IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
WANASIASA wameendelea kupinga kipengele cha elimu katika Sheria ya Kanuni za Gharama za Uchaguzi, wasomi na wananchi wanaunga mkono kwa madai kuwa kitaleta mabadiliko katika masuala ya uamuzi na uchangiaji maendeleo ya nchi.
Kipengele hicho kilicho katika sheria hiyo, kinamtaka mgombea urais, udiwani na ubunge, kuweka bayana kiwango chake cha elimu.
Katiba inaeleza kuwa mgombea wa nafasi hiyo, sifa yake kielimu ni kujua kusoma na kuandika.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, baadhi ya wenyeviti wa vyama vya siasa nchini, wameonesha wasiwasi wao juu ya kipengele hicho, huku wakidai kuwa elimu si kigezo cha kupata kiongozi bora.
Mwenyekiti wa Chama wa Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, alisema katika uongozi, kinachohitajika ni kiongozi imara, mwadilifu na mwenye sifa ya uongozi na awe anajua kusoma na kuandika.
“Hii ndiyo demokrasia, lazima watu wakupime kwa uwezo wako, utendaji wako na uwajibikaji na si kielimu pekee, suala la kutaka viongozi wenye vyeti pekee ni kinyume na demokrasia yetu ingawa kweli elimu inasaidia,” alisema Profesa Lipumba.
Hata hivyo, alisema si lazima kiongozi awe na elimu kubwa ndipo aongoze kwa uaminifu, kwani wapo wenye uwezo mkubwa na sifa za uongozi bora, lakini kiwango chao cha elimu ni kidogo.
Mwenyekiti wa Chama cha Labour (TLP), Augustine Mrema, alikiri kuwa elimu inasaidia sana katika maisha ambapo mtu mwenye elimu, hata kiwango chake cha umakini ni kikubwa, lakini akaongeza kuwa muhimu wa elimu hiyo, si katika kila kitu hususani kwenye uongozi.
Alisema yeye Mrema haamini kama elimu ni suluhisho la matatizo ya uongozi nchini. “Mbona ukifuatilia wanaokula rushwa ni hao hao wasomi viongozi, wapo viongozi wasio na elimu kubwa kama akina Tony Blair (Waziri Mkuu wa zamani Uingereza), lakini waliongoza vizuri,” alisema.
Alisema cha msingi apatikane kiongozi mwenye maadili mazuri, asiyejali maslahi binafsi na mwenye kuleta mabadiliko katika jamii inayomzunguka bila kujali kiwango chake cha elimu.
Hata hivyo, aliyekuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Mwesiga Baregu, aliunga mkono kipengele hicho na kuongeza kuwa kitaifanya Tanzania kuwa na viongozi makini wenye uwezo wa kuchambua mbivu na mbichi, hasa katika masuala ya maendeleo ya wananchi wao.
“Fikiria kuwa sheria zote hutungwa kwa Kiingereza, sasa mbunge huyu anajua kusoma na kuandika tu, ataipitishaje sheria ambayo hailewi, katika hili ni lazima uwe na elimu ili kutenda yale unayotarajiwa kutenda,” alisema.
Hata hivyo, alisema kwa kuwa kuna tatizo la mfumo wa elimu na hasa kuibuka tatizo la vyeti feki, iko haja ya kuwekwa utaratibu wa kuwapima uwezo wao kielimu, wale wanaotaka kugombea ili kukwepa kuwa na viongozi wengi mbumbumbu.
“Wengi wapo bungeni tunaowana, kazi yao kulala hata wanashindwa kuwawakilisha wananchi wao hata kuchangia kidogo, kwa kweli hili linapaswa kutazamwa,” alisema.
Ayub Rioba, Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika, tawi la Tanzania (MISA-TAN), alisema kutokana na Dunia ya leo inavyokwenda na mambo yake kuwa magumu, elimu ni muhimu kuzingatiwa.
Alisema kiongozi mwenye elimu ni vigumu kupitisha sheria na miswada ambayo inaiweka pabaya nchi au kumwangamiza mwananchi. “Lakini kipengele hiki kingekuwa kizuri zaidi kama kingewekwa na vyama vyenyewe lakini kaka nchi ni kukiuka Katiba,” alisema.
Alisema kwa mujibu wa Katiba, kila mwananchi ana haki ya kugombea uongozi ili mradi awe anajua kusoma na kuandika, hivyo ni makosa kwa sheria ya nchi, kumzuia mwananchi huyo kugombea uongozi.
Nao wananchi waliohojiwa na gazeti hili, waliunga mkono kipengele hicho, huku Mfanyabiashara Issa Mohammed, akisema kipengele hicho sasa kitaondoa tatizo kubwa la ubovu wa mikataba, ambayo imekuwa ikiikandamiza nchi na wananchi kwa ujumla.
You Are Here: Home - - Sifa ya wagombea yawagawa wanasiasa
0 comments