Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Inabidi viongozi wa Tanzania tumuige Rais Museveni wa Uganda...

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
Museveni asafiria daraja la walalahoi akitokea London
Na Mwandishi Wetu

VIONGOZI wa Afrika wamezidi kuchukua hatua za kupunguza gharama kwenye matumizi ya safari za nje baada ya Rais wa Uganda, Yoweri Museveni kuamua kusafiri kutoka London hadi Entebbe akiwa amepanda daraja la tatu kwenye ndege ya kibiashara.

Museveni, mpiganaji aliyetokea msituni hadi Ikulu ya Uganda, anakuwa kiongozi wa pili kuchukua hatua ya kupunguza gharama za safari za nje baada ya Bingu wa Mutharika wa Malawi ambaye aliamua kutoenda kuhudhuria mkutano wa Jumuiya ya Madola ili kuokoa mamilioni ya fedha za walipa kodi.

Chama tawala cha Uganda kilieleza kufurahishwa na hatua hiyo ya Rais Museveni ambaye msemaji wake alieleza kuwa amesafiri kwa kutumia daraja la tatu akiwa na nia ya kuonyesha mfano kwa maofisa wa serikali wanaolalamika kuwa usafiri huo haufai.

Lakini BBC, baada ya kuongea na watu kadhaa, iliripoti kuwa wananchi wanachukulia uamuzi huo wa kusafiria daraja la chini ni kampeni za kisiasa.

Kwa mujibu wa BBC ndege mtumba ilinunuliwa mwaka jana, kwa ajili ya safari za rais huku wapinzani wakipinga kitendo hicho.

Kwa mujibu wa msemaji wa rais, Tamale Mirundo, rais alisafiri Jumapili kutoka London hadi Entebbe akiwa amepanda daraja hilo.

Alikuwa akirejea nyumbani baada ya safari ya wiki mbili nje ya nchi ambako alihudhuria mkutano wa viongozi wa nchi za Jumuiya ya Madola nchini Trinidad & Tobago.

"Alipewa huduma kama wasafiri wengine," Mirundi aliliambia gazeti la serikali la Uganda, New Vision.

"Kama rais anaweza kusafiri kwa daraja la tatu, ni ishara kwamba matumizi ya fedha nyingi yanayofanywa na maofisa wa serikali yataisha," alikaririwa na gazeti hilo.

"Alitaka kujua matatizo ambayo wasafiri wanakabiliana nayo wanapopanda daraja la tatu na sababu za maofisa wa serikali kulalamikia daraja hilo."

Katika hatua za karibuni kumekuwepo na jitihada za baadhi ya viongozi wa nchi za Afrika kupunguza matumizi ya serikali, hasa kwenye safari za nje.

Rais wa Malawi,Bingu wa Mutharika aliamua kutoenda Trinidad & Tobago, akieleza kuwa amechukua uamuzi huo ili kupunguza matumizi ya serikali. Alifanya uamuzi huo siku chache baada ya kutangaza kupunguza safari za nje za mawaziri, makatibu wa wizara na maofisa waandamizi wa serikali hadi kufikia sita kwa mwaka.

Tags:

0 comments

Post a Comment