Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - ‘Tutafuatilia mabilioni ya Uswisi, Serikali ikishindwa’

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe, amesema Bunge litaunda kamati ya kufuatilia vigogo walioficha mabilioni ya fedha nchini Uswisi, kama Serikali ikishindwa kuwasilisha taarifa ya uchunguzi wake katika mkutano wa Bunge unaoendelea mjini Dodoma.
Wakati Zitto akisema hayo, Mbunge na mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali, PAC kutoka Sudan Kusini, Goc Mukleac Mayol, alirusha makombora kwa wahisani na nchi zilizoendelea, akiwatuhumu kuwafundisha Waafrika tabia ya wizi na ufisadi wa fedha na rasilimali za umma.
Kabwe ambaye yuko mjini Arusha kuhudhuria mkutano wa wabunge wa Kamati ya Hesabu za Serikali katika nchi za Kusini mwa Afrika (Sadcocap), alisema kwa mujibu wa maazimio ya Bunge, Serikali inapaswa kuwasilisha taarifa yake katika mkutano wa sasa.
“Awali taarifa ilikuwa iwasilishwe katika mkutano wa Bunge la mwezi wa nne, ikasogezwa mbele hadi Bunge la Bajeti, lakini wakaomba taarifa iwasilishwe katika Bunge hili. Hata hivyo kwenye ratiba ya vikao vya Bunge linaloendelea, taarifa ya Serikali kuhusu walioficha fedha Uswisi haipo,” alisema mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini.
Alisema hata hivyo, anaamini taarifa hiyo itawasilishwa bungeni kwa kuzingatia kuwa uchunguzi unakwenda vizuri na kwamba imebainika kuwa fedha za aina hiyo, zimefichwa pia katika benki za Dubai na Mauritius.
“Binafsi nimekutana nao wachunguzi, wamefanya kazi nzuri sana. Kuna fedha nyingi katika nchi za Dubai na Mauritius tena zimewekwa katika miaka ya karibuni,” alisema Kabwe.
Alisema katika hoja yake kuhusu fedha hizo, Bunge liliagiza Serikali kufanya uchunguzi na kupeleka taarifa bungeni kwa hatua zaidi.
Naye Mayol akichangia mada kuhusu utorashaji wa fedha za umma na ukwepaji kodi Afrika, alisema ni tabia ya wizi na ufisadi haukuwahi kuwa sehemu ya utamaduni ya Mwafrika bali imerithiwa kutoka kwa baadhi ya watawala wa kikoloni wanaoendelea kutumia uwezo wa kiuchumi wa nchi zao na uelewa mdogo wa Waafrika kupora fedha na rasilimali kuzihamishia nchini mwao.
Hoja hiyo ilionekana kuchafua hali ya hewa ukumbini kiasi cha aliyekuwa Mwenyekiti wa kikao wakati huo, Nehemiah Modubule ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa SADCOPAC, kuingilia kati kumtaka asubiri mada inayofuata ya Zitto Kabwe inayozungumzia utoroshaji wa fedha na rasilimali nje ya Afrika.
Mayol aliyeonekana kuzungumza kwa hisia kali aliwambia wajumbe zaidi ya 300 wa mkutano wa kumi wa umoja wa SADCOPAC, kuwa kwa kawaida kijana mdogo (mtoto), hawezi kuwa mwizi hadi pale anapofundishwa na kaka yake, akihusishwa mfano huo na tabia ya wizi Afrika kuigwa kutoka kwa nchi zilizoendelea.
Akiwasilisha mada ya utorashaji wa fedha na rasilimali za umma nje ya nchi zinazoendelea, Mwenyekiti wa PAC Tanzania, Zitto Kabwe aliunga mkono hoja ya mbunge Mayol kwa kusema kati ya mwaka 2000-210 zaidi ya dola dola za Kimarekani 844 bilioni zilitoroshwa kutoka nchi zinazoendele kwenda nchi za Ulaya na Marekani huku asilimia 69 sawa na dola za bilioni 582 zikitoroshwa kutoka barani Afrika.
Kwa mujibu wa Zitto ambaye ni mbunge Kigoma Kaskazini (Chadema), njia zinazotumika kutorosha fedha na rasilimali za nchi zinazoendelea zikiwemo za Kiafrika ni pamoja na wizi, rushwa, bakshishi kupitia mikataba ukwepaji kodi na ushushaji thamani wa bidhaa maligafi kutoka Afrika.

0 comments

Post a Comment