Moto huo uliowashwa na PAC katika kipindi ambacho, Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini ikiwa imejipanga kukabiliana na serikali kuhusu utekelezaji wa maazimio ya Bunge ya LLC hapo Januari 20, mwaka huu.
Jana ilikuwa ni siku ya PAC kukutana na watendaji wa ngazi ya juu wa Wizara ya Nishati na Madini, ambao waliongozwa na Katibu Mkuu David Jairo, ambaye ni mara yake ya kwanza tangu kuteuliwa kushika wadhifa.
Hata hivyo, Jairo na watendaji wake walionyesha kujiandaa kikamilifu kutokana na kujibu maswali yote aliyoulizwa.
Swali gumu lilikuwa la Richmond, ambapo aliulizwa juu ya utekelezaji wa agizo la PAC kwa wizara. Mbunge wa Pangani, Mohamed Rished, alihoji kama Richmond ilikwisha wahi kulipwa hata senti na kama pia serikali haikupata hasara katika mkataba huo uliosaniwa Juni 23, 2006.
Baada ya swali hilo, Jairo ambaye alifuatana na watendaji wake wakiwemo kutoka Tanesco na Shirika la Maendeleo la Petroli, alirudisha suala hilo kwa Kamishna wa Nishati Bashir Mrindoko, ambaye alijibu akisema: "Kuhusu Richmond sijui kama nitatoa majibu ya kuridhisha".
Mrindoko ambaye hadi sasa anatakiwa kuwajibishwa na mamlaka ya juu (Rais) kuhusiana na mkataba huo wa Richmond; alifahamisha kuwa baada ya Richmond kushindwa mitambo hiyo ilichukuliwa na Dowans ambayo ililipwa fedha baada ya kuzalisha umeme na kuingiza kwenye gridi ya taifa kama ilivyo katika mkataba.
Hata hivyo, jibu hilo halikuweza kumfurahisha Mwenyekiti wa PAC, John Cheyo ambaye alimwambia: " Hebu subiri, kuna pre (kabla) na post (baada) Dowans. Swali ni je, Richmond haikuwahi kulipwa hata senti?"
Swali hilo lilionekana kuzidi nguvu Mrindoko ambaye alirusha kwa Meneja Mkuu wa Malipo wa Tanesco, Anita Chengula, ambaye aliweka bayana kwamba serikali haikuwahi kuilipa Richmond hata senti.
Baada ya kauli hiyo, Cheyo aliitaka serikali kupitia wizara kutoa taarifa rasmi kwa umma ili kueleza bayana kwamba, Richmond haijawahi kulipwa hata senti, ili kuondoa wingu ambalo limekuwa likitanda kila kukicha.
"Tumeingia mwaka huu na Richmond, tunaelekea kwenye uchaguzi bado na Richmond sasa kumbe hawajawahi kulipwa kwanini serikali isiseme siku zote hizo?" alihoji Cheyo.
Kuhusu kesi ya IPTL, serikali ilisema tayari imempata mfilisi na kwamba, mchakato wa kununua mitambo hiyo utaanza mara baada ya kukamilika taratibu zote za msingi.
Hata hivyo, mpango huo uliibua maswali kutoka kwa wajumbe, ambapo Rished alihoji kama serikali inaweza kununua mitambo iliyokwishatumika wakati Sheria ya Manunuzi ya Umma ya Mamlaka ya Zabuni (PPRA), inakataza hatua hiyo.
Hata hivyo, Katibu Mkuu Jairo aliweka bayana kwamba, ununuzi wa mitambo hiyo unatokana na agizo la Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini ambayo ilitaka serikali inunue mitambo hiyo.
Mwenyekiti Cheyo, aliweka bayana kwamba, kamati yake haikuwa ikipingana na ile ya Nishati, lakini akasisitiza umuhimu wa mchakato huo kufanyika kwa haraka ili uweze kukamilika.
Ununuzi wa mitambo ya IPTL uliibua mvutano wa hoja kati ya Kamati ya Bunge ya Nishati na ile ya Hesabu za Mashirika ya Umma, ambayo chini ya mbunge wa Kigoma Kaskazini ilikuwa ikitaka inunuliwe mitambo ya Dowans kwani gharama zake ni ndogo.
Kwa mujibu wa nyaraka za serikali za mwaka juzi, hadi Mei IPTL ilikwishalipwa Sh 200 bilioni, huku gharama za kuibadili kwenda katika gesi ikifikia Sh 75 bilioni wakati iliwekeza mtaji wa Sh 50,000 tu. Gharama za kuinunua Dowans ni Sh 60 hadi 90 bilioni.
0 comments