Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Makamba atumia umafia kumng’oa Masauni

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter WAKATI kikao tete cha Baraza Kuu la Umoja wa Vijana (UVCCM) kikimalizika mjini Iringa, taarifa zaidi zimezidi kumtaja Katibu Mkuu wa CCM Yusuph Makamba, kwamba alimtisha kigogo huyo wa vijana akimwambia alipaswa kujiuzulu kwa agizo la vyombo vya dola.

Shinikizo hilo la kutumia lungu zito la Idara za serikali, linadaiwa kutolewa na Makamba baada ya kumwona Masauni anakuwa mzito kutekeleza uamuzi huo wa kujiuzulu.

Duru za kisiasa kutoka ndani na nje ya kikao hicho, zilifafanua kwamba Masauni alikuwa ameshikilia msimamo wa kutong’oka jambo lililofanya mkutano wa Baraza Kuu kuchelewa kufanyika juzi asubuhi 4:00 na badala yake ukaanza saa 2:30 usiku.

Lakini, Makamba mwenyewe alipoulizwa aling'aka na kuhoji:," Wewe bwana sikiliza, ninayo barua ya Masauni hapa, ...anasema amejiuzulu mwenyewe bila kushinikizwa."

"Sasa unaposema nimemshinikiza, una maana gani? Nimemshinikiza ili iweje... nimuweke mke wangu awe mwenyekiti?"

Makamba alizidi kufafanua kwamba, "Sioni sababu ya kumng'oa au kumshinikiza Masauni ajiuzulu. What do I get? Kwani jumuiya ni ya baba angu hii...eeee?"

Huku akichanganya lugha yake ya kabila la Kisambaa, Kiswahili na Kingereza kwa mbali, Makamba aliongeza: "Masauni kasema amejiuzulu mwenyewe kwa heshima yake, familia yake na chama, CCM siyo chama cha baba yangu wala mama yangu, wewe vipi?"

Ingawa Makamba alikanusha taarifa na kusoma barua hiyo ya Masauni,, vyanzo vya habari za kisiasa ziliweka bayana kwamba, baada ya juhudi za muda mrefu za kumshawishi kigogo huyo wa zamani wa UVCCM, kugonga mwamba, mtendaji huyo mkuu wa CCM alimwambia:, “Atajiaibisha kwa sababu idara moja ya serikali inamtaka lazima ang’oke.”

“Alitishiwa kwamba, msimamo wake ni bure kwa sababu idara hiyo imebariki atoke yeye mwenyewe au aondoshwe na kujiharibia heshima yake,” kilidokeza chanzo hicho habari na kuongeza.

“Vitisho alivyovipata Masauni ndivyo vilivyomfanya atoe uamuzi wa ghafla bila kuliarifu kundi lililokuwa nyuma yake licha ya kutoa msimamo kwamba, litamtetea kwa sababu lina hoja za kufanya hivyo.”

Moja ya hoja zilielezwa kwamba, waliokuwa wakimpinga walishinikizwa na mmoja wa vigogo ndani ya chama ambaye anataka aweke safu yake ya uongozi, itakayotengeneza njia laini ili awe rais wa awamu ya tano kuanzia mwaka 2015.

Hoja nyingine ni kwamba, kashfa inayomkabili Masauni ni ndogo ukilinganisha na nyingine kubwa za kifisadi walizonazo viongozi ndani ya CCM na wanaendelea kuwakumbatia na kuwalinda wasiguswe.

Maamuzi ya ghafla ya Masauni kujiuzulu kwenye nafasi hiyo yaliwafanya wajumbe wengi kutoka Zanzibar, waliokuwa mstari wa mbele kumtetea, kuangua kilio wakisema amewasaliti.

Chanzo kingine zaidi kilichokuwa ndani ya mkutano huo kilieleza kwamba, ilikuwa ni kama masihara kwa sababu baada ya wajumbe kugawiwa makabrasha ya ajenda za mkutano, viongozi walitambulishwa na Masauni alipopewa fursa ya kuzungumza kuwakaribisha wajumbe, alichomoa mfukoni barua ya kujiuzulu na kumkabidhi Makamba.

