Balozi Karume ashangaa kutounda serikali ya mseto Zanzibar |
Geofrey Nyang'oro BALOZI Ali Abeid Karume, amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inasifa zote za kuunda serikali ya mseto na kwamba, akichaguliwa na CCM kumrithi kaka yake atahamasisha iundwe serikali ya mseto kwa kushirikiana na Chama cha Wananchi (CUF). Wadau mbalimbali, wakiwemo wanazuoni, viongozi wakuu wastaafu na wanadiplomasia wamekuwa wakitaka kuundwa kwa serikali ya mseto Zanzibar, kama suluhu ya mpasuko wa kihistoria visiwani humo. Wakati tayari CUF imemtambua Rais wa sasa Aman Abeid Karume, akizungumza katika mahojiano maalumu na Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Ujerumani, mdogo huyo wa Rais Karume, alisema siyo haki kwa wakazi wa kisiwa hicho cha Pemba kutohusishwa ndani ya serikali kutokana na msimamo wao wa kuwachagua wagombea wa chama cha CUF. Balozi Karume alifafanua kwamba, kufanya hivyo kutasaidia kuleta umoja na na mshikamano miongoni mwa Wanzibari, ambao tangu kufanyika kwa uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995, chuki ilijengeka miongoni mwao. Alisema jamii inapaswa kubadilika na kutambua kuwa siasa siyo ugomvi bali wanapaswa kuzidisha ushirikiano baina yao na kuongeza kwamba anawasikitikia wote wanaopinga wazo hilo. "Siyo haki kwa watu walioko Pemba ambao wamejiunga na kuchaguana kwa umoja wao kiasi kile halafu wakakosa uwakilishi kwenye serikali yao," alisema Karume. "Mimi nikichaguliwa nitakishawishi chama changu kikubaliane na dhana ya kuundwa kwa serikali ya mseto Zanziba," alisema Balozi huyo, alieleza kufurahishwa na hatua ya maridhiano yaliyofikiwa na Rais wa sasa na mwenzake Katibu Mkuu wa CUF, Maalimu Seif Sharif Hamad. |
You Are Here: Home - - Balozi Karume ashangaa kutounda serikali ya mseto Zanzibar
IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
0 comments