Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - CCM wataka rais asiwe mwenyekiti wao

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter




WABUNGE wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamesema wakati umefika wa kumpunguzia rais majukumu ya kichama ili awajibike zaidi katika kazi za serikali na kukifanya chama kuwa na nguvu ya kuhoji utendaji wake.

Wakati mjadala dhidi ya utendaji kazi wa Rais Jakaya Kikwete ukielekea kupoa, Wana-CCM hao wameibuka upya na kujenga hoja kuwa kumuachia rais madaraka ya serikali na chama ni chanzo cha kukwama kwa utekelezaji wa malengo mbalimbali ya kitaifa na kinaondoa nguvu ya kumbana anaposhindwa kuwajibika ipasavyo.

Mwishoni mwa mwaka jana, mawaziri wawili wa zamani walionyesha kuwa na wasiwasi na utendaji wa Rais Kikwete wakisema anashindwa kufanya maamuzi magumu dhidi ya watuhumiwa wa ufisadi na kwamba chama kimepoteza hadhi yake kutokana na kutekwa na matajiri.

Mjadala huo ulipoa baada ya Rais Kikwete kuahidi kukaa na wenzake kuandaa majibu, hata hivyo suala hilo linaonekana kuibuka kwa sura nyingine.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Mwananchi katika ofisi ndogo za Bunge jiijini Dar es Salaam wakati wa kujadili ripoti hiyo ya Mfumo wa Kupima Utawala Bora wa Umoja wa Afrika (APRM), baadhi ya wabunge na wanaharakati wameshauri kutenganishwa kwa mamlaka ya chama na serikali kwa rais kwa maslahi ya taifa.

Wametaka pia vyama vya siasa kuangalia na kurekebisha katiba zao ili kuondoa utata huo ambao walidai unakwamisha uwajibikaji.

"Ni kitu kibaya kwa rais kuwa mwenyekiti wa chama," alisema mbunge wa Kishapu (CCM), Fred Mpendazoe alipozungumza na Mwananchi.

"Upo umuhimu wa kutenganisha nafasi hizo. Tatizo tumerithi katiba nusu nusu. Tumerithi nusu kutoka Marekani tunayotumia kuchagua rais na nusu ya Jumuia ya Madola tunayotumia kupata mawaziri na watendaji wengine, lakini sasa tunatakiwa kurekebisha katiba ya nchi na ya chama (CCM)."

Alifafanua kuwa tatizo la kofia mbili linaonekana katika utekelezaji wa maamuzi na kwamba mengi hukwama kutokana na hali hiyo na akaongeza kusema:"Ni vyema rais asiwe mwenyekiti wa chama ili kutoa nafasi ya uwajibikaji zaidi na chama kuwa na nguvu ya kuhoji utendaji wake."

"Hii ndiyo hali yetu ya sasa... rais ndiye mwenyekiti wa chama, kwa hali hiyo yeye ndiye anaongoza vikao vya kamati kuu ya chama pia ndiye mwenyekiti wa baraza la mawaziri. Nani atahoji utendaji wa serikali ikiwa rais ni mwenyekiti wa chama, baraza la mawaziri na hata vikao vya Nec."

Kwa mujibu wa Mpendazoe mfumo huo ni wa kulindana na unasababisha kuchelewa kutolewa kwa taarifa za utekelezaji zinazojadiliwa ndani ya chama na serikali.

Alisema tatizo hilo pia lipo kwa mawaziri ambao nao hutumia nafasi zao za uwaziri na kujipatia nafasi za ujumbe wa Halmashauri Kuu na Kamati Kuu, hivyo kuweka ugumu katika kufuatilia utendaji wao hasa serikalini kwa kuwa huweza kujijengea wigo wa kujilinda ndani ya chama.

Mbunge wa Kahama (CCM), James Lembeli alisema ili kudhibiti mfumo wa kulindana ambao alidai umeota mizizi, mawaziri wanaoteuliwa na rais wathibitishwe na Bunge.

"Hii itasaidia kuongeza ufanisi na uwajibikaji utakaokuwa na tija kwa maendeleo ya taifa," alisema.

Lembeli, ambaye ni mmoja wa wabunge wanaojipambanua kuwa wapambanaji wa vita ya ufisadi, alikwenda mbali zaidi na kuhoji: "Pamoja na baraza la sasa la mawaziri kuwa na vijana wengi, utendaji na ufanisi wake upo wapi? Haya ndiyo madhara ya kulindana na kubebana."

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM), Dk Benson Bana alisema si lazima rais kuwa mwenyekiti wa chama.

Hata hivyo, akasisitiza kwamba:" Hakuna utata wowote kwa rais ambaye anatokana na chama tawala pia kuwa mwenyekiti."

Dk Bana, ambaye ni mtaalamu aliyebobea katika masuala ya sayansi ya siasa, alifafanua kwamba kitendo cha rais kuwa na kofia mbili kinasaidia kuondoa migongano baina ya chama na serikali hasa katika nchi ambazo ni changa kidemokraia na mifumo ya utawala.

"Kutokana na uchanga wa mifumo ya utawala na masuala ya demokrasia katika nchi nyingi za bara la Afrika na hata Tanzania ni muhimu Rais akawa pia ni mwenyekiti wa chama ili aweze kudhibiti migongano ndani ya chama na pia kati ya chama na serikali. Lakini sio lazima rais awe ni mwenyekiti na pia sio mfumo mzuri," alisema Dk Bana.

Mtaalamu huyo alisema katika nchi zilizo na mifumo imara ya utawala na demokrasia, rais anaweza asiwe mwenyekiti wa chama.

Akizungumza hivi karibuni kuhusu viongozi kuwa sehemu ya mihimili ya nchi (Bunge na serikali) na hasa mawaziri, mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango alisema ni muhimu mfumo ukabadilishwa ili mawaziri wasitokane na wabunge.
Tags:

0 comments

Post a Comment