Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA LEO , LEO KATIKA MAGAZETI - Dk Ndalichako: Siasa zisipewe nafasi kwenye mitihani yetu

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
Arusha. Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), Dk Joyce Ndalichako amesema siasa hazipaswi kupewa nafasi katika mchakato wa usimamizi wa mitihani na kwamba athari za mwenendo wa aina hiyo ni kubwa kwa taifa.
Dk Ndalichako alisema akiwa kiongozi wa Necta hapendi ifike mahali ambako kila mtu atatakiwa afaulu hata kama hana sifa kwani madhara yake yatakuja kuonekana kwenye rasilimali watu siku zijazo.
Akizungumza katika mahojiano maalumu Arusha hivi karibuni alisema: “Tukiruhusu mitihani iingiliwe na wanasiasa tutakuwa tunajimaliza wenyewe, kama ni wanasiasa wafanye kazi ya kushauri halafu waache wanataaluma husika wafanye kazi yao.
“Wanaohusika na kutunga sheria watekeleze jukumu lao siyo kuingilia moja kwa moja suala la mitihani. Sisemi kuwa tuachwe tu tufanye kazi kama tunavyotaka, ikibidi kuwe na chombo cha wanataaluma kutukagua, kwa sababu hii ni taaluma siyo kitu cha kila mtu kuingilia.
“Madhara ya kuingilia mitihani matokeo yake yataweza kuja kuonekana baada ya miaka hata 10 ijayo, ili kukwepa hali hiyo, kila mtu afanye kazi yake kama itaonekana watendaji hawana sifa waondolewe wawekwe wengine wenye sifa.”
Dk Ndalichako ambaye hivi karibuni alichaguliwa kuongoza Mabaraza ya Mitihani Afrika (AEAA) alisema: “Mtu akipewa alama asizostahili na akawa mwalimu atawafundisha nini watoto? Hawa ndiyo utakuta wana sababu zisizokwisha, kila siku utamsikia akisema watoto wa siku hizi hawaelewi kabisa.” 
Dk Ndalichako pia alipinga mawazo kwamba Necta inapaswa kushirikiana na wadau wa elimu katika kila kitu. Alisema ni hatari... “Tusifike mahali tuambiwe tuwaulize watoto tuwaletee maswali gani kwenye mtihani.”
Kauli ya Dk Ndalichako imekuja wakati taifa likiendelea kuugulia maumivu yaliyotokana na matokeo mabaya ya mitihani ya kidato cha nne ya 2012 ambayo karibu nusu ya wanafunzi walifeli. Matokeo hayo yaliifanya Serikali kuunda tume iliyoogozwa na Katibu Mkuu wa sasa wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome ambayo ilipendekeza matokeo hayo yafutwe na yapangwe upya, hatua ambayo wengi waliita ni ya kisiasa.
Mahojiano kati ya Dk Ndalichako
Swali: Hii ni mara ya tano kwa Necta kuwa mwenyeji wa mkutano wa AEAA, na pia mmekuwa mkihudhuria mikutano kama hii inapofanyika nje ya nchi, ni nini hasa mmeona kuwa ni changamoto kwa mitihani inayotungwa katika ngazi ya shule?
Jibu: Hii mitihani inayotungwa shuleni ni changamoto sana, lakini ukiangalia utagundua kuwa tatizo lipo kwenye mitalaa ambayo walimu wanafundishiwa. Huko suala la ufundishaji limetiliwa mkazo sana lakini lile la kuwapima watoto halijapewa kipaumbele kabisa. 
Wanachofundishwa huko ni kama orientation (utangulizi) tu, walimu wanatakiwa wajue mbinu gani zitumike kutunga mitihani.

Source: Mwananchi

0 comments

Post a Comment