Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Kauli ya Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar kuwa Rais Kikwete ni Chaguo la Mungu imesababisha uhamisho wake

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter

Kauli ya "Kikwete chaguo la Mungu" bado yamuandama

Ukabila, umaarufu navyo vyazungumzwa

UHAMISHO wa aliyekuwa Askofu Msaidizi wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mhashamu Methodius Kilaini, kwenda kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo la Bukoba, umehusishwa na mambo mengi ikiwamo siasa za kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 na sintofahamu kati yake na wenzake ndani ya kanisa hilo, imefahamika.

Habari za ndani ya Kanisa Katoliki, zimethibitisha kuyumba kwa mahusiano kati ya Askofu Kilaini na wenzake ndani ya Jimbo Kuu la Dar es Salaam kutokana na sababu za kimfumo na kuchochewa zaidi na mahusiano binafsi ya viongozi wakuu ndani ya Kanisa hilo lenye nguvu na wafuasi wengi nchini.

Askofu Kilaini amekuwa kiongozi anayesikika zaidi kutoa matamko kwa niaba ya Kanisa Katoliki nchini, na inaelezwa kuwa hii ni moja ya sababu zilizomuondoa ikidaiwa kwamba baadhi ya matamko aliyotoa hayakuwa na baraka za viongozi wenzake na hiyo imekuwa ikiwakera wenzake ndani ya mfumo wa kanisa hilo.

Kabla ya kuteuliwa kuwa Askofu Msaidizi kumsaidia Askofu Mkuu wa Jimbo hilo, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Askofu Kilaini alikuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki (TEC), nafasi ambayo ilikuwa ikimpa fursa ya kuwa msemaji wa Baraza la Maaskofu, na kwamba “aliizoea nafasi hiyo hata baada ya kuondoka”.

Ukiacha mambo hayo ya ndani, taarifa zinasema Askofu Kilaini atakuwa pia ameponzwa na kauli yake aliyotoa baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005. Akizungumzia matokeo ya uchaguzi huo, baada Jakaya Kikwete kupita kwa kura nyingi, Kilaini alikaririwa akisema Rais Jakaya Kikwete, alikuwa ni “chaguo la Mungu” kwa Watanzania. Kauli hiyo iliwakera baadhi ya viongozi na waumini walioanza kuona kuwa Kanisa linakuwa karibu kabisa na uongozi wa kisiasa.

Hata hivyo, Askofu Kilaini ambaye katika siku za karibuni naye amekuwa haisemi vizuri Serikali ya Kikwete, akijitetea kuhusu kauli yake ile, alisema maandiko yanaainisha kwamba kiongozi yeyote anayechaguliwa kwa ridhaa ya wananchi walio wengi anakuwa ni “chaguo la Mungu”.

Pamoja na utetezi huo wa Kilaini, bado amekuwa akisakamwa kwa kauli yake hiyo ambayo ilihusishwa pia na safari yake ya matibabu India, Septemba 2007, ambayo inaelezwa ya kuwa ilifadhiliwa na Rais Kikwete binafsi. Kauli na safari hii vimekuwa kayi ya vyanzo vya ufa kati yake na viongozi wenzake wa Kanisa, wakimwona kuwa amekwenda kinyume cha mambo kwa kuwa, kwa mfano, Kanisa lisingeshindwa kumlipia matibabu nje, ama hata kama ingebidi, basi angefadhiliwa na Serikali badala ya Rais Kikwete binafsi.

Akofu Kilaini hakuweza kupatikana wiki hii kuzungumzia kuhamishwa kwake, lakini watu wanaomfahamu wamethibitisha kuyumba kwa mahusiano yake na wenzake kutokana na sababu kadhaa, zikiwamo za kiutendaji na sababu nyingine binafsi.

Sababu za kiutendaji zinazotajwa kumponza Askofu Kilaini ni pamoja na wasiwasi wa viongozi wenzake kwamba anaweza “kutumiwa na wanasiasa” katika mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa 2010 kutokana na mahusiano yake ya karibu na wanasiasa wengi pamoja na kuwa karibu na vyombo vya habari.

Imeelezwa kwamba sababu binafsi zilizoyumbisha mahusiano yake na wenzake ni pamoja na madai ya kuwapo ukabila katika maamuzi yake mengi ikiwamo kuwaingiza watu kutoka mkoani Kagera katika nafasi nyingi za Kanisa ya Dar es Salaam na watendaji katika asasi kadhaa japo watu wanaomfahamu kwa karibu wameeleza ya kuwa madai hayo yametokana na chuki binafsi walizonazo baadhi ya wenzake.

