapo.
Hata hivyo wajumbe wengine walisema uwezekano Moyo kung’olewa uongozi ni mdogo kutokana na tuhuma zilizokuwa zikielezwa na baadhi ya wajumbe kwamba amefuja fedha za umoja huo, kuthibitika kwamba hazina ukweli wowote.
“Nakuhakikishia kweli tupu, kwamba kuna ajenda inapikwa ya kutaka kuwang’oa viongozi hawa, sasa amini maneno yangu, Moyo hang’oki, ila Masauni hali yake ni tete, labda ajenda hiyo isiingie katika kikao cha Baraza,” alisema mmoja wao.
Wengi wa wajumbe wa umoja huo, kutoka Bara walisema mvutano wa uongozi ndani ya umoja huo, unasababishwa na chuki za kisiasa za wajumbe wa Zanzibar dhidi ya viongozi hao.
“Hakuna kiongozi tutakayemwondoa kati ya hao wawili, sisi wa Bara tunaona wako safi na wanachapa mzigo kwa mujibu wa Katiba,” alisema mwingine.
Hata hivyo wakati mitazamo dhidi ya viongozi hao ikiwa katika hali hiyo, Masauni anatuhumiwa kutotaja umri wake sahihi wakati akiwania uenyekiti wa umoja huo Desemba mwaka juzi.
Tuhuma hizo zinadai kuna cheti kinaonesha alizaliwa Oktoba 3, 1973 na fomu za kuomba hati mpya ya kusafiria zinaonesha alizaliwa Oktoba 3, 1979.
Vita ya makundi ndani ya umoja huo yanayoongozwa na wanaopinga na kufumbia macho rushwa ndani ya chama hicho, ni sababu nyingine inayohatarisha amani ya uongozi ndani ya UVCCM.
Wakiwa nje ya ofisi hizo za CCM za mkoa, baadhi ya wajumbe walisema kama kikao cha Baraza kitafanyika, kitaweza kumalizika saa sita usiku kwa sababu lazima yote yaliyokifanya kichelewe, yajadiliwe kwa kina.
“Na tutataka tunapoingia katika kikao hicho ajenda zote lazima tuzifahamu kabla hakijaanza,” alisema mmoja wao.
Katibu Mkuu wa CCM, Yusuph Makamba, aliyewasili mjini hapa juzi, na kukutana na baadhi ya viongozi wa UVCCM katika majadiliano ambayo yameendelea kuwa siri, jana alitarajiwa kufungua kikao cha Baraza.
Wakati ikiwa haieleweki nini yatakuwa matokeo ya kikao cha baraza hilo, baadhi ya wanachama wanawake wanaowania nafasi 10 za ubunge kupitia umoja huo, wako mjini hapa, wakijaribu kufahamiana na wajumbe wa Baraza hilo na hata kutangaza nia zao za kutaka nafasi hizo ili wachaguliwe kuingia katika Bunge lijalo.
Naye Flora Mwakasala, anaripoti kwamba Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM wa Wilaya ya Kinondoni, Emmanuel Makene, amesema baadhi ya wanasiasa waliozusha maneno Masauni ameghushi umri na kumtaka ajiuzulu wana lengo la kuvuruga umoja huo.
Alisema umri si kigezo wala pingamizi katika utendaji kazi na kuwa Masauni alipitishwa na vikao halali na kuchaguliwa kuwa kiongozi kwa kuwa anafaa na hakuna kundi linalompinga.
Alisema lengo lake si kusema mwaka aliozaliwa Masauni, bali ni kuwaambia vijana kutobabaika na maneno ya baadhi ya wajumbe na viongozi wasio waaminifu wenye nia ya kuiharibu jumuiya yao na kuwaomba kuendelea kuwa na imani na Masauni.
Masauni alichaguliwa kushika wadhifa huo Desemba mwaka juzi na anatarajiwa kumaliza muda wake kikatiba mwaka 2012.
You Are Here: Home - - Wingu zito Baraza la UVCCM
0 comments