Kabla ya kumkabidhi alitoa maelezo machache akisema uamuzi huo ameufanya yeye binafsi bila kulazimishwa, kwa:, " “heshima ya chama chake, umoja wa vijana, yeye binafsi na familia yake.”

Maelezo hayo ya ghafla yalililichanganya kundi lililokuwa nyuma yake, ambalo lilitarajia hoja ingeibuliwa, waanze kuijadili na hapo ndipo wangewasha moto wa kumtetea.

Wajumbe hao walisema walikuwa wamejiandaa kikamilifu kuhakikisha wanamtetea dhidi ya tuhuma zinazomkabili za kughushi umri wakati anachaguliwa kwenye nafasi hiyo mwaka 2008, na walionyesha msimamo huo mapema wakati mkutano wa baraza unaanza.

Katika hali ya kuonyesha walivyokuwa wamejiandaa, wakati viongozi wanaingia kuanza mkutano, walianzisha wimbo wakionyesha msimamo wao kwamba Masauni ni mtu safi na watamlinda kwa namna yoyote.

“Masauni ni kiongozi bora, safi… Masauni tutamlinda na kumtetea,” walisikia wakiimba kwa hisia, nguvu na umoja huku makofi yakiongeza hamasa kwa ajili ya kukaribisha viongozi kuanza mkutano.

Mbali na Makamba, kiongozi mwingine asiye wa ngazi ya vijana aliyehudhuria mkutabno huo wa Baraza ni Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mohamed Abdul-Azizi.

Hali iligeuka, hamasa pamoja na mhemko wa kumtetea ukawa ni kilio baada ya Masauni kutangaza kiwepesi kwamba, anajuzulu kwa hiari.

Wajumbe wengi walianza kutaharuki na wengine kuamua kutoka nje ya ukumbi wakilia, wengi wao wakiwa ni wale kutoka Zanzibar.

“Kama mambo ya chama ndiyo haya bora tujitoe. Hiki ni chama cha majungu, bora tujitoe,” alilalamika mmoja wa wajumbe wa Zanzibar huku akilia na kufunika uso na ushungi aliokuwa amebeba mkononi.

Kundi la hilo la wajumbe wapatao 20, waliotoka nje wakiangua kilio, baadhi yao waliondoka na kuachana na mkutano huo, huku wakirusha lawama nyingi kwa uongozi wa chama.

Mmoja wao aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina aliweka wazi kwamba, amewasiliana na wenzao Zanzibar ambao walikuwa wanafuatilia kikao hicho kwa makini na kuonya uwezekano wa kurejesha kadi za CCM.

Hata hivyo, baada ya mkutano wa baraza kumalizika saa 7:25 usiku, Makamba alitoka kwenye ukumbi akionekana mwenye furaha na bashasha akisema bado UVCCM ni imara na inaendelea kuwa imara.

“Tumeingia tukiwa imara na tumetoka tukiwa imara… jumuiya ni imara na tumetoka na msimamo kwamba ni lazima tushinde kwa kishindo katika uchaguzi mkuu ujao,” alisema Makamba huku akionyesha uso wenye tabasamu la hali ya juu.

Kwa upande wa Masauni alipotakiwa kueleza sababu za kujiuzulu kwake alikataa kuzitaja na hata alipokumbushwa kwamba vyombo vya habari vinadai alighushi, alisema:, “hilo umesema wewe. Ni la kwako. Mimi sijasema.”

Mkutano huo wa baraza ulifanyika wakati ambapo Naibu Katibu Mkuu Mohamed Nassor Moyo, akiwa tayari amejiengua kwenye nafasi hiyo na mkakati huo kuridhiwa na Kamati ya Utekelezaji.

Katibu Mkuu wa UVCCM, Martine Shigela leo mchana anakutana na waandishi wa habari kuelezea kwa kina sakata hilo
Tags:

0 comments

Post a Comment