Ndani ya Kanisa Katoliki kumekuwapo na maswali mengi yanayoulizwa baada ya kutangazwa kwa uhamisho wa Askofu Kilaini ikiwa ni pamoja na wanaohoji kama atateuliwa Askofu Msaidizi mwingine badala yake kumsaidia Pengo.

“Kawaida Askofu Msaidizi anaombwa. Ina maana Pengo, aliomba kuwa na Askofu Msaidizi. Je, sasa ameona hana haja tena kuwa na Askofu Msaidizi? Je, Askofu wa Bukoba ameomba kuwa na askofu Msaidizi? Maana ni lazima aombe!” Alihoji msomaji mmoja wa Raia Mwema lakini ambayo ni miongoni mwa waumini wa Kanisa Katoliki nchini na anayemfahamu vyema Askofu Kilaini.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana Askofu Msaidizi hawezi kuhamishwa kwenda kwingine kama si kupanda daraja na hivyo kwamba kwa kuwa Kilaini alikuwa Askofu Msaidizi Dar es Salaam kuhamishwa kwake kwenda kuwa Askofu Msaidizi wa Bukoba ambako si Jimbo Kuu kama Dar es Salaam ni jambo jipya katika mfumo wa Kanisa Katoliki.

“Hili ni jambo jipya. Maana baada ya kuwa Askofu Msaidizi kwa miaka 10 ilitarajiwa awe Askofu Kamili au awe Askofu Msaidizi Mrithi. Kwa vile ni Askofu Msaidizi, hata akifa Askofu wa Bukoba, si lazima Kilaini awe Askofu wa Jimbo la Bukoba, maana yeye si Askofu Msaidizi Mrithi,” anasema muumini huyo.

Lakini baadhi ya watu wa ndani ya Kanisa Katoliki wamekuwa wakiamini kwamba uhamisho huo una nia njema na unalenga kumpandisha ngazi Askofu Kilaini ama pia kumsogeza karibu na nyumbani kwake apate kupumzika kutokana na kuyumba kwa afya yake.

Hoja nyingine inayojadiliwa ni kwamba Askofu Kilaini anaweza kuwa anaandaliwa kuwa Askofu Mkuu wa Mwanza, na kwamba kwenda kwake Kanda ya Ziwa kunamsogeza zaidi karibu na nafasi hiyo kwa kuwa kwa kawaida nafasi ya kwanza ya uteuzi wa Askofu wa Mwanza itatolewa kwa ya mtu mwenye sifa aliyeko Kanda ya Ziwa.

Taarifa ya Kanisa Katoliki iliyosainiwa na Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Padre Anthony Makunde ilieleza kwamba Baba Mtakatifu, Benedicto wa 16, amemhamisha Askofu Kilaini, kwenda kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo la Bukoba.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Askofu Kilaini, ambaye amekuwa akimsaidia Askofu Mkuu Jimbo Kuu la Dar es Salaam kwa miaka mingi, ameruhusiwa kuendelea kushika Kiti cha Jimbo la Strumnizza.

Aliteuliwa kushika nafasi ya Askofu Msaidizi Jimbo Kuu la Dar es Salaam na Baba Mtakatifu, Yohane Paulo wa Pili.

Kilaini amekuwa mmoja wa viongozi wa dini anayesikika sana katika vyombo vya habari na alikuwa mmoja wa wachangiaji wakubwa waliozungumza katika kongamano la Mwalimu Julius Nyerere, lililofanyika jijini Dar es Salaam hivi karibuni akiifananisha nchi ilivyo na mtu anayetembea bila nguo.

Miongoni mwa vichwa vya habari vilivyotikisa vikimnukuu Askofu Kilaini ni pamoja na:

“Askofu Kilaini atoa angalizo uchaguzi mkuu ujao; Askofu Kilaini: 2009 punguzeni pombe; Mafisadi EPA warejeshe riba pia - Askofu Kilaini; Askofu Kilaini, si ufisadi tu, yako mengi; Askofu Kilaini: Kikwete ameelemewa na mafisadi; Askofu Kilaini: Kingunge anajadili hewa.”

Kanisa Katoliki limeandaa na kusambaza nyaraka zake maalumu kuhusiana na Uchaguzi Mkuu wa 2010, Askofu Kilaini akiwa mmoja wa washiriki wakuu katika maandalizi na uhamasishaji wa yaliyomo ndani ya nyaraka hizo zilizowakera wanasiasa wengi na kuibua mjadala mkubwa katika jamii.

Tags:

0 comments

Post a Comment