You Are Here: Home - HABARI ZA MICHEZO - Kaseja, Sunguti watemwa Yanga
IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
SIKU saba kabla ya kumalizika kwa mkataba wake wa mwaka mmoja, Kocha wa Yanga, Dusan Kondic amemtema rasmi kipa wake, Juma Kaseja.
Kaseja, aliyesajiliwa na Yanga kwa kitita cha dola 30,000 (Sh milioni 36) msimu uliopita ni miongoni mwa majina matano ambayo Kondic ameyapeleka kwa uongozi kuwa waachwe.
Pamoja na Kaseja, Yanga imewatema washambuliaji wake wawili, Gaudence Mwaikimba na mkongwe, Maurice Sunguti aliyeibuka mfungaji bora na kinara wa mabao misimu miwili iliyopita.
Kondic pia amewatema wachezaji wawili watoro sugu, Laurent Kabanda ambaye alikwenda kwao Congo na Credo Mwaipopo aliyetoka kwenda Sweden kabla ya kurejea miezi kadhaa iliyopita.
Habari za uhakika kutoka Yanga zinasema kuwa kikao cha juzi Alhamisi cha uongozi, kocha Kondic na mfadhili, Yusuf Manji umepitisha uamuzi huo na majina hayo matabo yatatangazwa wakati wowote kuwa wameachwa.
Habari hizo zenye uhakika ni kuwa Yanga imemuacha Kaseja baada ya Kondic raia wa Serbia kumuweka katika orodha ya wachezaji asiowahitaji tena kwa ajili ya msimu ujao na hasa baada ya kupata habari kuwa kipa wake wa Serbia, Obren Curkovic anarejea.
Kondic amefanya hivyo ikiwa ni siku chache baada ya kuiambia Mwanaspoti kuwa kipa namba moja wa Simba, Ally Mustapha 'Barthez' ni bora kuliko Kaseja.
Katika kikao hicho, Mserbia huyo aliueleza uongozi huo kwamba pamoja na ubora wa Kaseja katika mambo mengine lakini kasoro ya umbo na hasa ufupi ndio kimefanya asitake kuendelea naye.
Kondic alisema hakuwahi kumtaka Kaseja na hata msimu uliopita alitua Jangwani kutokana na siasa za Yanga na Simba, lakini halikuwa chaguo lake.
Tayari kocha huyo ameanza mipango ya kuhakikisha wanasajili kipa mwingine hapa nchini lakini ikiwa ni baada ya kurejea kwa kipa Mserbia, Obren Curkovic ambaye aliondoka nchini kwa hofu ya vitisho na kwenda kwao Serbia, baadaye Austria kufanya majaribio ambako anaelezwa ameshindwa.
Kwa upande wa Mwaikimba na Sunguti, Kondic alikieleza kikao hicho kwamba wameshindwa kuonyesha mchango wowote hata pale alipowapa nafasi ya kufanya hivyo, lakini Sunguti ikiwa ni kutokana na umri kumtupa mkono.
Kondic amekieleza kikao hicho kwamba, kitu muhimu kwa Yanga ni kufanya usajili wa wachezaji wachache tu huku akisisitiza kuwa Nurdin Bakari 'Kibajaji', Ben Mwalala na Mike Baraza hawatakwenda popote kwani anawahitaji kwa msimu ujao.
Kondic amewaweka mabeki Yusuf Hamis na Abuu Mtiro na Mkenya, George Owino katika orodha ya wachezaji watakaouzwa kwa kuwa bado wana mkataba na jeshi hilo la Jangwani.
Wengine ambao Kondic amewaweka katika orodha ya kuuzwa nje ya nchi ni Nadir Haroub 'Cannavaro' (Vancouver-Canada), Shadrack Nsajigwa (Ufaransa) na Boniface Ambani (China).
Akizungumza na Mwanaspoti jana Ijumaa, Katibu Mkuu wa Yanga, Lucas Kisasa alikiri kuwa na kikao hicho na kusema kilihusu mambo ya Yanga na si kwa ajili ya taarifa kwenye vyombo vya habari.
"Kweli tumekutana, lakini ilihusu mambo ya Yanga na tusingependa yazungumziwe hadharani. Tukiwa tayari tutawaita na kuwaeleza," alisema Kisasa.
Lakini kwa upande wa Kondic alisisitiza kwamba, usajili mpya hautakuwa na mabadiliko makubwa kama wengi wanavyofikiri.
"Kweli tulikutana, lakini ni mambo yetu ya ndani ukiwamo usajili. Tumejadili mengi ukiwamo usajili, kweli kuna ambao wataachwa, wengine watauzwa na wengine tunawasiliana nao kwa ajili ya usajili.
Ila hatutakuwa na mabadiliko makubwa kwa kuwa tuna wachezaji wa kutosha na kumbuka kuna Joseph Shokokoti na John Njoroge ambao wako Tusker kwa mkopo. Pia tuna chipukizi wetu ambao tuliwapandisha mwaka jana. Hivyo ni sehemu chache tutaongeza.
Mwanaspoti ilimsaka mfadhili Mkuu wa Yanga, Yusuf Manji ambaye alimsajili Kaseja mwaka jana na kuweka rekodi ya usajili kwa wachezaji wandani ikiwa ni pamoja na kumpa mshahara wa Sh milioni moja ambaye alisema suala hilo ameachiwa Kondic.
"Tunaweza kusajili mchezaji yeyote kama anaweza kuisaidia Yanga hata kama itakuwa Sh milioni 50, lakini kocha ndiye anatuelekeza wapi twende kwenye hili. Hivyo kama kumbakiza au kumuacha mchezaji ni suala la kocha," alisema Manji.
Akizungumza jana kuhusu hilo, Kaseja alisema hawezi kuzungumzia suala hilo kwa kirefu kwa kuwa ameelekeza nguvu zake kwenye mechi ya leo Jumamosi ya fainali ya Kombe la Taifa.
"Mkataba haujaisha nitakuwa nimeachwa vipi, hapo sielewi lakini naomba mnipe muda kwa kuwa nikiamua kuzungumza nitakuwa na mengi tu. Ila naelekeza nguvu zangu katika mechi ya kesho (leo Jumamosi) ya Taifa Cup baada ya hapo naweza kuzungumza vizuri," alisema Kaseja ambaye ndiye kipa bora namba moja nchini.
0 comments