Mageuzi katika siasa ya kigeni ya Marekani chini ya Barack Obama
Vita katika Iraq na Afghanistan, mivutano baina ya Pakistan na india, mapigano baina ya Israel na Wapalastina, mzozo wa kinyukliya na Iran na uhusiano uliozorota na Russia- orodha ni ndefu ya shughuli za siasa za kigeni ambazo zinaingojea serekali mpya ya Rais Barack Obama huko Marekani. Ni muhali kabisa kwa mithani yote hiyo kukabiliwa na kutanzuliwa kwa wakati mmoja, hasa kutokana na mzozo wa sasa wa kifedha na matatizo yalioko ndani kwenyewe Marekani ambayo pia yatataka yazingatiwe na rais mpya. Hata hivyo, timu ya Barack Obama inayoshughulikia siasa za kigeni zamani imeshaanza kazi, na waziri wa mambo ya kigeni mteulie, Hilary Clinton, alipohojiwa na Baraza la Senate la Bunge la Marekani, alidhihirisha kwamba siasa ya kigeni ya Marekani itaanzisha enzi mpya.
"Marekani haiwezi pekee kuyatanzuwa matatizo makubwa ya dunia, na dunia haiwezi, bila ya Marekani, kuyatanzuwa matatizo hayo."
Badala ya kufuata siasa ya kujiamuliya mambo wenyewe tu na yenye misimamo ya kinadharia, sasa Marekani itafuata siasa ya kutumia mamlaka yake kwa uangalifu.
"Lazima tuendeshe siasa ya kutumia mamlaka kwa uangalifu, kutumia njia zote tulizo nazo, za kibalozi, kiuchumi, kijeshi, kisiasa, kisheria na kitamaduni. Katika hali ya mambo lazima tutumie njia ifaayo au tuchaguwe mchanganyiko mzuri wa njia mbali mbali."
Lakini wachunguzi wa mambo huko Marekani wanasema Barack Obama katika hotuba yake ya mwanzo atakapokamata madaraka ataweka wazi kwa dunia kwamba Marekani itaendesha pia siasa yake ya kigeni kwa vitisho na pia kwa sauti laini. Kwanza kabisa katika mzozo baina ya Israel na Wapalstina, hali katika Ukanda wa Gaza itabidi itulizwe; mapigano yakomeshwe na vyakula na bidhaa nyingine ziweze kuingia katika eneo hilo. Allen Leiswetter wa Taasisi juu ya Mashariki ilioko Washington anasema jambo hilo linawezekana kwa kuwekwa wanajeshi wa kimataifa katika eneo hilo:
"Katika hatua ya pili, mazungumzo ya amani baina ya Israel na Wapalastina lazima yarejewe tena. Kwa pande zote mbili ni muhimu kwamba ziwe na matarajio ya kuwa na amani."
Ni hapo ndipo kutakapokuweko nafasi ya kuutanzuwa mzozo huo, ikiwa si kwa muda mfupi ujao, basi katika miaka au miongo ijayo. Hadi sasa nia ya kisiasa imekosekana katika pande zote mbili. Bwana Allen Keiswetter anasema kwamba kwa mtizamo wa muda mrefu ujao, ni tu Wapalastina wanaoweza kuwapa Wa-Israeli kile wanachokitaka, nacho ni amani, na ni Wa-Israeli tu wanaoweza kuwapa Wapalastina kile wanachotaka, nacho ni aina ya nchi.
Lakini vita baina ya Israel na Wapalastina ni moja tu ya matatizo ya Mashariki ya Kati, ambayo yametanda baina ya Iraq hadi India.
" Nafikiri Iran ndio mtuihani mkubwa kabisa kwetu. Kama vile nilivosema wakati wa kampeni za uchaguzi, Iran inasafirisha ngambo sio tu ugaidi, kwa msaada wa vyama vya Hamas na Hizbullah, lakini inawania kuwa na silaha za kinyukliya. Mkakati wetu lazima ugeuke. Kuwa na mdahalo ni mwanzo mzuri."
Wahakiki wanakubaliana kwamba vita vya Iraq, ambavyo vilitawala katika kampeni za uchaguzi, sasa sio jambo linalowashughulisha sana wananchi, kwa vile utumiaji nguvu umepungua sasa katika nchi hiyo na hali ya usalama imeboreka. Na zaidi ni kwamba sasa kuna mkataba wa kijeshi ambao unataja kwamba majeshi ya Kimarekani yataondoka kutoka nchi hiyo ifikapo mwaka 2011.
Barack Obama ametangaza kwamba atavishughulikia zaidi vita vya Afghanistan, lakini serekaliya nchi hiyo inatuhumiwa kuwa imezongwa na ufisadi na rushwa na imepoteza uhalali wake.
Licha ya mizozo ya Mashariki ya Kati, Iran, Iraq na Afghanistan, Barack Obama anarithi mitihani ya siasa za kigeni, kama vile mvutano katika uhusiano na Uchina, Korea Kaskazini au Russia. Lakini rais huyo hawezi kulishughulikia tatizo moja tu.
0 comments